Na Sabiha Khamis Maelezo
Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC) imewataka wafanyabiashara kutumia fursa za kuibua changamoto zilizopo katika ulipaji wa kodi ili kuiletea nchi maendeleo.
Akizungumza katika ufunguzi wa warsha ya wadau wa sekta binafsi kuhusu majadiliano ya changamoto za kodi na mapendekezo ya marekebisho, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Ali Suleiman Amour amesema utozaji wa kodi umeathiri sana sekta ya viwanda hivyo ameutaka mjadala huo kuhakikisha unajadili na kuondoa changamoto zilizopo ili kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara.
Amesema fursa hizo zitasaidia kuibua maoni yatakayojenga misingi bora ya ufanyaji kazi pamoja na kutoa mapendekezo yatakayo kubalika na kupewa kipaumbele katika kujenga mfumo bora wa kodi.
Aidha, amesisitiza ushirikiano katika kutoa ushauri ambao utajenga ushirikiano baina ya sekta binafsi na za Serikali ili kuhakikisha tunajenga ukaribu wenye kutaleta manufaa katika kuiletea nchi maendeleo.
Amemalizia kwa kusema kuwa warsha hiyo italeta mapendekezo ambayo yataweza kuleta tija na manufaa kwa kutengeneza mfumo bora wa kodi utakaoweza kujenga mazingira rafiki ya biashara kwa Zanzibar na Tanzania bara.
Nae Mkurugenzi Mtendaji Jumiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC) Hamad Hamad amesema katika kuimarisha mifumo bora ya kodi ni vyema kuzitambua na kutoa mapendekezo kuhusu changamoto za kodi zilizopo.
Amesema kutokana na elimu ndogo ya kodi mamlaka zinazohusika na kadi zinapaswa kutoa elimu zaidi kwa wafanyabiashara wanaoanza na waliopa awali kutoka na mabadiliko ya kodi mara kwa mara pamoja na kuwavutia wawekezaji wa ndani hasa wanaoanza biashara.
Ameeleza changamoto zilizopo ni pamoja na mifumo ambayo haisomani kwa mamlaka za kodi kutokana na vitu vinavyorikodiwa na mamlaka moja kuwa hakitambuliki na mamlaka nyengine hali inayopelekea usumbufu kwa wafanyabiashara.
"Kwa mamlaka inayotambulika kisheria kama ZRA basi iweze kutambulika na mamlaka nyengine kama TRA na hata mamlaka za chini za Serikali za mitaa kama vile manispaa ambazo zipo katika kukusanya kodi" alisema Mkurugenzi Hamad.
Akitoa maoni kwa Serikali zote mbili kuzishirikisha Sekta binafsi wakati wa kuandaa Sera na sheria za kodi kwa kutoa michango na kuithamini michango yao kutokana na sekta binafsi ndio wadau wakuu wa biashara katika kuingiza kodi nchini.
Nao washiriki wa mjadala huo wamesema kuwa mkutano huo umewapa elimu ya kujua majukumu yao ya kodi wanazotakiwa kulipa wamiliki wa kampuni na wafanyabiashara.
Hata hivyo wameiomba Serikali kuendelea kutatua changamoto za biashara katika kurahisha mazingira ya kufanyia biashara ili kuongeza tija na maendeleo katika nchi.
Mkutano huo umetokana na kikao cha Baraza la Taifa la Biashara Tanzania kilichofanyika Julai 2024 ambacho kiliibua malalamiko mengi kwa Sekta binafsi kuhusu kodi.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake