Ilikuwa ni video ya harusi iliyonipeleka kwenye story ya maisha ambayo sikuitarajia kabisa. Jumamosi nilitumiwa video za sherehe ya harusi ya Sharlene Ruto huko Kilgori, iliyofanyika katika ranchi ya Rais William Ruto. Pamoja na video hiyo kulikuwa na caption fupi iliyosema: “Mtanzania achumbia binti wa Ruto.” Kwa udadisi, nilianza kutafuta jina la Mtanzania huyo. Nilichotarajia kukutana nacho ni story ya kijana Mtanzania ambaye kwa namna fulani amejikuta akiingia katika familia moja ya kisiasa yenye nguvu zaidi nchini Kenya. Lakini nilichokutana nacho kilikuwa kikubwa zaidi.
Kiu changu cha kumuelewa vizuri huyu kijana kikaongezeka wakati wa sherehe hiyo, Rais William Ruto alimuelezea Isaiah kama kijana jasiri na mstahimilivu, ambaye aliweza kupenya na kujenga uhusiano ndani ya familia yenye watu mashuhuri, hadhi kubwa na ulinzi mkali, hadi kufikia hatua ya kumchumbia binti yake. Kauli hiyo ilinifanya nijiulize zaidi: Huyu kijana ni nani? Kadiri nilivyozidi kutafuta na kujifunza kuhusu maisha yake, ndivyo nilivyozidi kugundua kwamba nyuma ya yule kijana aliyekuwa akitajwa kwenye story ya harusi kulikuwa na historia ya maisha ambayo, kwa maoni yangu, ilipaswa kujulikana zaidi Tanzania.
Isaiah hakuzaliwa katika mazingira ya upendeleo. Alizaliwa na baadaye kutelekezwa na wazazi wake, akaenda kuishi na bibi yake kijijini Mwanza, katika mazingira ambayo umasikini haukuwa neno tu bali ulikuwa sehemu ya maisha ya kila siku. Hakukua katika mazingira ambayo yangempa mtu sababu ya kuamini kwamba siku moja angekuwa mhitimu wa chuo kikuu au kijana anayetambuliwa kimataifa. Alikuwa mchungaji wa mifugo na hata alianza shule akiwa na umri mkubwa. Kwa mtoto anayekulia katika mazingira kama hayo, maisha yanaweza kuonekana tayari yameamua hatima yake. Lakini kwa Isaiah, haikuwa mwisho wa safari. Alikuwa na kitu ambacho hata umasikini haukuweza kumpokonya: azma, uthubutu na ubunifu.
Alipambana kupata elimu. Kutoka kwenye maisha ya kijijini na kuchunga mifugo, aliweza kufika sekondari na hatimaye kupata degree yake katika Institute of Finance Management (IFM). Hilo pekee lilikuwa ni jambo kubwa. Mtoto aliyekulia kwenye mazingira magumu, akawa mchungaji wa mifugo, lakini akapambana na kufika chuo kikuu. Lakini kinachofanya story ya Isaiah iwe ya kipekee zaidi si degree aliyopata. Ni kile alichofanya baada ya kufanikiwa.
Isaiah hakusahau alikotoka. Alirudi kijijini kwao. Hakurejea kwa ajili ya kujionyesha kwamba ametoboa. Alirudi kuwainua wengine. Aliwafundisha watoto na vijana wa kijijini English na Mathematics. Alikuwa amepata nafasi ya kuondoka kwenye mazingira yaliyomlea na kupata elimu iliyomfungulia milango mipya, lakini hakuruhusu mafanikio yake yamfanye awasahau wale waliokuwa bado nyuma. Badala yake, alirudi na elimu yake na kuitumia kuwasaidia watoto waliokuwa wanaishi katika mazingira yale yale aliyokuwa ameyapitia yeye. Alikuwa ametoka kwenye umasikini, lakini hakusahau umasikini alioishi nao.
Hapo ndipo elimu yake ilianza kuwa zaidi ya cheti. Ikawa chombo cha kubadilisha maisha ya wengine, kamba ya kuwavuta vijana kutoka kwenye shimo la giza. Lakini Isaiah hakuishia kwenye kufundisha watoto kijijini. Alianza pia kutumia teknolojia na ubunifu kutatua changamoto ambazo yeye mwenyewe alikuwa ameziona na kuzipitia. Baada ya kumaliza IFM, angeweza kuchagua njia rahisi kukaa ofisini, kupata kazi na kuendelea na maisha yake. Badala yake, alitazama tatizo ambalo alilifahamu vizuri: vijana talented and bright ambao wanataka kusoma lakini wanakosa taarifa, fursa na scholarship. Kutokana na uelewa huo, alianzisha SomaApp, akilenga kutumia teknolojia kusaidia wanafunzi kupata fursa za elimu na scholarships nje ya nchi.
Hapa ndipo tunapoona tofauti kati ya mtu mwenye elimu na mtu anayejua kutumia elimu yake. Isaiah hakuiona degree yake kama mwisho wa safari. Aliiona kama uwezo wa kutafuta solutions. Alitumia kile alichojifunza kutatua matatizo aliyoyaona katika jamii yake na kwa vijana wengine. Na huu ndio mtazamo ambao Afrika inahitaji zaidi: siyo kuona changamoto kama sababu ya kukata tamaa, bali kuziona pia kama opportunities za innovation.
Mchango wake kwa watoto, vijana na jamii yake hatimaye ulianza kuvutia attention nje ya Tanzania. UNICEF ilimtambua na kumchagua kushiriki katika tamasha la vijana nje ya nchi. Lakini recognition hiyo haikuishia hapo. Isaiah alifika hatua ya kutunukiwa zawadi na Queen Elizabeth, akitambuliwa kama kijana mbunifu aliyekuwa akitumia uwezo na mawazo yake kusaidia jamii yake kupambana na umasikini.
Hebu rudi nyuma uangalie safari yote. Msukuma wa kijijini, aliyetelekezwa na wazazi wake. Mtoto aliyekulia kijijini kwa bibi yake. Mchungaji ngombe. Mtoto aliyechelewa kuanza shule. Mwanafunzi aliyepambana kupata elimu. Mhitimu wa IFM. Kijana aliyerudi kijijini kuwafundisha watoto English na Mathematics. Mbunifu aliyeanzisha SomaApp ili kusaidia vijana kupata fursa za elimu. Kijana ambaye juhudi zake zilitambuliwa na UNICEF. Na hatimaye kijana aliyepokea recognition kutoka kwa Queen Elizabeth. Dunia ilimuona. UNICEF ilimuona. Queen Elizabeth alimuona. Na hata Rais wa Kenya alimuona kama kijana jasiri na mstahimilivu.
Lakini swali linabaki: Kwa nini Tanzania yenyewe haikumwona?
Hili ndilo swali ambalo linanifanya niione story ya Isaiah kama zaidi ya historia ya mtu mmoja. Inaibua swali kuhusu namna tunavyotambua mafanikio na mchango wa watu wetu. Mara nyingi tunawatafuta mashujaa kwenye majukwaa makubwa. Tunawatafuta kwenye siasa, biashara, michezo, entertainment au kwenye nafasi kubwa za uongozi. Tunapenda mafanikio yanayoonekana, yanayokuwa na headlines na yanayoweza kutambulika kwa urahisi. Lakini kuna aina nyingine ya mafanikio ambayo mara nyingi hayapati headlines: mafanikio ya mtu anayemaliza chuo na kurudi kijijini; mafanikio ya mtu anayewafundisha watoto bila kutafuta umaarufu; mafanikio ya mtu ambaye baada ya kuinuka, anawainua wengine.
Isaiah anatufundisha kwamba mafanikio si tu kutoka kwenye umasikini. Mafanikio ya kweli yanaweza kuwa kutoka kwenye umasikini, kupata elimu, kufanikiwa, halafu kutumia mafanikio hayo kuwasaidia wengine nao wasonge mbele. Unaweza kuanza maisha ukiwa mtoto wa kijijini. Unaweza kuwa mchungaji wa mifugo. Unaweza kukulia katika mazingira ambayo hayakupi guarantee yoyote ya mafanikio. Lakini bado ukawa na ndoto, ukapata elimu, ukafanikiwa na muhimu zaidi ukawakumbuka wengine.
Pengine somo lingine kubwa kutoka kwa Isaiah ni kwamba Afrika si bara la matatizo pekee; ni bara lenye watu wenye uwezo wa kutengeneza solutions. Isaiah hakuangalia changamoto alizoziona kama sababu ya kukata tamaa. Aliziona pia kama fursa ya kubuni solution. Kupitia SomaApp na kazi zake nyingine, alijaribu kutumia technology, education na innovation kushughulikia matatizo yanayowakabili vijana na kufanikiwa kuwapatia vijana zaidi ya 700 scholarship za kusoma nje ya nchi. Huu ni mtazamo ambao kizazi kipya cha Waafrika kinahitaji: tusione kila tatizo kama ushahidi kwamba Afrika imeshindwa; wakati mwingine tatizo lenyewe linaweza kuwa mwanzo wa innovation.
Labda sasa tunapaswa kujiuliza swali kubwa zaidi: Je, Tanzania ina mashujaa wachache, au tuna mashujaa wengi ambao hatujawahi kuwatazama kwa karibu? Je, ni watu wangapi wamefanya mambo makubwa katika jamii zao lakini majina yao hayajawahi kufika kwenye national conversation? Ni vijana wangapi wamepambana kutoka kwenye mazingira magumu, wakapata elimu, wakarudi kuwasaidia wengine, lakini story zao hazikuwahi kusimuliwa? Kwa sababu wakati mwingine si kwamba nchi haina watu wa kujivunia.Tatizo ni kwamba tunashindwa kuwaona wakati bado wako miongoni mwetu.
No comments:
Post a Comment