Monday, December 23, 2024

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWEKA JIWE LA MSINGI SEKONDARI YA MWANZA GIRLS’


*Akagua ujenzi wa mradi wa maji Kisesa, wilayani Magu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifungua kitambaa alipoweka jiwe la msingi la shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mwanza iliyopo katika kijiji cha Ihushi kata ya Bujashi, Wilayani Magu. Desemba 21, 2024.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia majiko yaliyopo katika shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mwanza baada ya jiwe la msingi la shule hiyo iliyopo katika kijiji cha Ihushi kata ya Bujashi, Wilayani Magu.
Muonekano wa Tanki la kuhifadhia maji la Kisesa lenye urazo wa lita milioni 5 ambalo likikamilika litaweza kuhudumia wananchi 75,000Mkoani Mwanza
Muonekano wa Daraja la Sukuma linalounganisha vijiji vya Ngh’aya na Lumeji ambalo ujenzi wake utagharimu shilingi bilioni 10 hadi kukamilika. Mheshimiwa Majaliwa ameweka jiwe la Msingi la ujenzi wa Daraja hilo liliopo Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifungua kitambaa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Sukuma linalounganisha vijiji vya Ngh’aya na Lumeji ambalo ujenzi wake utagharimu shilingi bilioni 10 hadi kukamilika kwake, Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Mwanza (Mwanza Girls’) na kuweka jiwe la msingi la msingi la shule hiyo katika kijiji cha Ihushi, kata ya Bujashi, wilayani Magu.

Shule hiyo ni miongoni mwa shule za sekondari za bweni 26 zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000 ambazo zinaendelea kujengwa nchi nzima kwa ajili ya wasichana wanaosoma masomo ya sayansi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita.

Akizungumza na wananchi waliofika shuleni hapo (Jumamosi, Desemba 21, 2024), Waziri Mkuu amesema suala la elimu ni hitaji la muhimu kwa ajili ya watoto wa Kitanzania na kwamba ujenzi wa shule hiyo chini ya mradi wa kuboresha elimu ya sekondari (SEQUIP) ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Mheshimiwa Rais alielekeza tutekeleze miradi inayogusa moja kwa moja ya kila siku ya wananchi. Shule ni hii inaribia kukamilika; katika sekta ya afya zililetwa sh. milioni 250 kwa ajili ya zahanati tano; Hospitali ya Wilaya tayari imekamilika, hivi karibuni sh. milioni 700 zililetwa kukamilisha majengo ikiwemo wodi ya wanaume.”

Amesema kwenye umeme, vijiji 81 kati ya 82 vya wilaya hii tayari vimepata umeme na kijiji kimoja kilichobakia kiko kwenye kisiwa ndani ya Ziwa Victoria lakini tayari mikataba imeshainiwa ili maeneo ya visiwani yaweze kupelekewa umeme.

Naye, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Zainab Katimba alisema ujenzi wa shule hiyo ambayo iko kwenye hatua za umaliziaji, umegharimu sh. bilioni 4.5 na kwamba hadi sasa wanafunzi 514 wamekwishaanza masomo kwenye shule hiyo.

Alisema ifikapo Januari 2025, shule hiyo inatarajiwa kupokea wanafunzi 120 wa kidato cha kwanza.

Mapema asubuhi, Waziri Mkuu alikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa tenki la kuhifadhi maji la Kisesa, wilayani Magu, mkoani Mwanza ikiwa ni mpango wa muda wa kati wa kuboresha huduma ya maji jijini Mwanza ambao unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 3.54.

Ujenzi wa tenki hilo lenye ujazo wa lita milioni tano, unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania pamoja na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (France Development Agency). Hadi sasa, ujenzi wake umefikia asilimia 93 na unatarajiwa kuhudumia wakazi 75,000 wa maeneo ya Kisesa Bujora, Igudija na maeneo ya jirani pindi utakapokamilika.

Akizungumza na wananchi wa eneo la Kisesa baada ya kukagua mradi huo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi mikubwa inayowagusa wananchi moja kwa moja kwenye sekta za elimu, afya, maji, kilimo, uvuvi na barabara.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema wizara hiyo itaendelea kusimamia maagizo ya Rais Dkt. Samia ya kuhakikisha wananchi wanapata maji katika maeneo yao. “Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alisema hataki kuona wanawake wa nchi hii wakiteseka kutafuta maji.”

Alitumia fursa hiyo kumpongeza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Nelly Msuya kwa kazi kubwa ya kusimamia ujenzi wa miradi ya maji ambayo ilisaidia kuongeza upatikanaji wa maji jijini Mwanza hata kabla ujenzi wa tenki hilo kubwa haujakamilika.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Nelly Msuya alisema kuwa ujenzi wa tenki la Kisesa unatarajiwa kukamilika ifikapo Februari, 2025 na kwamba kazi iliyobakia sasa ni kufunika tenki, ujenzi uzio na kibanda cha mlinzi.

Alisema ujenzi wa mradi huo ulianza Juni 2023 hadi sasa sh. bilioni 2.9 zimekwishalipwa kwa mkandarasi.

Mbali na tenki hilo, Bi. Msuya alisema kwamba matenki mengine yanajengwa katika maeneo ya vilima vinavyozunguka Jiji la Mwanza ikiwemo Nyamazobe (lita milioni 10); Buhongwa (lita milioni 5); Fumagila (lita milioni 10) na Usagara (lita milioni moja).

“Utekelezaji wa mradi huu wa thamani ya shilingi bilioni 49 umeanza na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili ifikapo Desemba 2026.”

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake