ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 27, 2011

Binti wa miaka 11 ajifungua salama

Image
WAKATI Serikali ikikuna kichwa kukabiliana na wimbi la mimba kwa wanafunzi, binti mwenye umri wa miaka 11 mkazi wa Ngarananyuki mkoani Kilimanjaro, Nangakwa Lowasa, amejifungua mtoto mwenzie salama nyumbani kwake kwa usaidizi wa wakunga wa jadi. 


Binti huyo kutoka jamii ya Kimasai iliyoko wilayani Siha mkoani hapa, amewashangaza wengi baada ya kujifungua bila kupata tatizo lolote, na kwa sasa anaishi na mume wake aliyejulikana kwa jina moja la Narida, anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30 hadi 35. 

Gazeti hili wiki hii lilizungumza na binti huyo katika wodi ya wazazi ya Hospitali ya Wilaya ya Hai iliyoko Machame alikolazwa baada ya kuugua malaria mara baada ya kujifungua ambapo licha ya kutokwenda shule kabisa katika maisha yake, pia hajui hata lugha ya Kiswahili. 

Kutokana na mazingira aliyokulia, Nangakwa aliyekuwa akizungumza kwa msaada wa mfasiri, haoni tatizo lolote kwa yeye kujifungua mtoto na hata kuwa na mume. 

Binti huyo alisema aliolewa mwaka jana na kwa sasa anaishi na mume wake Narida, na kwamba wakati wa kujifungua, ingawa ilikuwa nyumbani na kwa njia za kienyeji, hakupata tatizo lolote.

Pamoja na kwamba katika hali ya kawaida, alikuwa akihatarisha maisha yake kwa kujifungulia nyumbani, Nangakwa hakuwa na namna kwa kuwa kwa mujibu wa maelezo yake, hajawahi kwenda kliniki tangu alipopata ujauzito mpaka alipojifungua. 

Binti huyo alisema akiwa na umri wa miaka mitano alikuwa tayari ameshalipiwa mahari na mume wake huyo na alipofikisha miaka kumi, wazazi wake walimshauri kuolewa, ambapo alisisitiza kwamba kwake ni jambo la kawaida. 

Alisema hajawahi kwenda shule ndio maana hajui kuongea hata kidogo lugha ya Kiswahili na maisha yake na ya mumewe ni ya ufugaji. 

Mama mkwe wake ambaye alikuwa akimuuguza hospitalini hapo, alikataa kuzungumza na gazeti hili na kwa jinsi ilivyokuwa, inaonekana alikuwa akijua kuwa ni kosa kisheria kwa kuwa alisema anahofia kuchukuliwa hatua na alifikia hatua ya kumkimbia mwandishi. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya 1971, inayopingwa na wana harakati, mtoto wa kike anaweza kuolewa akiwa na umri wa miaka 14, lakini baada ya wazazi kuafiki achukue hatua hiyo. 

Hata hivyo, sheria hiyo inapingana na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya 1998, ambayo imeeleza wazi kuwa mtoto yeyote chini ya miaka 18 akiingiliwa kimwili atakuwa amenajisiwa. 

Gazeti hili lilizungumza na wagonjwa waliokuwa katika wodi hiyo ambapo wote walielezea kushangazwa na binti huyo kujifungua mtoto, ambapo walisema ni uonevu mkubwa usio stahili kwa jamii ya sasa. 

Wagonjwa wenzake hao walisema binti huyo bado anahitaji malezi ya baba na mama, pamoja na haki yake ya msingi ya kwenda shule. Hata hivyo, waliomshauri aolewe akiwa na miaka kumi tu ni wazazi hao ambao walipaswa kumpa malezi bora. 

Kutokana na hali hiyo, mmoja wa wagonjwa hao ambaye hakutaka kutaja jina lake, aliiomba Serikali kuwachukulia hatua wazazi wa mtoto huyo pamoja na mumewe. 

Pia aliiomba Serikali itoe elimu ya athari za mimba za utotoni vijijini hususani kwa jamii ya Wamasai, ili waondokane na hali hiyo inayowanyima fursa watoto wa kike kukosa malezi ya baba na mama pamoja na elimu.


CHANZO:HABARI LEO:

No comments: