NI furaha iliyoje kukutana tena leo katika ukurasa huu? Sina shaka mambo yako ni mazuri kabisa na umekaa mkao wa kupokea maarifa mapya katika kuboresha zaidi uhusiano wako.
Naam! Leo ni siku maalumu kwa ajili ya kujibu maswali yenu ambayo mmekuwa mkinitumia kwa njia ya waraka pepe na ujumbe mfupi wa maneno (SMS).
Huwa napokea meseji zenu nyingi sana, lakini inakuwa vigumu kujibu zote, hasa kutokana na ukweli kwamba ni nyingi sana. Katika matoleo mawili mfululizo nitajibu meseji zenu.
Hata kama hujatuma, lakini kwa kufuatilia majibu ya maswali ya wenzako kwa namna moja ama nyingine unaweza kupata kitu fulani cha kuongeza ujuzi katika uhusiano wako na mpenzi wako.
Haya marafiki, hebu tuone maswali ya wasomaji.
INTERNET INANIPOTEZEA MPENZI WANGU
Naitwa Jenipher, nipo Mwanza. Ninaye mpenzi wangu ambaye nampenda sana kwakweli, mpaka sasa penzi letu lina mwaka mmoja. Tatizo la huyu bwana, anapenda sana kutafuta marafiki kwa njia ya mtandao wa internet.
Mpaka sasa nimeshamshtukia akianzisha uhusiano na wasichana nane tofauti, mwanzo nikimuuliza anasema ni marafiki wa ku-share idea na ku-reflesh mind, lakini nikichunguza zaidi nagundua kwamba kuna kitu kinaendelea, nikimbana anakiri na kuomba msamaha, cha ajabu baada ya muda mfupi sana anarudia tena tabia hiyo.
Niliwahi kumpima siku moja kwa kumwambia kwamba na mimi nahitaji marafiki wa kubadilishana nao mawazo, akachukia sana, akasema siku akigundua kwamba ninao ataachana na mimi moja kwa moja.
Hivi karibuni amepata msichana mwingine wa hapa hapa Mwanza, nilipomwuliza anasema ni rafiki tu! Kaka Shaluwa kwa utalaamu wako wa haya mambo ya mapenzi, kuna mapenzi ya kweli hapo au napoteza muda? Naomba msaada wako.
MAJIBU YA SHALUWA: Zipo site nyingi sana kwenye mitandao siku hizi kwa ajili ya kutafuta marafiki na wachumba, kwa ujumla wake si mbaya kama zikitumiwa vizuri. Kwa baadhi ya watu wasio wastaarabu, hutumia njia hizo kwa ajili ya kufanya mambo machafu.
Kwa maelezo yako, huyo bwana ni mmoja wao, ili kuthibitisha hilo, ndiyo maana ulipomwambia na wewe unataka marafiki wa kubadilishana nao mawazo amekuwa mkali, hiyo ni kwasababu anajua uchafu unaofanyika huko. Ukichambua majibu yangu kwa makini utajua la kufanya.
NAWEZA KUWA NA WAPEZI WAWILI KWA WAKATI MMOJA?
Wakati nasoma Sekondari nilianzisha uhusiano na kijana mmoja, lakini baadaye tulipotezana baada ya kuhama shule, kwakuwa wote hatukuwa na simu. Sasa nina mpenzi mwingine, lakini hivi karibuni amenipigia na kuanza kunieleza tena mambo ya mapenzi, hii ni baada ya miaka minne ya kupotezana.
Nimemweleza kwamba nina mpenzi mwingine lakini haelewi, anasema kama vipi niwe nao wote. Naomba msaada wako kaka yangu.
MAJIBU YA SHALUWA: Naanza kupata wasiwasi na huyo mpenzi wako wa zamani. Hakuna mapenzi ya kuchangia dada yangu. Mtu anayekupenda kwa dhati, lazima atakuonea wivu, kwanini yeye anakubali kuwa katika penzi la kuchangia? Tafakari...
DENTI MWENZANGU ANATAKA PENZI LANGU...
Kaka pole na kazi. Nina miaka 19, niko kidato cha nne, nimeokoka na nina rafiki ambaye yupo kama kaka yangu tangu siku nyingi, yupo kidato cha sita. Ametokea kunipenda, nami pia nampenda kama kakangu, lakini amekuwa akinieleza kwamba kutokana na hisia za kimwili tuwe tunafanya mapenzi ili kupunguza hamu na kujenga uaminifu. Nimejitahidi kumshauri lakini haelewi. Ukweli nampenda sana, nifanyeje?
MAJIBU YA SHALUWA: Kwa umri wako, unatakiwa kuzingatia zaidi masomo, andaa maisha yako ya baadaye. Mapenzi utayakuta, usipote muda kumuwaza mtu ambaye anataka tu, penzi lako. Wazazi wako wakijua kwamba unawaza upuuzi kama huu watasikitika sana. Kubwa zaidi, umesema wewe ni mlokole, kwenye maandiko iko wazi kabisa, kuzini ni dhambi, kwanini unapoteza muda kujadili dhambi?
SIYO MUWAZI, ANATAKA KUNIOA, NI MKWELI?
Hello kaka Shaluwa. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 22, ninaye mpenzi wangu ambaye nina miezi miwili tangu nimeanza kuwa naye katika mapenzi. Ni msiri sana wa mambo yake muhimu, hataki kuniambia yeye ni kabila gani, ana umri wa miaka mingapi n.k lakini anasisitiza kwamba anataka kunioa.
Nina wasiwasi naye, wewe unanishauri nini kaka Shaluwa? Naomba msaada wako.
MAJIBU YA SHALUWA: Inashangaza mpaka anafikia kukuambia kwamba anataka kukua hujamjua sawasawa! Kati ya mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kuwa wachumba (si ndoa) ni pamoja na kufahamiana kwa undani.
Ujue asili yake, kabila lake, dini, familia, kazi, tabia na mengine muhimu. Naanza kuaprwa na wasiwasi kwamba yawezekana ukaolewa na jambazi! Kuolewa si jambo la kukimbilia au la kubahatisha kama ambavyo baadhi ya watu wanafikiria. Tulia kwanza, acha papara, mchunguze umfahamu vizuri kabla ya kuchukua uamuzi wa kuingia katika ndoa.
Waswahili wanasema; Ndoa si lelemama. Ukitafakari vyema usemi huu, utaelewa vizuri maandishi yanayosomeka hapo juu.
Majibu ya maswali yenu yataendelea wiki ijayo...
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Secret Love.
No comments:
Post a Comment