MWENYEKITI wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila anayekabiliwa na tuhuma za kumkashifu Rais Jakaya Kikwete kwa kumwita gaidi, amewasilisha waraka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akimtaka hakimu Waliarwande Lema, ajitoe katika kesi hiyo.
Katika waraka huo, Mtikila ambaye Ijumaa iliyopita alitoka mahabusu alikuwa amekaa kwa wiki mbili kufuatia kitendo chake cha kutohudhuria mahakamani, anadai kuwa hakimu huyo hana uwezo wa kutenda haki kwa sababu ameonyesha kuwa na kisirani na ukatili dhidi yake.
Waraka huo uliowasilishwa mahakamani jana na Mtikila mwenyewe, unamtaka hakimu Lema ajitoe katika kesi hiyo kwa madai kuwa amekosa uwezo wa kutenda haki katika kesi yake kwavile ana kitu kibaya moyo mwake dhidi ya Mtikila.
Kwa heshima kubwa nakuomba uienzi haki kwa kujitoa katika mwenendo wa kesi yangu, kwa sababu umeonyesha kuwa na kisirani na ukatili dhidi yangu, na kunifokea hovyo, kwa sababu ambazo unazijua moyoni mwako,anadai Mtikila kupitia waraka huo.
Mtikila alidai kuwa Oktoba 22 mwaka 2009 alichelewa kwenda mahakamani na baada ya jalada la kesi yake kuitwa, iliamuriwa akamatwe na , kupelekwa mbele ya hakimu huyo, ambaye alimuuliza sababu za kuchelewa.
Alidai kuwa katika utetezi wake aliiambia mahakama kuwa alichelewa kwa sababu wakati akiwa njiani alilazimika kubadili gari katika eneo la Kamata- Shoprite na kwamba bahati mbaya suruali yake ilipasuka, jambo lililomlazimisha kurudi nyumbani haraka, ili kubadili nguo, tarai kwenda mahakamani.
"Lakini hata baada ya kuiona dhamira yangu njema na kufuta amri ya kunifutia dhamana, ulitumia muda mwingi kunifokea na kunikamia kwamba ˜ukirudia tena utaniona!' nikabaki kujiuliza ninachoonywa kutorudia tena ni ajali ya kupasukiwa nguo au kukimbia nyumbani kubadili nguo ili nisije mahakamani uchi...Nigekuja mahakamani uchi ningedharaulisha heshima ya mahakama na utu wangu mwenyewe,"alisisitiza Mtikila.
Alidai kuwa Novemba mosi mwaka huu, baada ya kuhangaikia mguu wake uliogongwa na nyoka aina ya Cobra akiwa nchini Zimbabwe, kwa sababu ya taabu kubwa aliyoipata usiku lakini baada ya hekaheka zote alipelekwa mahakamani.
Mchungaji huyo aliendelea kudai kuwa watu wote walihofia athari ya sumu ya nyoka huyo kwa sababu wanaogongwa wanakufa ndani ya saa 24, ingawa yeye bwana Yesu alimtendea muujiza mkubwa sana.
"Lakini wewe ulinifokea kwamba kuhangaikia uhai wangu siyo sababu ya msingi, ukafoka kwamba huna huruma na mimi, ukafuta dhamana yangu huku ukinifokea,"alidai Mchungaji Mtikila katika waraka huo.
Mchungaji Mtikila aliongeza kuwa ingawa hatimaye hakimu huyo ulimuonea huruma na kumrejeshea dhamana yake baada ya kuombwa na ndugu zake waliohangaikia hali yake, bado hakimu huyo alimtesa kwa makusudi kwa kuhakikisha kuwa anasota gerezani kwa kutotoa kibali ambacho kinandaliwa ndani ya dakika kumi tu.
"Siku kilipokosekana kigezo cha kuninyima uhuru wangu ikabidi unirejeshee dhamana yangu, nilikuwa na maralia kali sana na maumivu makali mwili wote nikitetemeka, nilikuomba nikae chini, lakini katika ukatili usio kawaida uliamuru nisimame tu potelea mbali hata ningeanguka!.
Na uliponirejeshea dhamana yangu ulizidi kunifokea bila kosa, na kuniambia ˜ukirudia tena utakiona' na kutuacha tunajiuliza kama ninachokamiwa kutorudia tena ni kugonjwa na lile joka au kule kuhangaikia uhai wangu,"alidai.
No comments:
Post a Comment