Saturday, December 28, 2024

KUKAMILIKA KWA UJENZI WA BARABARA YA MWERA- POLICE HADI KIBONDE MZUNGU KUTASAIDIA KUKUWA KWA UCHUMI WA NCHI


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Baraza ya Mwera-Polisi - Kibonde Mzungu ikiwa ni katika shamra shamra za kuadhimisha kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Mtukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Mwera- Police hadi Kibonde Mzungu kutasaidia kukuwa kwa uchumi wa nchi pamoja na kuongezeka kwa thamani katika vijiji vilivyopitiwa na Baraza hilo.

Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Baraza ya Mwera-Polisi - Kibonde Mzungu uliofanyika katika viwanja vya Mwera Polisi ikiwa ni katika shamra shamra za miaka 61 ya Mapinduzi maatukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Amesema ukuaji wa uchumi katika nchi na kuwepo kwa maendeleo endelevu kunategemea uwepo wa miundombinu bora na Imara inayojengwa na serikali kwa maslahi mapana ya wananchi ikiwemo miundombinu ya Barabara na mengineyo.

Makamu wa Pili wa Rais amesema kila mwananchi ana wajibu wa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Mwinyi za kuwaletea wananchi maendeleo ambapo katika sekta ya Miundombinu ya Barabara jumla ya kilomita 897.2 zimejengwa kwa kiwango cha lami mijini na vijijini na kupitiliza agizo la Ilani ya Uchaguzi lililoitaka Serikali kujengwa kilomita 196.7 za Barabara.

Mhe. Hemed amesema kuwa kuwepo kwa babarara hio kunaendana na fikra na falsafa za muasisi wa mapinduzi na Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karume za kuwarahisishia wananchi kupata huduma zilizobora na kukuza uchumi wa wananchi wote wa unguja na pemba.

Mhe. Hemed amewataka wananchi wa maeneo hayo na maeneo jirani kutoa ushirikiano katika kuilinda miundombinu mbali mbali ya maendeleo pamoja na kuwataka madereva na watumiaji wa barabara hio kufuata sheria za usalama barabarani ili kupunguza wimbi na ongezeko la ajali pamoja na kutokufanya uharibifu wa barabara hizo ili iweze kufikia malengo ya ujenzi huo.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameendelea kuwasisistiza wananchi wa Zanzibar kuendelea kudumisha Amani na mshikamano uliopo nchini ili kuweza kupiga hatua zaidi kimaendeleo kwa maslahi mapana ya Taifa.

Nae Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi Mhe.Dkt Khalid Salum Muhammed amesema Serikali ya Awamu ya Nane (8) katika kuhakikisha Zanzibar inaimarika na kuzidi kupiga hatu kimaendeleo imedhamiria kujenga barabara zenye urefu wa zaidi kilomita 897.2 ambapo wananchi wa Jimbo la Mwera na Jimbo la Fuoni wamenufaika na ujenzi wa barabara ya Mwera - Kibonde Mzungu.

Mhe. Dkt Khalid amesema wajenzi wa barabara hio kutoka kambuni ya Iris wameihakikishia Serikali kuwa ujenzi wa barabara ya Mwera hadi Kibonde Mzungu umezingatia viwango na ubora unaotakiwa utakaoiwezesha Barabara hio kudumu zaidi ya miaka 35 endapo itafanyiwa matengeneze kwa ndani ya muda uliopangwa na wakandarasi.

Akitoa taarifa ya kitaalamu juu ya ujenzi wa Barabara ya Mwera - kibonde Mzungu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiano na Uchukuzi Dkt.Habiba Hassan Omar amesema barabara hiyo yenye urefu wa Kilomita 6.1 iliyojengwa na Mkandarasi Kampuni ya Iris na kusimamiwa na Mshauri elekezi mzalendo kutoka wakala wa Barabara (ZANROD) hadi kumalizika kwake imegharimu zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 80 ambazo gharama hizo ni fedha kutoka Serikalini.

Dkt. Habiba amesema katika kipindi cha miaka minne(4) ya uongozi wa serikali ya awamu ya nane (8) imejipanga kuzisanifu na kuzijenga barabara za ndani mijini na vijijini kwa kiwango cha lami Unguja na Pemba zenye jumla ya kilomita 225.9 ambazo zitasaidia upatikanaji wa huduma bora za kiuchumi na kijamii kwa wakati.

Dkt. Habiba ameishukuru Serikali kwa kuiwezesha Wizara ya Ujenzi, Mawasiano na Uchukuzi kuendelea kuzijenga barabara za ndani Unguja na Pemba sambamba na kuwashukuru wananchi waliopitiwa na ujenzi wa miundombino ya Barabara katika maeneo yao kuweza kutoa ushirikiano kwa Wizara na wakandarasi katika kuhakikisha barabara hizo zinakamilika ndani ya wakati uliopangwa.

Imetolewa na Kitengo Cha Habari ( OMPR)
Leo tarehe ..27 / 12 / 2024

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake