Waandishi Wetu
HATUA ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kukataa kuzungumza chochote kuhusu kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans katika kikao chake na Kamati ya Nishati na Madini, pamoja na kukaa kimya bila kujibu hoja na barua za Dowans kutaka wakae mezani, imedaiwa ni kutokana na shirika hilo kutojua, wala kuhusika na ujio wa kampuni hiyo nchini.
Habari za kiuchunguzi ambazo zilithibitishwa na baadhi ya watendaji ndani ya Tanesco zinaeleza kuwa shirika hilo lilifanya makusudi kutozungumzia Dowans kwa kuwa halijawahi kukutana wala kuingia mkataba wowote na kampuni hiyo ya uzalishaji umeme wa dharura, inayomilikiwa na mfanyabiashara wa Oman, Suleyman Al Adawi.
Kwa mujibu wa habari hizo, uongozi wa Tanesco chini ya Mkurugenzi wake, William Mhando uligoma kuzungumzia Dowans ukidai kuwa hauna mkataba wowote na kampuni hiyo.
Taarifa za msimamo huo wa Tanesco zimekuja siku moja tangu kampuni ya Dowans Tanzania, kupitia kwa mkurugenzi wake wa Fedha, Stanley Munai kuilaumu hadharani Tanesco, kwa kile alichodai kuwa ni uongozi wa shirika hilo kukataa kufanya mazungumzo ambayo yangeweza kuondoa sintofahamu iliyopo baina ya pande hizo.
Munai alisema Tanesco wanapaswa kulaumiwa kwa kuchangia tatizo la mgawo wa umeme nchini kwani Dowans mara kadhaa wametaka mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mivutano iliyopo ikiwa ni pamoja na deni la Sh94 bilioni ambalo linatokana na tuzo iliyopewa Dowans katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa kibiashara, ICC.
Mmiliki wa Dowans, Al Adawi alikuwepo nchini siku chache zilizopita ambapo alikutana na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari nchini, na kueleza nia yake ya kukutana na Serikali ili kujadili mvutano kuhusu malipo ya tuzo ya Sh94 bilioni anazotakiwa kulipwa baada ya kushinda kesi ICC.
Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya kuaminika toka ndani ya Tanesco, msimamo wa menejimenti ya shirika hilo ni kutowasha mitambo ya Dowans na kwamba kwao ni bora kuongeza mafuta katika mitambo ya IPTL iliyopo Tegeta ili iongeze uzalishaji toka megawati 10 za sasa.
"Tanesco haipo tayari kuwasha mitambo ya Dowans wala kuzunguza nao kwani haijawahi kukutana, kuzungumza wala kuingia mkataba wowote na Dowans. Ni bora kuongeza mafuta mitambo ya IPTL izalishe umeme zaidi ya megawati 10 za sasa, " alisema mmoja wa watendaji wa Tanesco aliyeomba kuhifadhiwa jina lake kwa kuwa si msemaji wa shirika hilo.
Suala la IPTL kufanya kazi chini ya uwezo wake wa kawaida lilithibitishwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba alipozungumza na waandishi wa habari huku akiitaka Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kununua mafuta yatakayowezesha mitambo hiyo kuzalisha kiasi kikubwa zaidi cha umeme.
Kadhalika Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) katika taarifa iliyotolewa jana na mwenyekiti wake, Felix Mosha, wameitaka serikali kufanya mazungumzo na kampuni ya IPTL ili izalishe umeme kwa kiwango cha juu kama moja ya njia ya kusaidia pia kutatua tatizo lililopo.
Habari zinasema Tanesco inadai kuwa mitambo hiyo ilifikishwa ilipo sasa na serikali ambayo iliielekeza tu kuanza kuitumia hivyo kwa hali ya sasa anayepaswa kuzungumza na Dowans ni serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini.
"Msimamo wa Tanesco ni kuwa serikali au Wizara ya Nishati na Madini ndiyo izungumze na Dowans kwa kuwa ndiyo walioileta mitambo Ubungo,Tanesco haihusiki, vinginevyo suala hilo lirejeshwe Bungeni likajadiliwe na kutolewa uamuzi," kinaeleza chanzo chetu ndani ya Tanesco.
Kilisema kwa Tanesco, Dowans ni kama mwanamke aliyefumaniwa, mumewe akamtembeza mitaani utupu na kumuacha hivyo hawezi kumrudia au mtu wa jamii husika kumuoa tena.
"Kuna kabila moja kanda ya ziwa mwanaume akimfumania mkewe, humtembeza mitaani akiwa utupu na kumuacha hivyo hawezi kumrudia, ndivyo ilivyo kwa Tanesco, Dowans ni kama mwanamke wa aina hiyo utamuoaje?, serikali yenyewe ndiyo inayoweza kuamua siyo Tanesco," alisema.
Aliongeza, "Serikali ndiyo izungumze na Dowans na kuamua kwani ndiyo iliyoingia mkataba na Dowans na kuileta nchini siyo Tanesco."
