ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 8, 2010

Masheikh, Wachungaji hapatoshi viwanja vya Biafra Kinondoni

TIMU ya Masheikh itatoana jasho na timu ya Wachungaji katika mpambano mkali, unaotarajiwa kufanyika Februari 13 mwaka huu katika viwanja vya Biafra Kinondoni.

Mchezo huo wa kukata na shoka unatarajiwa kuchezwa majira ya saa 4:00 asubuhi katika viwanja vya Biafra na kufuatiwa na hotuba mbalimbali za masheikh na wachungaji pamoja na dua maalum ya kuliombea taifa.


Hii ni mara ya pili kwa timu ya masheikh na wachungaji kukutana ambapo mara ya kwanza zilikutana katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam mwaka jana.


Katika mechi ya kwanza masheikh walilala kwa mabao 2-0 dhidi ya wachungaji.


Akizungumza na waandishi jana Mchungaji Filesteus Christopher alisema timu yake tayari imeingia kambini kujifua kwa ajili ya kutetea ubingwa dhidi ya timu ya masheikh.


"Sisi hatuna maneno mengi, timu yangu tayari ipo kambini Vingunguti inajifua na tunasubiri tu kuendeleza ushindi kwa masheikh wangu hawa," alisema Christopher.


Naye ustadh Salum Khamis kutoka Zanzibar alitamba mbele ya wachungaji hao kuwa ni mkali kwa mbio na kupachika mabao na kwamba mara hii hawatafanya kosa.


"Makosa tuliyoyafanya mwaka jana mwaka huu hatutokubali kujirudia mimi peke yangu naahidi bao tatu, kwa hiyo kama wanajifua wachungaji, inabidi wajifue kisawasawa," alisema.


Mechi hiyo inatarajiwa kushuhudiwa na watu mbalimbali wakiwamo Agostine Mrema mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour na mbunge wa Afrika ya Mashariki Aman Kabourou.

No comments: