Thursday, February 13, 2025

ACT WAZALENDO YASHINDA MAPINGAMIZI 7 KATI YA 13 MAHAKAMANI



Chama cha ACT Wazalendo kimefanikiwa kushinda mapingamizi saba kati ya 13 yaliyowekwa na mawakili wa serikali katika kesi zilizofunguliwa na chama hicho kupinga matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji, na vitongoji uliofanyika Novemba mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Kigoma, Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Ndugu Yunus Luhovya, alisema kuwa mawakili wa chama hicho wamepambana kwa nguvu na kufanikiwa kushinda mapingamizi saba hadi kufikia leo, huku mengine yakendelea kusikilizwa.

Luhovya alionyesha masikitiko yake kwa serikali kwa kuzuia kusikilizwa kwa kesi za msingi kwa kuweka mapingamizi katika kesi zote za uchaguzi. Alisema kuwa mawakili wa serikali wanadai kuwa waliofungua kesi hizo hawakuwa wagombea halali, jambo ambalo si la kweli na linakusudia kuziondoa kesi hizo mahakamani kabla ya ushahidi kusikilizwa.

Luhovya alitoa wito kwa wanachama wa ACT Wazalendo wanaohudhuria mahakamani kuendelea kufika kwa ujasiri ili kujionea wenyewe jinsi haki inavyopatikana mahakamani.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake