📍 Viwanja vya Sabasaba, Dar es Salaam
Matokeo ya tafiti za Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) yanayoonesha kuwa asali ya Tanzania inakidhi viwango vya soko la kikanda na kimataifa kwa kuzingatia ubora wake, yamekua kivutio kwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Daniel Pancras, alipotembelea taasisi hiyo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Bw. Pancras alitembelea TAFORI leo Julai 12, 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua na kutembelea taasisi na idara zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zinazoshiriki maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika banda hilo, alipata maelezo kuhusu tafiti mbalimbali zinazotekelezwa na TAFORI, ikiwemo utafiti uliochambua ubora wa asali inayozalishwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuzingatia mikoa, hali ya hewa, aina ya udongo na vyanzo vya maua.
Matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa sifa za asali ya Tanzania, zikiwemo utamu, riha na viambata vyake, zinakidhi viwango vya soko la kikanda na kimataifa.
Bw. Pancras pia ameipongeza TAFORI kwa kuendelea kusogeza huduma za kitafiti karibu na wananchi na wadau kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo.
TAFORI inaendelea kuwakaribisha wananchi na wadau kutembelea banda lake ndani ya Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii ili kupata elimu, ushauri wa kitaalamu na kufahamu matokeo ya tafiti zinazochochea maendeleo ya sekta ya misitu na nyuki.



No comments:
Post a Comment