Wednesday, February 3, 2010
SAKATA LA JERRY MURO
SAKATA la mwandishi wa habari za uchunguzi, Jerry Muro, limeingia katika hatua mpya baada ya wanasheria kusema kitendo chake cha kukutwa na pingu si kosa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Muro, mfanyakazi wa Shirika la Utangazaji (TBC) na ambaye amejipatia umaarufu kutokana na kufichua aina tofauti za rushwa, Jumapili iliyopita alikutwa na pingu katika gari alilokuwa akilitumia mara baada ya kukamatwa kwa kudaiwa kutaka fedha kwa njia ya vitisho kwa aliyekuwa mhasibu wa Halmashauri ya Bagamoyo, Michael Wage.
Wage alisimamishwa kazi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali za serikali pamoja na viongozi wengine wa halmashauri hiyo.
Kamanda wa polisi Kanda ya Dar es salaam, Suleiman Kova alisema kuwa baada ya kulifanyia upekuzi gari la Muro walikuta pingu na bastola na hivyo wakamuagiza mwandishi huyo awapelekee risiti zinazoonyesha kuwa alinunua pingu hizo kihalali.
Kamanda huyo akadokeza kuwa pamoja na kumwambia awapelekee risiti, wanajua kuwa hangefanikiwa kuzipata kwa kuwa pingu haziuzwi ovyo na kwa kuwa mwenye mamlaka ya kumuweka nguvuni mtu ni polisi pekee.
Hadi jana, Muro alikuwa hajawasilisha risiti hiyo na Kova alisema jeshi lake linaendelea kumpa muda wa kutafuta kidhibiti hicho.
Lakini wanasheria waliozungumza na Mwananchi wanapingana na maelezo hayo ya Kamanda Kova.
Wakizungumza jana jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti, mawakili wa jijini Dar es salaam, Profesa Abdallah Safari na Mabere Marando walisema kwa mujibu wa sheria za nchini, hakuna kosa kwa mtu kukutwa na pingu.
"Kwa mujibu wa sheria za nchi, kukutwa na pingu si kosa ila utakuwa na kosa tena la jinai endapo ukikutwa na government stores (mavazi ya kijeshi na polisi ikiwemo kofia na mabuti) pamoja na kumiliki isivyo halali bunduki, bastola na hata risasi," alisema Profesa Safari.
Profesa Safari alifafanua kwamba katika mwenendo wa makosa ya jinai, hakuna kipengele kinachoonyesha kuwa ni kosa mtu kukutwa na pingu.
Naye Marando alisema hakuna kosa kukutwa na pingu kwa kuwa kifaa hicho ni kama bidhaa nyingine.
Alisema ndio maana duka la silaha huu vitu hivyo kwa hiyo kisheria si kosa kukutwa na pingu.
"Hakuna tatizo kukutwa na pingu kwa kuwa ni bidhaa na ndo maana inauzwa kwenye duka la silaha," alisema Marando.
Kova alidai polisi walikuta bastola aina ya CZ97B yenye namba A6466 iliyokuwa na risasi 10 iliyotengenezwa Jamhuri ya Check na pingu. Polisi pia walikuta miwani ambayo inadaiwa kuwa ya Wage pamoja na karatasi nyepesi (tissue) ambazo mhasibu huyo anadai alizisahau kwenye gari hilo.
Katika kanda ya video ilivyo mtandaoni, Muro anaonekana akieleza kuwa amekuwa na bastola na pingu hizo kwa takriban miaka minne na kwamba Kova anajua hilo, lakini anashangaa kwamba hataki kueleza ukweli wote.
Hata hivyo, Kova alikana kuwa na uhusiano na Jerry na tuhuma za kumpa pingu hizo huku akikanusha kuwepo na tukio la kutishiwa kwa mwandishi huyo wa zamani wa ITV na mtangazaji wa kipindi kinachoanza kupata umaarufu cha Usiku wa Habari kinachorushwa na TBC1.
Katika hatua nyingine watu mawili wamekamatwa juzi jioni katika mgahawa wa PR Camp Kinondoni jijini Dar es salaam kwa tuhuma za kushirikiana na Muro kufanya vitisho na kudai kiasi cha Sh10 milioni kwa Michael Karoli.
Polisi imedai iliwakamata watu hao juzi jioni wakiwa pamoja katika mgahawa huo na kwamba hawatawekewa dhamana kutokana na kutoaminika.
Walidai kuwa watu hao wataendelea kushikiliwa na polisi tofauti na Muro ambaye bado yupo nje kwa dhamana.
Kamanda Kova aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa watu hao walikamatwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema jana jioni.
Alisema kabla ya kukamatwa kwao, wapelelezi waliziona picha za kumbukumbu za watuhumiwa hao kwenye kamera maalum za CCTV ambazo hurekodi na kutunza kumbukumbu za matukio.
Kamanda Kova alisema watu hao wanaonekana kwenye mkanda wa kamera hizo wakiwa watatu na wanafanya mazungumzo kwenye meza pamoja na mlalamikaji.
Kova pia alisema kumbukumbu nyingine za CCTV zinaendelea kufuatiliwa katika mtindo huo kwa kutumia vifaa vya teknolojia ya kisasa ili kuondoa utata wa tukio hilo linalomkabili Jerry Muro.
"Tunaendelea kufuatilia tukio zima lilivyofanyika... kwa kutumia teknolojia za kisasa tutaweza kutambua ukweli wote na kuondoa ubishi au utata uliopo kwa lengo la kuweka mambo wazi,’’ alisema Kova.
Aliongeza kuwa baada ya kuonekana kwa watu hao kwenye mkanda wa CCTV, mlalamikaji Wage aliwatambua kuwa hao ndiyo waliotaka rushwa na kumtishia kwa kumtaka awape Sh10milioni.
"Hawa jamaa walitambuliwa katika gwaride maalum la kutambua wahalifu. Baada ya mlalamikji kuja aliwatambua lakini pia hawa jamaa katika kumbukumbu zetu tumegundua kuwa ni matapeli ambao tuliwahi kuwakamata wakihusika katika matukio mbalimbali na walifikishwa mahakamani ambako hadi sasa wana kesi,"alisema Kova.
Kova alidai kuwa upelelezi wa tukio hilo unaendelea kwa kasi na kwa umakini kwa kuzingatia sheria na taratibu.
This comment has been removed by the author.
ReplyDeleteThis comment has been removed by a blog administrator.
ReplyDelete