ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 25, 2010

Heri penzi la dhati la masikini kuliko la tajiri anayekuliza kila siku!

Tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana tena kupitia safu hii tukiwa wazima kabisa. Lakini wakati tunakutana hivi, tujue kabisa wapo wenzetu ambao hawana amani kabisa katika maisha yao.

Machozi hayakauki machoni mwao, sura zao zimetawaliwa na majonzi kila wakati, chanzo kikiwa ni mapenzi.

Wapo watu wanaofikia hatua ya kujuta kwanini wameletwa duniani kutokana na jinsi mapenzi yanavyowatesa. 

Lakini wakati hao wakiwa hivyo, kuna ambao maisha yao ni ya furaha kwa kuwa wamebahatika kuwa na wapenzi ambao wameyageuza maisha yao kuwa ya furaha.

Jamani, maisha ya furaha hayawezi kuwepo bila kuwa na mwenza ambaye atakuonesha mapenzi ya dhati. Ukishampata huyo bila kujali yuko na hali gani, muonekano gani wala elimu gani, mshikilie na usiwe tayari kumkosa licha ya kwamba, baadhi ya watu huenda wakajiuliza sababu ya kumpenda yeye.

Nilishawahi kusema huko nyuma kwamba kupenda ni upofu, moyo ukishapenda huwezi kuuzuia, endapo utauzuia unajiweka katika mazingira ya kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye moyo wako haujamridhia na mwisho ni kuja kuumizwa na kuishia kujuta.

Mwanzo wa makala haya nimesema kwamba, wapo watu ambao sasa hivi wanalia kwa sababu ya mapenzi. Ukijaribu kuchunguza utabaini kuwa, watu hao wako kwenye hali hiyo kwa sababu walidiriki kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na watu ambao hawakuwa na mapenzi ya kweli kwao. 

Yawezekana waliwapendea pesa zao, muonekano wao ama kitu kingine lakini walishindwa kufahamu kuwa, hivyo si vigezo vya kumchagua mwenza sahihi. Tukikosea katika hili tujue huko baadae ni lazima tutakuja kutoa machozi na asiwepo mtu wa kutufuta.

Tamaa ya pesa imewafanya watu wengi kuingia katika mapenzi ambayo mwisho wa yote ni vilio. Hivi unapompenda mwanaume kwa sababu ya pesa zake unatarajia nini? Watampenda wangapi kwa sababu hiyo? Jaribu kuchunguza na utagundua kuwa wanaume wengi wenye pesa ni vigumu kutulia na mpenzi mmoja, je wewe uko tayari ‘kushea’ penzi?

Hata wale ambao wameoa ukiwafuatilia sana utagundua kuwa, wana vinyumba vidogo vingi nje ya ndoa. Ni wachache sana ambao wana pesa zao na wakawa watulivu katika mahusiano yao.

Wenye pesa wanakuwa na mapenzi ya kweli?
Hatuwezi kuwahukumu wote wenye pesa kuwa hawana mapenzi ya kweli, wapo ambao wamejaaliwa busara na uelewa wa hali ya juu kwamba, kuwa na wapenzi wengi sio ujanja wala sifa bali inaweza kuwa sababu ya kujipunguzia umri wao wa kuishi. Lakini sasa, wengi wenye pesa wamekuwa wakitajwa kuwa na tamaa ya kuwa na wapenzi wengi kiasi kwamba ukimpata mtu wa dizaini hii, usitarajie mapenzi ya dhati. 

Chunguza na utabaini kuwa, ni wanawake wachache sana ambao wameolewa au wana uhusiano wa kimapenzi na wanaume wenye pesa na wakawa na maisha ya furaha.

Wengi kusalitiwa, kunyanyaswa na kutishiwa kuachwa ndiyo maisha yao ya kila siku. Wengine sasa wameamua kutowafuatilia waume zao wakihofia kujipa presha kwakuwa wanawajua kuwa hawajatulia.

Ukifikia hatua hiyo ndipo linapokuja lile swali kwamba, kuna faida gani sasa ya kuwa na mwanaume mwenye pesa lakini akawa haoneshi mapenzi ya dhati kwako? Sikatai maisha bila pesa ni lazima ugumu utakuwepo lakini utakuwa hujafanya maamuzi sahihi kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na mwanaume eti kwakuwa tu ana pesa.

Pesa sawa lakini, penzi la dhati analo kwako? Je ametulia? Hakika ukitokea kupendwa na mwanaume ambaye unajua ana uwezo, tafakari mara mbili mbili kabla ya kumkubalia na wala usimkubalie haraka haraka kwa sababu ya pesa zake kwani zinaweza kuja kukutokea puani.

Masikini na penzi lake la dhati kwako vipi?
Huu nao ni mtihani mkubwa sana hasa katika maisha yetu ya sasa. Unakuta mwanaume hana uwezo kiivyo kipesa lakini anaonesha kukupenda kwa dhati, unafanyaje? Nishawahi kusema huko nyuma kwamba, mapenzi yanaweza kuwepo bila pesa kwa sababu vitu hivyo havina uhusiano wa karibu. 

Ndiyo maana leo hii tunaona binti mzuri mwenye uwezo wake kipesa anaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanaume hohehahe, kwa nini? Kwa sababu tu amempenda na yeye akaonesha mapenzi ya dhati kwake. 

Tutambue tu kwamba, masikini nao wanayo nafasi ya kupendwa na inashauriwa na wataalam wa masuala ya mapenzi kuwa, ni bora umpe nafasi mtu mwenye mapenzi ya dhati kwako asiye na uwezo kiivyo kuliko kukubali kuwa na tajiri ambaye haishi kukuliza.

Naandika haya nikiwa na ushahidi wa wanawake wengi ambao wameolewa na wanaume wenye pesa lakini leo hii wanalia na kuona ni heri hata wangeolewa na watu masikini ambao wangewapa mapenzi ya dhati. Wapo wanaume ambao wameingia katika uhusiano na wanawake wenye pesa zao lakini leo hii pesa walizozifuata wanaziona ni chungu. 

Nihitimishe kwa kusema tu kwamba, usiulazimishe moyo wako kumpenda mtu kwa sababu ya pesa zake, mpende mtu ambaye moyo wako umeridhia kuwa naye hasa kwa kuwa anakupa kile ambacho moyo wako unakitaka, mambo ya pesa yaje baadae! Tukutane tena wiki ijayo kwa makala nyingine.

2 comments:

Anonymous said...

hivi penzi lipo kati ya wazungu tu.Kila siku mnatuwekea wazungu ina maana weusi hawapendani kidhat au la?

Anonymous said...

nikweli wanzungu wanapendana tofauti na weusi ,weusi hata akiwa na mke lazima nje awe na mwanamke ndio maana mara kwa mara tunatoa mfano wa wazungu