ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 27, 2010

Tanzania yaingia ubia umeme wa upepo


Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Power Pool East Africa, Machwa Kagoswe, akitoa maelezo kwa Naibu waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu (katikati)kuhusiana na eneo litakalotumika kuzalishia umeme wa upepo mkoani Singida juzi. Serikali imeingia ubia kupitia Shiriaka la Maendeleo la Taifa (NDC) na kampuni binafsi ya Power Pool East Aftrica ili kuzalisha umeme huo kuanzia mwakani
Mpoki Bukuku
Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), limeingia ubia na Kampuni ya Power Pool East Africa kuzalisha umeme wa upepo mkoani Singida utakaogharimu zaidi ya Sh180 bilioni.
Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Lazaro Nyalandu, alisema tayari makubaliano yamesainiwa na NDC na kwamba, serikali itakuwa ikimiliki asilimia 51 ya hisa na nyingine zitakuwa za mwekezaji.
Nyalandu alisema mradi huo utakuwa wa gharama nafuu katika uzalishaji utaingizwa kwenye gridi ya taifa na kwamba, kwa kuanzia zitazalishwa megawati 50 na baadaye zitaongezwa kulingana na uwezo wa wabia hao.
 “Tokea kuanza kufungwa kwa mitambo, itachukua takriban miezi 15 ili umeme uingie gridi na hii itakuwa ufumbuzi wa matatizo ya umeme kwa sasa,” alisema Nyalandu.
Waziri huyo alisema katika makubaliano hayo, serikali itakuwa ikimiliki hisa za asilimia 51, nyingine zitabaki kwa mwekezaji binafsi na ujenzi unatarajia kuanza muda wowote.
Mkurugenzi wa Viwanda wa NDC, Alley Mwakibolwa, alisema ujenzi wa mitambo ya kutumia upepo kutasaidia kuzalisha umeme mapema, kwani mitambo ya aina hiyo huchukua muda mfupi kuwekwa ikilinganishwa na ile ya maji au gesi.
”Tutajitahidi mradi huu uende kwa kasi kubwa, kwani kwa kuanzia tutazalisha megawati 50 na baadaye tutaongeza 50 ili kuingia gridi ya taifa,” alisema Mwakibolwa.
Mwakibolwa alisema kwa kuingia ubia huo, itasaidia kupunguza gharama kwa taifa, kwani ni rahisi kuliko umeme wa aina nyingine na kuwa shirika hilo litalinda maslahi ya taifa na wananchi.
”Tuna maeneo mengine ambayo tunaweza kuzalisha umeme, ikiwamo wa makaa ya mawe na kwa mikoa ya kusini machimbo ya makaa ya mawe tunaweza kuzalisha zaidi ya megawati 1,800 wakati mahitaji ya nchi kwa sasa ni 800,” alisema.
Alisema nchi itaanza kuuza umeme kwa nchi za jirani hususan za Afrika Mashariki na kwamba, tayari viongozi wa nchi hizo wamekubaliana kuachia Tanzania kuzalisha umeme kwa ajili ya nchi zote tano.
Mkurugenzi Mtendaji wa Power Pool East Afrca, Machwa Kagoswe, alisema wameagiza mashine zinazoweza kumudu upepo wa Singida, kwani kwa kawaida nchi za Ulaya zinazalisha umeme wenye kasi ya mita tano kwa sekunde wakati wa Singida hufikia hadi mita 21 kwa sekunde.
“Huu ni umeme mkubwa ndiyo maana tumeweka oda maalum ya mitambo itakayoweza kuhimili upepo huu, natumaini hii itakuwa njia rahisi ya kuzalisha umeme mwingi kwa gharama nafuu,” alisema.

                          Chanzo:Mwananchi

No comments: