Wednesday, December 11, 2024

RAIS WA ZANZIBAR DK.HUSSEIN MWINYI AMEZINDUA RASIMU YA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akielekea katika ukumbi wa mkutano wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Jijini Zanzibar, kwa ajili ya Uzinduzi wa Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, uzinduzi huo uliofanyika leo 11-12-2024 na (kushoto kwa Rais) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla na (kulia kwa Rais) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Uzinduzi wa Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Jijini Zanzibar leo 11-12-2024





















RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameiagiza timu kuu ya kitaalamu ya Dira ya Maendeleo ya 2050 kukutana na wadau mbalimbali kuhakikisha kazi ya kupokea maoni inakamilika kikamilifu ili kuwa na Dira yenye kubeba maono ya wananchi wote.

Pia, Dk. Mwinyi ameziagiza Tume za Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Serikali ya Mapiduzi ya Zanzibar kuhakikisha wanaratibu zoezi la uhakiki kwamba linafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu pamoja na kuisambaza rasimu hiyo kwa vyombo mbalimbali na kuweka mfumo halisi wa kupokea maoni.

Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipozindua Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hotel ya Golden Tulip Uwanja wa ndege Mkoa wa Mjini Magharibi, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali za SMT na SMZ akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amewaagiza viongozi na wataalamu wote wa Serikali zote mbili kutoa ushirikiano kwa timu ya kitaalam ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwani kutoshiriki kwao hakutofanikisha azma ya Dira hiyo.

Rais Dk. Mwinyi pia ameisisitiza timu hiyo ya Kitaalam kuhakikisha inamfikia kila mwanchi kote nchini ili kutoa maoni bila kujali tofauti za dini, siasa, jinsia, makundi maalum au eneo mtu analotoka kwani Raisimu hiyo ni ya Watanzania wote, hivyo alieleza ni lazima ibebe maono yao ya miaka 25 ijayo.

Dk. Mwinyi amebainisha malengo makuu ya Rasimu hiyo ni kuona yamegusa moja kwa moja katika kuboresha maisha ya watu, elimu, afya, ustawi wa amani na haki pamoja na kuwa na Dira jumuishi ambayo itamshirikisha kila mwananchi kutoa mchango wake kwa maendeleo ya Taifa.

Ameishauri timu hiyo kuweka muktadha wa maendeleo ya Taifa katika mwelekeo wa makubaliano au mipango ya kikanda na kimataifa, akitolea mfano “Dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki” (EAC) 2050; “Dira ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika” (SADC) 2050; “Makubaliano ya Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi” (Paris Agreement); “Ajenda ya Maendeleo ya Afrika” (Ajenda 2063); “Doha Programme of Action 2022 – 2023” na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs)

Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameishauri timu hiyo ya kitaalamu kuandaa usimamizi mzuri wa kukusanya maoni ya wadau kwa kuzunguka nchi nzima na kuandaa makongamano na majadiliano na wadau.

Akitaja mafanikio ya Dira ya 2025 ambayo inafikia tamati mwezi Juni 2025, amesema kuwa ni pamoja na Kuboresha hali ya Maisha ya watu, elimu, Uboreshaji wa huduma za afya, kupunguza vifo na kuongezeka wastani wa umri wa kuishi, kuimarika kwa utawala wa kisheria na ukuaji wa uchumi.

Alisema, kwa kipindi chote cha utekelezaji wa Dira 2025, nchi imekuwa kitovu cha amani na imeshiriki kikamilifu hata katika duru za kimataifa kulinda amani barani Afrika, aliwasisitiza Watanzania kuendelea kulinda amani, utulivu na umoja kama misingi muhimu ya kupata maendeleo ya nchi.

Ameeleza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zenye utoshelevu wa chakula kwa asilimia 124. Licha ya kuwa bado kilimo hakijawa cha kisasa, lakini wakulima wamefanya kazi kubwa ya kuhakikisha nchi haikabiliwi na njaa.

Akizungumzia ustawi wa Elimu amesema kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la madarasa, vyuo vikuu na walimu. Aidha, udahili wa elimu ya msingi umeongezeka kutoka 69% kutoka mwaka 2000 hadi kufikia 97% mwaka 2022, kuongezeka kwa kiwango cha kumaliza elimu kutoka 51% mwaka 2000 hadi 70% mwaka 2022 na kufanikiwa kuondoa pengo kubwa lililokuwepo katika elimu ya msingi na sekondari kati ya watoto wa kike na watoto wa kiume.

Aidha, kuimarisha kiwango cha ufaulu katika mitihani ya darasa la saba kutoka 22% mwaka 2000 hadi kufikia 80% mwaka 2022; kuongezeka kwa kiwango cha kujiunga na elimu ya sekondari kutoka 20% hadi 70%; na ongezeko la wanafunzi wanaopata elimu ya juu kutokana na Serikali kuongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu. Hatua hiyo imefikiwa kutokana na Serikali kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika sekta ya elimu kwa kuzingatia umuhimu wake katika kuchochea maendeleo ya nchi yetu.

Kuhusu Uboreshaji wa huduma za afya alisema Dira 2025 ilifanikiwa kupunguza vifo na kuongezeka wastani wa umri wa kuishi, kuimarika kwa hizo kuanzia kwenye vituo vya fya, zahanati, hospitali za wilaya, mikoa, kanda hadi Taifa.

Akielezea Utawala bora na utawala wa sheria ameeleza kuwa limebaki kuwa kipaumbele kwa Taifa licha ya changamoto ndogo ndogo ambazo zimeendelea kushughulikiwa na Serikali kwa masilahi mapana ya wananchi ikiwemo kuundwa kwa Tume ili kupendekeza namna ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini ikiwa ni njia ya kuendelea kuimarisha zaidi mifumo ya haki jinai na hivyo kudumisha utawala bora na utawala wa sheria.

Hata hivyo ameweleza mafanikio ya uchumi wa nchi umekuwa kwa wastani wa 6.7% ikiweko kukua kwa biashara na uwekezaji, kujenga miundombinu muhimu kwa sekta zote ikiwemo ujenzi wa barabara na madaraja makubwa, reli ya kisasa, ukarabati mkubwa wa reli ya kati, bandari, meli, viwanja vya ndege, miundombinu ya mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaaliwa amsema uzinduzi wa rasimu ya 2050 ni jambo kubwa lenye mustakabali muhimu kwa Taifa la Tanzania.

Amebainisha kuwa Raismu hiyo ni ya Watanzani wote na kuahidi timu ya kitaalamu ya Dira hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uaminifu ili hatimye kuwa na Dira ya 2050 yenye tija na manufaa kwa Watanzania.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Kitaifa ya Maandalizi ya Dira 2050, Prof. Kitila Mkumbo, ameleza msingu mkuu wa Rasimu hiyo umejikita katika usalama, amani na utulivu na kuwa na uchumi imara. Pia ameeleza uzinduzi wa Rasimu hiyo ni mwanzo wa safari na hatimaye itawasilishwa Bungeni kwaajili ya mijadala.

Kwa upande wake Dk. Saada Mkuya Salum, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Fedha na Mipango wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Uongozi ya Kitaifa ya Maandalizi ya Dira 2050, Zanzibar imeshiriki kikamilifu kutoa maoni juu ya rasimu hiyo kwa hatua mbalimbali ikiwemo kuratibu maoni ya wananchi huku kukiwa na ushiriki mkubwa wa wanawake.

Rais Dk. Mwinyi alikabidhi Rasim ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaaliwa kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Pamoja na Watendaji wa kuu wa Taasisi za Umma na binafsi.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake