ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 9, 2026

TMDA YANG'ARA TUZO ZA PRST - YATWAA TUZO YA BEST MEDIA RELATIONS TANZANIA 2026

 

Tuzo ya mshindi wa Uhusiano Bora na Vyombo vya Habari Tanzania 2026 (Best Media Relations in Tanzania 2026) aliyoshimda TMDA, 9, Oktoba.


Dodoma:


MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeendelea kung'ara katika sekta ya mawasiliano baada ya  kunyakua tuzo ya mshindi wa Uhusiano Bora na Vyombo vya Habari Tanzania 2026 (Best Media Relations in Tanzania 2026)

Tuzo hizo zimetolewa jana 8 Oktoba, 2026 katika hafla ya utoaji tuzo za Umahiri wa Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano (PR & Communications Awards ) iliyoandaliwa na Chama cha Uhusiano wa Umma Tanzania (PRST).

Tuzo hizo ni kielelezo cha umahiri wa taasisi hiyo katika matumizi ya vyombo vya habari kufikisha elimu sahihi kwa umma kuhusu masuala ya dawa na vifaa tiba na kuongeza  chachu ya kuendelea kudumisha weledi na ufanisi katika mawasiliano ya umma.

Tuzo hizo, hutolewa kila mwaka na PRST kwa kupigiwa kura na wadau mbalimbali.



Wednesday, October 7, 2026

TADB YATOA TUZO KWA WANAFUNZI 13 BORA SUA, YAAHIDI KUENDELEZA USHIRIKIANO WA KUKUZA VIPAJI

 

MOROGORO, Oktoba 7, 2026 | Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa tuzo kwa wanafunzi 13 wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) waliofanya vizuri katika masomo kwa mwaka 2026, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono ubora wa taaluma na kukuza wataalamu wa baadaye katika sekta ya kilimo.
Tuzo hizo zimetolewa katika hafla iliyofanyika SUA, ambapo TADB imesisitiza umuhimu wa kutambua na kuhamasisha wanafunzi wanaofanya vizuri, hususan katika taaluma zinazohusiana na kilimo, sekta ambayo ni muhimu katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania. 

Akizungumza kwa niaba ya TADB katika hafla hiyo, Afisa Rasilimaliwatu Mkuu wa Benki hiyo, Bi. Edna Nyatta, amesema ushiriki wa TADB katika utoaji wa tuzo hizo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano (MoU) yaliyopo kati ya TADB na SUA.

Amesema kupitia ushirikiano huo, TADB imeendelea kushirikiana na SUA katika kutambua, kuhamasisha na kuunga mkono wanafunzi wanaofanya vizuri, pamoja na kuweka mazingira yanayowawezesha vijana kupata fursa za kujifunza na kujenga uzoefu wa kazi.                   Bi. Nyatta amewapongeza wanafunzi waliotunukiwa tuzo hizo na kuwataka kuendelea kujifunza, kuwa wabunifu na kutumia maarifa wanayoyapata chuoni katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili Tanzania, hususan katika sekta ya kilimo.

“Tunawapongeza kwa kufanya vizuri. Mafanikio haya yasiishie darasani. Tunawahimiza kutumia elimu, ubunifu na maarifa mnayoyapata kutengeneza suluhisho la changamoto zinazolikabili Taifa, hasa katika sekta ya kilimo,” amesema Bi. Nyatta.

Aidha, Bi. Nyatta amesema TADB imeanzisha mpango wa ‘Learn with Us’, unaolenga kuwapa vijana fursa ya kujifunza kwa vitendo kupitia programu ya mafunzo kwa vitendo (Internship).

Amesema kupitia mpango huo, takribani wanafunzi 10 kutoka SUA tayari wamepata fursa za kufanya mafunzo ya vitendo TADB, huku wanafunzi sita kati yao wakifanikiwa kupata ajira za kudumu baada ya kumaliza mafunzo.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za TADB kuwaandaa vijana kwa soko la ajira kwa kuwapatia uzoefu wa vitendo na kuwaunganisha elimu wanayoipata chuoni na mahitaji halisi ya mazingira ya kazi.


Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda, ameishukuru TADB kwa kushiriki katika kutambua na kuwatia moyo wanafunzi waliofanya vizuri.

Prof. Chibunda ameiomba TADB kuendelea kutoa fursa za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi, akiwemo wanafunzi 13 waliotunukiwa tuzo katika hafla hiyo.

Amesema fursa hizo zitawasaidia wanafunzi kuunganisha elimu waliyoipata chuoni na uzoefu wa vitendo katika mazingira ya kazi, jambo litakalowaandaa zaidi kwa ajira na ujasiriamali katika sekta ya kilimo.

TADB imeipongeza SUA kwa kuendelea kutoa wataalamu wanaohitajika katika sekta ya kilimo na kuahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano na Chuo hicho katika kukuza vipaji, kutoa fursa za kujifunza kwa vitendo na kuwaandaa vijana kwa ajira na ujasiriamali katika sekta ya kilimo.

Ushirikiano huo unaendelea kuakisi dhamira ya TADB ya kushirikiana na taasisi za elimu katika kuwawezesha vijana na kujenga kizazi cha wataalamu wenye uwezo wa kuchochea maendeleo ya kilimo na uchumi wa Tanzania.









Saturday, October 3, 2026

MAADHIMISHO YA MIAKA 121 YA KUANZA KWA VITA VYA MAJIMAJI LEO

  



Na Oscar Mbuza, Kilwa


MKUU wa Wilaya ya Kilwa Mohamed Nyundo atakuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 121  ya kuanza kwa vita vya Majimaji katika kijiji cha Nandete, Tarafa ya Kipatimu wilayani Kilwa mkoani Lindi leo Oktoba 3, 2026.

Maadhimisho hayo yanafungwa leo  ikiwa ni siku ya tatu tangu kuanza kwa tamasha lake kuelekea siku ya kilele yakiwa yamezinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Adam Malima, ambapo pamoja na mambo mengine limebeba dhana ya utalii wa utamaduni kutokana na kushirikisha maonesho ya historia ya vita vya Majimaji, midahalo, vikundi vya ngoma na burudani, vyakula na vinywaji vya asili na kazi nyinginezo za mikono za kitamaduni.

Tofauti na miaka iliyotangulia, mwaka huu maadhimisho hayo yametawanywa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kilwa yakizinduliwa katika eneo la Kilwa Kisiwani na kufanyika pia katika maeneo ya Kilwa Kipatimu huku kilele kikiwa katika kijiji cha Nandete ambako Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa jengo la kisasa la Makumbusho ya Kuanza kwa Vita vya Majimaji ambalo ujenzi wake umefikia  zaidi ya asilimia 88 ili kukamilika.

Akizungumzia umuhimu wa jengo hilo, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Malikale, Wizara ya Maliasili na Utalii, William Mwita ambaye amekagua maendeleo ya ujenzi wake jana Oktoba 2, 2026, amesema litakuwa chachu katika kuchechemua utalii wa Kusini kutokana na eneo la Kilwa pia kuwa na vivutio vingi vya utalii.

“Kama inavyofahamika kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii na Serikali kwa ujumla inaweka mikakati mbalimbali ya kuchechemua vivutio vya utalii vilivyo Kusini mwa Tanzania hivyo litakapokamilika na kuanza kufanya shughuli zake ni wazi kuwa tutakuwa tumecheza kete muhimu sana katika kufungua utalii wa kusini,” amesema Mwita.

Aidha Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilwa (DAS) Yusuph Mwinyi amesema Serikali ya Wilaya kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wanachukua hatua mbalimbali za kuboresha Maadhimisho hayo kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kuyafanya kuwa miongoni mwa vivutio bora kabisa vya utalii nchini hivi karibuni.

*Kisa cha Wamatumbi kung’oa miche ya pamba shamba zima na kusababisha vita vya Majimaji*

Vita hiyo ilizuka ghafla kutokana na mzozo wa utumikishwaji wa wakazi wa eneo hilo wa kabila la Wamatumbi kwenye mashamba makubwa ya pamba yaliyokuwa yakimilikiwa na Serikali ya Mjerumani katika eneo la Nandete Julai 15, 1905, na baadaye kusambaa na kuwa moja ya vita kubwa ya kihistoria nchini ikipiganwa katika mikoa saba wakati huo ya Lindi, Mtwara, Pwani, Dar es Salaam, Morogoro, Iringa/Njombe na Ruvuma kabla ya kuhitimishwa Agosti 8, 1907.

Mzozo ulianza katika mashamba hayo makubwa ya pamba ya Nandete, katika Tarafa ya Kipatimu Lindi ambapo Wajerumani walioweka makazi yao katika kijiji cha Kibata kilometa kadhaa kutoka Nandete na kuanzisha mashamba hayo  waliwatumikisha Wamatumbi kwa lazima kwa kuwaamuru kupanda miche ya pamba na kuwaamuru tena wang’oe baadhi ya miche ili pamba hiyo ipate nafasi ya kukua vizuri hatua iliyowakasilisha Wamatumbi ambao waliamua kung’oa miche yote ya pamba  shambani kitendo ambacho pia  kiliwachukiza Wajerumani na kuanzisha mzozo ulioanzisha vita hiyo.

Aidha Wamatumbi pia walichoshwa na mateso ya kulazimishwa kuwabeba Wakoloni wa Kijerumani kwa machela umbali mrefu kutoka Kibata yaliko makazi yao hadi Nandete kwenye mashamba kila siku kwenda na kurudi huku mbebaji anayejikwaa njiani na kumuangusha Mkoloni akichapwa viboko 25 kwa 50, mateso yaliyokoleza moto wa hasira na kusababisha vita hiyo kuripuka.

Hadithi ya kusisimua zaidi katika vita hiyo ambayo umaarufu wake umeegemea zaidi katika Mkoa wa Ruvuma katika eneo la Songea ambako ilisambaa baadaye ni uwepo wa mtani wa Wamatumbi, Kinjeketile Ngwale kutoka kabila la Wangindo aliyewahamasisha Wamatumbi  kuingia katika vita kwa kutumia silaha za jadi huku akiwapa dawa ya asili akidai ina uwezo wa kugeuza risasi za Wajerumani kuwa maji, hatua iliyosababisha watu wengi  katika mikoa husika waliopigana vita hiyo dhidi ya Mjerumani kupoteza maisha kwa kupigwa risasi za moto.






Friday, October 2, 2026

WMA YATOA ELIMU YA VIPIMO KWA MAAFISA NA ASKARI WA JKT


Na WMA  - Dodoma


Wakala wa Vipimo (WMA)  Oktoba 1, 2026 ilifanya ziara ya kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo kwa Maafisa na Askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika Makao Makuu ya Jeshi hilo yaliyopo eneo la Buigiri, Chamwino jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoa elimu hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka WMA, Bw. Francis Olwero, alisema amefurahishwa na mwitikio mkubwa na shauku waliyoionesha askari na maafisa wa JKT.

"Askari ni sehemu ya jamii, maisha yao kama yalivyo ya wananchi wengine yamezungukwa na vipimo kuanzia asubuhi hadi jioni. Ndio maana WMA iliona ni busara kuwaelimisha," alisema Olwero.

Alisema katika elimu hiyo, WMA imewasisitiza askari kuhoji na kujiridhisha kama vipimo vinavyotumika katika biashara mbalimbali wanazonunua vimehakikiwa na WMA, ikiwemo gesi ya kupikia, maji, umeme, mizani za madukani na sokoni na hata pampu za mafuta.

Kwa upande wake, Private Fatma Mohamed alisema elimu hiyo imemfungua macho kama mwananchi kujua haki yake.

"Mimi  binafsi nimevutiwa na elimu hii, kama mwananchi nina haki ya kuhoji na kujiridhisha kama mizani ya buchani na hata pampu ya mafuta ya Sheli imehakikiwa na WMA kabla sijanunua bidhaa. Watanzania wenzangu hakikisheni mnafuatilia elimu inayotolewa na WMA ili kujua haki zenu kuhusu vipimo ili msipunjwe," alisema Private Fatma.

Naye Luteni Isaka Zacharia alisema ujio wa WMA umekuwa fursa muhimu kwa JKT.

"Tumejua kuwa tunapaswa kujiridhisha kuhusu matumizi ya vipimo sahihi kwenye huduma zinazogusa maisha yetu ya kila siku ikiwemo dira za maji na hata mita za umeme. Natoa rai kwa WMA kuendelea kutoa elimu ya vipimo kwa makundi mbalimbali katika jamii hususan wananchi wa kawaida na walioko vijijini," alisema Luteni Zacharia.

Private Michael Mdegela alisema elimu aliyoipata itamsaidia kuachana na mazoea ya kununua bidhaa bila kupima.

"Tumejifunza na tunaenda kuthibitisha hilo, maana kuanzia sasa tutaanza kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo na tutahoji kujiridhisha kama bidhaa tunazonunua zimepimwa kwa usahihi, hususan gesi ya kupikia. Kama gesi haijapimwa kwenye mzani uliohakikiwa na WMA, Siitaki!" alisisitiza.

Akifafanua kuhusu mkakati wa WMA, Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma kutoka WMA, Bi. Veronica Simba, amesema WMA inaendelea na zoezi la utoaji elimu ya vipimo kwa makundi mbalimbali katika jamii kwa kutumia mbinu mbalimbali za mawasiliano.

"Lengo letu ni kuhakikisha elimu ya matumizi sahihi ya vipimo inafika kwa kila mtu nchini, kwa kaulimbiu yetu isemayo, _Kipimo Sahihi ni Haki Yako_ alisema Bi. Simba.








Tuesday, September 29, 2026

ASNAT PHILBERT NDIYE MISS KARAGWE 2026

 


KARAGWE: Binti Asnat Philbert ametwaa taji la Miss Karagwe 2026 katika shindano lililofanyika usiku wa kuamkia Septemba 27, 2026, chini ya maandalizi ya The Boom Vibe.

Asnat mzaliwa wa Kata Kayanga alifanikiwa kuwashinda washiriki wenzake, katika shindano lililowakutanisha jumla ya warembo nane wakiwemo washiriki watano kutoka Karagwe na watatu kutoka Wilaya ya Kyerwa.

Ushindi huo unamuweka Asnat katika nafasi ya kuiwakilisha Karagwe kuelekea hatua inayofuata ya mashindano ya urembo ya Miss Kagera 2026, yanayotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2026.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baada ya shindano hilo, washindi watatu bora kutoka katika mashindano hayo wataungana na washindi kutoka wilaya nyingine za Mkoa wa Kagera, kwa ajili ya kushiriki katika tamasha la Miss Kagera 2026.





Tuesday, September 22, 2026

TFS YATUMIA MEL 2026 KUONYESHA FURSA ZA UHIFADHI, NYUKI NA UTALII



Na Omega Shemakala


ARUSHA. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umetumia Kongamano la Tano la Kitaifa la Wiki ya Ufuatiliaji, Tathmini na Ujifunzaji (MEL) 2026 kuonyesha namna uhifadhi wa misitu na nyuki unavyoweza kuleta fursa za afya, biashara, utalii na ustawi wa jamii, huku huduma ya apitherapy ikiwa miongoni mwa vivutio vinavyowavutia washiriki katika Banda la TFS, Ngurudoto, Arusha.

Mhifadhi wa TFS, Subira Matimbwa, amesema apitherapy ni miongoni mwa huduma zinazohusisha matumizi ya nyuki na bidhaa zitokanazo na nyuki, ambapo katika banda hilo washiriki wanapewa elimu kuhusu huduma hiyo pamoja na matumizi mbalimbali ya bidhaa za nyuki. Huduma hiyo imekuwa kivutio kwa washiriki wanaotaka kufahamu zaidi uhusiano kati ya nyuki, bidhaa zao na matumizi yake katika maisha ya binadamu.

Katika banda hilo, TFS pia inaendelea kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa misitu, ufugaji nyuki na utalii ikolojia, sambamba na kuonesha na kuuza bidhaa mbalimbali zitokanazo na nyuki, zikiwamo asali za aina tofauti, honey nuts na bidhaa nyingine zinazotokana na shughuli za ufugaji nyuki.

Afisa Utalii wa TFS, Salome Kivuye, amesema ushiriki wa TFS katika kongamano hilo unalenga pia kuwafahamisha washiriki kuhusu maeneo ya utalii yanayoweza kutembelewa wakati wakiwa Arusha, akitaja Ziwa Duluti pamoja na Maporomoko ya Napuru yaliyopo katika Msitu wa Kupandwa Meru kuwa miongoni mwa maeneo hayo.

Kivuye amesema maeneo hayo yanatoa fursa kwa washiriki kuchanganya shughuli za kongamano na utalii, huku akiwahamasisha kutumia huduma za kidijitali za TFS, ikiwamo e-Misitu, ili kupata taarifa na kurahisisha upatikanaji wa huduma za utalii katika maeneo yanayosimamiwa na TFS.

Kongamano hilo la siku tano linafanyika Arusha kuanzia Septemba 22 hadi 26, 2026, likiwakutanisha zaidi ya washiriki 1,500 kutoka Serikali, taasisi na wadau mbalimbali kujadili matumizi ya ushahidi wa kitafiti na takwimu katika kupima matokeo na kuboresha utekelezaji wa mipango ya maendeleo. Kaulimbiu ya kongamano hilo ni “Kutoka katika Ushahidi hadi Vitendo, Kuimarisha Tathmini kwa Maendeleo Endelevu.”

Akihusisha ushiriki huo na maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani, Kivuye pia amewaalika washiriki kuelekea Kondoa Rock Art Site kushiriki katika tukio litakalojumuisha shughuli mbalimbali za utalii na burudani, zikiwamo Outdoor Movie Night, Night Games, Guide and Tour, Bonfire, Painting, Paintball Game, Bata Pori Fun Run, Live Music Performance, Bata Pori Bike Ride Challenge, Karaoke Night pamoja na ziara za kuongozwa katika eneo hilo la urithi wa dunia.









MUHIMBILI YAPOKEA MSAADA WA TZS. 23 MIL KUTOKA LIONS CLUB INTERNATIONAL

  

 
 

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), leo imepokea vifaa vya kutolea huduma za tiba aina ya Infusion Pumps vyenye thamani ya Shilingi milioni 23, vilivyotolewa na Lions Club International, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ubora wa huduma za afya na kuongeza usalama wa wagonjwa wakati wa matibabu.

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi, Dkt. Mbonea Yonazi, ameishukuru Lions Club International kwa mchango huo muhimu, na kuongeza kuwa vifaa hivyo vitaenda kuongeza ufanisi wa matibabu na usalama wa wagonjwa.

“ Vifaa hivi vitasaidia kuboresha utoaji wa huduma na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma sahihi kulingana na mahitaji yao, huu ni mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa mgonjwa na ubora wa huduma tunazozitoa,”amesema Dkt. Yonazi.

MNH inaendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa katika huduma za afya, hatua inayochangia kuongeza ufanisi, usahihi na usalama wa huduma kwa wagonjwa.








SHEMDOE: MITAALA MIPYA KUJENGA MWANAFUNZI MWENYE UJUZI WA KUJIAJIRI



WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, amesema mitaala mipya ya elimu inalenga kumuandaa mwanafunzi kuwa na ujuzi wa vitendo utakaomwezesha kujiajiri na kuajirika baada ya kumaliza masomo yake.

Profesa Shemdoe amesema hayo leo Septemba 22, 2026, wakati akifungua Kongamano la Sita la Jumuiya ya Taasisi za Mitaala Afrika (ACA), linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali imefanya maboresho makubwa kutoka mtaala wa mwaka 2014 hadi mtaala wa mwaka 2023 ambao unajikita zaidi katika umahiri, ubunifu na ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira.

"Tumewekeza katika elimu ya amali. Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule za Amali na hadi sasa tumeshajenga shule 103 nchi nzima," amesema Prof. Shemdoe.

Aliongeza kuwa kongamano hilo limewakutanisha wajumbe kutoka nchi 22 za Afrika kujadili mustakabali wa mitaala barani humo.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, alisema ajenda kubwa ya kongamano hilo ni kuhakikisha Afrika inakuwa na mitaala inayozingatia utamaduni na utambulisho wa Mwafrika.

Dkt. Komba amesema kwa muda mrefu nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikitumia mitaala iliyonakiliwa kutoka kwa wakoloni, na sasa ni wakati wa kuwa na mitaala inayoandaa Mwafrika mzalendo.

"Ajenda kubwa ya kongamano hili ni kuhakikisha tunakuwa na mitaala inayolenga kumwandaa Mwafrika mzalendo ambaye atajisikia fahari kuitwa Mwafrika," amesema Dkt. Komba.

Kongamano hilo la siku nne linatarajiwa kuhitimishwa Septemba 25, 2026.