ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 10, 2026

TANI 9 ZA DAWA ZA KULEVYA ZAKAMATWA NCHINI TANZANIA

TANI 9 ZA DAWA ZA KULEVYA ZAKAMATWA NCHINI TANZANIA, BASI LA KING MASAI LANASWA

*Raia wa Kenya akamatwa akitumia biashara ya chai kuficha uuzaji wa dawa za kulevya.
*Basi la King Masai linaswa likisafirisha skanka.
*Mirungi iliyofungwa kama majani ya mwarobaini yakamatwa.
*Watumishi wa serikali wanaswa wakihusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini imetekeleza operesheni maalum mwishoni mwa mwezi Desemba 2025 na kufanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 9,689.833 za dawa za kulevya, sawa na tani 9. Pia pikipiki 11 na magari matatu yamekamatwa, huku watuhumiwa 66 wakitiwa mbaroni kwa tuhuma za kuhusika na biashara hiyo haramu.

Katika operesheni iliyofanyika Sinza C, mtaa wa Bustani, nyumba namba 16 jijini Dar es Salaam, Jefferson Kilonzo Mwende mwenye umri wa miaka 35, raia wa Kenya, alikamatwa akiwa na gramu 131.88 za heroin. Uchunguzi umebaini kuwa mtuhumiwa huyo, ambaye aliishi Tanzania tangu mwaka 2023, alikuwa akitumia biashara ya kuuza chai kama kificho cha kuendesha mtandao wa uuzaji wa dawa za kulevya.

Katika eneo la Wailes, Temeke jijini Dar es Salaam, mamlaka ilikamata pakiti 20 za skanka zenye uzito wa kilo 20.03, zilizokuwa zimefichwa ndani ya balo la nguo za mitumba na kusafirishwa kwa basi aina ya Scania la kampuni ya King Masai Tours, lenye namba za usajili AAM 297 CA kutoka Msumbiji. Basi hilo hufanya safari kati ya Nampula nchini Msumbiji na Tanzania. Watuhumiwa waliokamatwa ni Amasha Iddi Mrisho mkazi wa Buza, Dar es Salaam, pamoja na Seleman Juma Ally, raia wa Msumbiji.

Katika Kinyerezi, mtaa wa Majoka wilayani Ilala, watuhumiwa watatu Erick Ernest Ndagwa, Paul Blass Henry na Tido Emmanuel Mkude walikamatwa wakiwa wanasafirisha bangi yenye uzito wa kilo 193.66 kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam.

Kadhalika, kupitia ukaguzi uliofanyika katika kampuni za usafirishaji wa mizigo jijini Dar es Salaam, paketi 20 za mirungi zenye uzito wa kilo 9.54 zilikamatwa zikiwa zimefungwa na kufanana na majani ya mwarobaini yaliyokaushwa. Mizigo hiyo ilikuwa ikisafirishwa kutoka Kenya kuelekea Australia.

Katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Morogoro, Tanga, Lindi, Kilimanjaro, Njombe, Kigoma na Arusha, operesheni mbalimbali zilifanikiwa kukamata heroin gramu 37.34, skanka kilo 1.015, bangi kilo 7,969.98 na mirungi kilo 1,363.701. Pia mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 14 yaliteketezwa.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imesisitiza wananchi kutoa taarifa pale wanapoona viashiria vya biashara ya dawa za kulevya na kuepuka kubeba mizigo wasiyoijua. Mamlaka itaendelea na operesheni nchi nzima na kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika wote wa uhalifu huu.

No comments: