ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 8, 2026

DC LINDI MHE. VICTORIA MWANZIVA ATEULIWA KATI YA WANAWAKE 15 BARANI AFRIKA KUSHIRIKI PROGRAMU YA UONGOZI KWA WANAWAKE YA EJS CENTRE


Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Mhe. Victoria Mwanziva, ni miongoni mwa Wanawake 15 Barani Afrika waliopata bahati ya kuchaguliwa kwenye program maalum ya Uongozi kwa Wanawake, mafunzo ambayo yanafanyika nchini Liberia na Sierra Leone.

Katika mchujo huo, Mhe DC Mwanziva amebainisha kuwa, amepitia mchujo wa maombi ya zaidi ya Wanawake viongozi 600 Barani Afrika.


Kauli ya Mhe. DC Mwanziva:

"Ninamshukuru Mwenyezi Mungu nimechaguliwa kuiwakilisha Tanzania kushiriki katika Programu mahususi na maalumu ya Uongozi kwa wanawake inayoratibiwa na Rais wa kwanza Mwanamke Barani Afrika- Rais Mstaafu wa Liberia- Mhe Ellen Johnson Sirleaf.

Programu hii inayojulikana kama *“Amujae Leadership Initiative”* chini ya Ellen Johnson Sirleaf Presidential Centre for Women and Development- EJS Centre ninaenda kuungana na wanawake viongozi waliopata fursa na heshima ya kushiriki wakiwemo- Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii wa Namibia Mhe Dkt Esperance Luvindao, Waziri wa Mazingira wa Guinea Mhe Djami Diallo,

Wabunge mbalimbali kama Mbunge kundi la wanawake kutoka Senegal Mhe Anta Diack na wanawake Viongozi wa Mashirika na Taasisi mbalimbali barani Afrika kama Dr Anneline Chetty Mtendaji mkuu wa kituo cha Biashara, Viwanda na Uwekezaji Afrika ya Kusini.


Aidha, nimekuwa miongoni mwa Wanawake 15 Barani Afrika waliochaguliwa kushiriki mafunzo haya nchini Liberia na Senegal- baada ya kupitia mchujo wa maombi ya zaidi ya wanawake viongozi 600 barani Afrika- nikilivutia jopo la mchujo na haswa kilichowavutia juu ya kunichagua ni sababu ya kazi ninazofanya za uongozi wa jamii hususani maeneo ya vijijini na zenye kugusa jamii moja kwa moja na vijana kupitia utendaji wangu kama Mkuu wa Wilaya ya Lindi- nafasi niliyoaminiwa kuteuliwa na Rais wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan.

Programu hii ya kimkakati na kihistoria imelenga kuleta pamoja Wanawake viongozi kutoka barani Afrika na kuwapa uwanda wa kukutana na kujadiliana kwa pamoja masuala ya Uongozi kwa wanawake yenye mrengo wa ajenda za maendeleo barani Afrika.

Mafunzo haya yana tija kubwa kwenye uwakilishi wa nchi ya Tanzania barani Afrika na zaidi kuzidi kufungua fursa za mashirikiano mema baina ya mataifa ya Barani Afrika." Amebainisha DC Mwanziva.



#Tags:

@ejscenter #EllenJohnsonSirleaf #AmujaeInitiative #AmujaeForum #MonroviaLiberia #Tanzania

No comments: