• Kapewa vipi kibali cha kumiliki pingu
UTATA wa kumiliki pingu alizokamatwa nazo mwandishi wa habari za uchunguzi wa Shirika la Utangazi la Taifa (TBC), Jerry Muro, umezusha maswali yanayokosa majibu juu ya kazi yake halisi.
Miongoni mwa maswali yanayoonekana kuumiza zaidi vichwa vya watu ni kwa namna gani mwandishi huyo aliweza kupata kibali cha kununua pingu hizo kutoka duka la Jeshi la Mzinga lililopo Upanga, jijini Dar es Salaam.
Blog ya vijimambo imebaini kuwapo kwa waandishi wa habari kadhaa ndani na nje ya nchi wanaomiliki silaha kama sehemu ya kujilinda lakini limeshindwa kusikia au kuona mwandishi anayemiliki pingu, ambayo inasadikika ni bidhaa maalumu kwa ajili ya majeshi pamoja na kampuni za ulinzi.
Maswali hayo yanayoumiza vichwa vya baadhi ya watu pia yalitokana na taarifa za mmoja wa wasemaji wa JWTZ ambaye aliweka bayana kuwa si jambo la kawaida kwa raia kumiliki pingu isipokuwa kwa kibali maalumu.
Maelezo hayo yaliongezwa nguvu zaidi na Mkuu wa Jeshi la Polisi Insekta Jenerali (IGP), Said Mwema, baada ya kuwaambia waandishi wa habari kuwa ameunda kikosi cha askari kuichambua sheria ili kutoa tafsiri ya raia kumiliki pingu.
IGP Mwema alionekana kupata wakati mgumu, kujua kama kuna kipengele katika sheria za nchi au kanuni za Jeshi la Polisi ambazo zinatamka juu ya raia kumiliki pingu ambazo hutumika kwa ajili ya kuwafunga watuhumiwa au wahalifu mbalimbali.
Mwema pia amesema watachunguza kama risiti ya umiliki wa pingu aliyoitoa Muro ni halali na kama alipewa kibali, na kwa lengo gani.
Blog ya vijimambo ilizungumza kwa njia ya simu na baadhi ya watu ambao pia hawakusita kuonyesha wasiwasi wao juu ya sakata la raia kukutwa na pingu. Wengine walianza kumhusisha mwandishi huyo na kazi ya askari wa Usalama wa Taifa aliyepewa jukumu maalumu.
Hoja hiyo inaonekana kupata mashiko zaidi hasa kutokana na mazingira na kauli ya Muro mwenyewe kudai kuwa pingu hizo huwa anazitumia katika kazi zake na hata pale alipotakiwa na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, kuwasilisha risiti alizonunulia pingu hizo, hakusita kufanya hivyo.
Kova, katika mkutano wake na waandishi wa habari, alisema kuwa wamempa muda Muro kuwasilisha risiti ya pingu aliyonayo kwa kuwa bidhaa hiyo ni maalumu kwa majeshi ambayo pia huziagiza nje ya nchi.
Blog ya vijimambo imedokezwa na chanzo kimoja cha habari kuwa huenda baadhi ya watendaji wa jeshi waliompa kibali cha kununua pingu mtangazaji huyo wakawa katika wakati mgumu zaidi pindi watakapobainika.
Taarifa hizo zinadai kuwa watendaji hao si tu wanaweza kukosa ajira lakini pia wanaweza kufikishwa katika mahakama ya jeshi na baadaye katika mahakama za kiraia.
Umiliki wa pingu hizo unaonekana kuwachanganya hata baadhi ya vigogo jeshini ambao wamekuwa na wasiwasi wa kuwa huenda wanashughulika na mtu wasiyemjua kwa undani zaidi jambo ambalo pia limechangia kulishughulikia suala hilo kwa ufanisi zaidi.
Mkanganyiko huo ulizidishwa zaidi na taarifa za baadhi ya magazeti ambazo pia zilitoa kivuli cha nakala ya risiti yenye namba 34357310 inayoonyesha kuwa pingu hiyo ilinunuliwa katika duka la Shirika la Mzinga lilioko Upanga, jijini Dar es salam.
Blog ya vijimambo ilifanya mawasilino kwa simu na muuzaji wa duka hilo ambalo linamilikiwa na JWTZ ambaye alisema yeye si msemaji wa vitu vinavyonunuliwa hapo huku akilielekeza limpigie simu meneja mkuu wa shirika hilo ambaye anapatikana Morogoro.
Juhudi za Blog ya vijimambo kupata ukweli wa risiti hiyo ziligonga mwamba baada ya simu iliyopewa kupokelewa na msaidizi wa meneja huyo ambaye alisema bosi wake yuko kwenye mkutano.
Baadhi ya wanasheria waliozungumza na Blog ya vijimambo, waliweka wazi kuwa hakuna sheria inayoweka wazi juu ya raia kumiliki pingu, hivyo Muro anaweza asikumbane na rungu la dola kwa kukutwa na bidhaa hiyo.
Pamoja na utata huo, macho na masikio ya watu wengi zaidi yako kwa IGP Mwema ambaye ameahidi leo au kesho kutoa majibu juu ya uhalali wa raia kumiliki pingu hasa baada ya vijana wake aliowatuma kuichambua sheria kumpatia majibu.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake