Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu. Hemed Suleiman Abdulla amesema Chama cha Mapinduzi kinatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na Jumuiya ya Wazazi katika kuimarisha chama ili kiendelee kushikilia dola na kuwaongoza wanachi wa Tanzania.
Ameyasema hayo katika hafla ya kukabidhi Vifaa vilivyotolewa na Mbunge wa Jumuiya ya Wazazi Mhe.Najma Giga kwa Mkoa wa Mjini Kichama iliyofanyika katika Ukumbi wa CCM Amani Mkoa.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema vifaa vilivyotolewa na Mbunge wa Wazazi Mkoa wa Mjini vitatoa matokeo chanya hasa katika mkakati wa kuhakikisha kila anaestahiki kusajiliwa na kuandikishwa katika daftari la kudumu la mpiga kura anapatiwa haki yake hio ili aweze kupiga kura katika uchaguzi ujao.
Mhe. Hemed ameihakikishia Jumuia ya Wazazi kuwa ataendelea kushirikiana nao katika kufanya kazi za Chama cha Mapinduzi ikiwa ni pamoja na kukipambania Chama kuendelea kushinda kwa kishindo katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na chaguzi nyengine zijazo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Chama cha Mapinduzi kitaendelea kushikilia dola na kuongoza kutokana na Sera zake zinazotekelezeka na miradi mbali mbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025.
Nae Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi anaefanyia kazi zake Zanzibar Ndugu. Dogo Iddi Mabruk amesema Jumuiya wa Wazazi imeongoza katika zoezi la uwandikishaji wanachama wapya wa CCM kwa njia ya kielectroniki ambao wataongeza nguvu katika kukipatia ushindi Chama cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Ndugu Dogo amekiomba Chama cha Mapinduzi kuiangalia Jumuiya ya Wazazi katika kuwaongezea nafasi za Wabunge, Wajumbe wa Baraza laWawakilishi na Madiwani kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Jumuiya hiyo.
Kwa upande wake Mbunge wa viti maalum kupitia Jumuiya ya wazazi(MNEC) Mkoa wa Mjini Mhe. Najma Murtaza Giga amesema lengo la kutoa vifaa hivyo ni kuondoa changamoto ya kuzorota kwa utendaji kazi katika jumuiya hiyo sambamba na kuwasisitiza viongozi wa jumuiya kufanya kazi zo kwa weledi mkubwa na umakini.
Mhe. Giga amesisitiza ushirikiano kwa wanachama wa CCM kupitia jumuia mbali mbali na kuacha tabia za makundi na majungu ndani ya jumuiya na badala yake kuunganisha nguvu zao katika kukitumikia chama na kuhakikisha chama cha mapinduzi kinashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020-2025.
Amemuomba Mhe. Makamu wa Pili wa Rais kuwasaidia katika upatikanaji wa Sera ya Malezi ya Mtoto Zanzibar ambayo itasaidia katika kutoa miongozo ya malezi mema na yenye maadili ili kuweza kuwa na kizazi bora kitakacho kitumikia Chama cha Mapinduzi na Taifa kwa uzalendo mkubwa.
Vifaa vilivyotolewa na Mbunge wa Wazazi Mhe.Najma Giga kwa Jumuiya hiyo ni pamoja na gari,viti,rimu za karatasi na simu za mkononi ambavyo vitatumika katika kuongeza ufanisi wa utendaji kazi ndani ya Junuiya ya Wazazi Mkoa wa Mjini.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake