Na Oscar Mbuza, Kilwa
MKUU wa Wilaya ya Kilwa Mohamed Nyundo atakuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 121 ya kuanza kwa vita vya Majimaji katika kijiji cha Nandete, Tarafa ya Kipatimu wilayani Kilwa mkoani Lindi leo Oktoba 3, 2026.
Maadhimisho hayo yanafungwa leo ikiwa ni siku ya tatu tangu kuanza kwa tamasha lake kuelekea siku ya kilele yakiwa yamezinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Adam Malima, ambapo pamoja na mambo mengine limebeba dhana ya utalii wa utamaduni kutokana na kushirikisha maonesho ya historia ya vita vya Majimaji, midahalo, vikundi vya ngoma na burudani, vyakula na vinywaji vya asili na kazi nyinginezo za mikono za kitamaduni.
Tofauti na miaka iliyotangulia, mwaka huu maadhimisho hayo yametawanywa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kilwa yakizinduliwa katika eneo la Kilwa Kisiwani na kufanyika pia katika maeneo ya Kilwa Kipatimu huku kilele kikiwa katika kijiji cha Nandete ambako Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa jengo la kisasa la Makumbusho ya Kuanza kwa Vita vya Majimaji ambalo ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 88 ili kukamilika.
Akizungumzia umuhimu wa jengo hilo, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Malikale, Wizara ya Maliasili na Utalii, William Mwita ambaye amekagua maendeleo ya ujenzi wake jana Oktoba 2, 2026, amesema litakuwa chachu katika kuchechemua utalii wa Kusini kutokana na eneo la Kilwa pia kuwa na vivutio vingi vya utalii.
“Kama inavyofahamika kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii na Serikali kwa ujumla inaweka mikakati mbalimbali ya kuchechemua vivutio vya utalii vilivyo Kusini mwa Tanzania hivyo litakapokamilika na kuanza kufanya shughuli zake ni wazi kuwa tutakuwa tumecheza kete muhimu sana katika kufungua utalii wa kusini,” amesema Mwita.
Aidha Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilwa (DAS) Yusuph Mwinyi amesema Serikali ya Wilaya kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wanachukua hatua mbalimbali za kuboresha Maadhimisho hayo kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kuyafanya kuwa miongoni mwa vivutio bora kabisa vya utalii nchini hivi karibuni.
*Kisa cha Wamatumbi kung’oa miche ya pamba shamba zima na kusababisha vita vya Majimaji*
Vita hiyo ilizuka ghafla kutokana na mzozo wa utumikishwaji wa wakazi wa eneo hilo wa kabila la Wamatumbi kwenye mashamba makubwa ya pamba yaliyokuwa yakimilikiwa na Serikali ya Mjerumani katika eneo la Nandete Julai 15, 1905, na baadaye kusambaa na kuwa moja ya vita kubwa ya kihistoria nchini ikipiganwa katika mikoa saba wakati huo ya Lindi, Mtwara, Pwani, Dar es Salaam, Morogoro, Iringa/Njombe na Ruvuma kabla ya kuhitimishwa Agosti 8, 1907.
Mzozo ulianza katika mashamba hayo makubwa ya pamba ya Nandete, katika Tarafa ya Kipatimu Lindi ambapo Wajerumani walioweka makazi yao katika kijiji cha Kibata kilometa kadhaa kutoka Nandete na kuanzisha mashamba hayo waliwatumikisha Wamatumbi kwa lazima kwa kuwaamuru kupanda miche ya pamba na kuwaamuru tena wang’oe baadhi ya miche ili pamba hiyo ipate nafasi ya kukua vizuri hatua iliyowakasilisha Wamatumbi ambao waliamua kung’oa miche yote ya pamba shambani kitendo ambacho pia kiliwachukiza Wajerumani na kuanzisha mzozo ulioanzisha vita hiyo.
Aidha Wamatumbi pia walichoshwa na mateso ya kulazimishwa kuwabeba Wakoloni wa Kijerumani kwa machela umbali mrefu kutoka Kibata yaliko makazi yao hadi Nandete kwenye mashamba kila siku kwenda na kurudi huku mbebaji anayejikwaa njiani na kumuangusha Mkoloni akichapwa viboko 25 kwa 50, mateso yaliyokoleza moto wa hasira na kusababisha vita hiyo kuripuka.
Hadithi ya kusisimua zaidi katika vita hiyo ambayo umaarufu wake umeegemea zaidi katika Mkoa wa Ruvuma katika eneo la Songea ambako ilisambaa baadaye ni uwepo wa mtani wa Wamatumbi, Kinjeketile Ngwale kutoka kabila la Wangindo aliyewahamasisha Wamatumbi kuingia katika vita kwa kutumia silaha za jadi huku akiwapa dawa ya asili akidai ina uwezo wa kugeuza risasi za Wajerumani kuwa maji, hatua iliyosababisha watu wengi katika mikoa husika waliopigana vita hiyo dhidi ya Mjerumani kupoteza maisha kwa kupigwa risasi za moto.





No comments:
Post a Comment