Mwananchi ilimtafuta mkurugenzi wa Tanesco William Mhando ili atoe ufafanuzi wa taarifa hizo lakini alipopatikana alisema," Ahh Mwananchi, unaweza kunipa muda nakula kwanza."Alipoulizwa baada ya muda gani atakuwa tayari alisema, "Nipe nusu saa hivi."
Maelezo ya Tanesco
Hata hivyo Mhando alipopigiwa simu mara kadhaa iliita bila kupokelewa ambapo baadaye Meneja Mahusiano wa shirika hilo Badra Masoud alilipigia simu gazeti hili ili kujua shida yake, lakini naye baada ya kuulizwa kuhusu taarifa hizo alionyesha msimamo huo.
"Kuhusu Dowans kwa sasa hatuzungumzi chochote, tutakapokuwa tayari tutazungumza kwani hakuna cha kuficha," alisema Badra na kuongeza:"Hawa watu (Dowans) bado tuna kesi nao, ninyi mnataka tuzungumze nao nini?, subirini tu tutakapomalizana nao mahakamani tunatunguza na kila kitu kitawekwa wazi".
Hata hivyo, habari zaidi zinasema kuwa menejimenti ya Tanesco imeshindwa kuweka wazi ukweli huo mbele ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini inayoongozwa na Januari Makamba mbunge wa Bumbuli kwa kuwa kila inapotaka kufanya hivyo anakuwepo Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja hivyo kukosa uhuru wa kweli kuzungumza.
Jumatano wiki hii Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, ikiongozwa na Makamba ilikutana kwa zaidi ya saa tano na uongozi wa Tanesco huku kukiripotiwa kuwapo kwa mvutano mkubwa baina ya pande hizo ambapo Tanesco walidaiwa kukataa kujadili suala la Dowans.
Tanesco ilidaiwa kukataa kuzungumzia suala la Dowans nje ya Mahakama, pia suala la kuwashwa kwa mitambo ya kampuni hiyo ili itoe megawati 100 za umeme kwa lengo la kupunguza makali ya mgao wa nishati hiyo unaondelea sasa.
Hata hivyo, akizungumzia hitimisho la kikao baina yao na Tanesco Makamba alisema suala la kuamua kuwasha mitambo au la, ni la shirika hilo na wao ni washauri tu wa namna ya kuondoa mgao wa umeme nchini.
Alisema wameliagiza shirika hilo kuhakikisha hakuna utata wowote wa kisheria iwapo wataamua kuingia mkataba na kampuni hiyo na kushauri uwe wa muda mfupi usiozidi miezi minne.
Juzi kamati hiyo ya makamba ilitembelea mitambo ya kuzalisha umeme jijini Dar es Salaam ikiwemo wa Dowans, Songas, IPTL na mtambo wa Tanesco wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Ubungo.
Hata hivyo, habari za uhakika zinasema kuwa serikali ipo katika harakati za kumaliza utata baina Tanesco na Dowans ambapo juzi iliwakutanisha Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhando, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, Gavana wa Benki Kuu, Beno Ndullu na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo.
Kwa mujibu wa habari hizo watendaji hao walikutana usiku katika ofisi za Wizara ya Fedha ambapo uchunguzi unaonyesha kuwa kikao chao kilianza majira ya saa moja usiku.
Badra mbali ya kukiri kuwepo kwa kikao hicho, alisema ni mapema mno kueleza kilichojadiliwa akidai kilikuwa kikao cha kawaida, lakini akasema kwamba wakati ukifika yatokanayo na kikao hicho yatatolewa kwa umma.
"Kikao cha jana (juzi) ni cha kawaida na si mara ya kwanza kufanyika, vikao kama hivyo hufanyika mara kwa mara na hujadili mambo ya kawaida ya kiutendaji, kwa sasa yaliyojadiliwa siwezi kuyaweka wazi ila wakati ukifika tutawataarifu kwani hakuna cha kuficha,"alisema Masoud.
Kauli ya Ngeleja
Jana gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza kwa simu na Waziri Ngeleja ambaye alisema "hata ukinibana vipi mimi siwezi kuzungumzia masuala haya, utanichinja tu rafiki yangu".
Ngeleja alisema Tanesco wanapaswa kutoa ufafanuzi wa masuala yote kuhusu umeme kwa sababu wana bodi na menejimenti inayojitegemea.
Kuhusu Dowans Ngeleja alisema pia yeye hawezi kulizungumzia suala hilo kutokana na kesi iliyopo mahakamani. "Tanesco wana uamuzi, wakitaka kuingia mkataba mfupi au wa aina yoyote ni uamuzi wao maana vyombo vyote vya uamuzi vipo," alisema Waziri huyo na kuongeza:
"Nadhani watazungumza tu kama walivyoahidi pengine kwa sasa hawajajipanga na kama unavyojua pressure kutoka kwenye public (msukumo wa umma) ni mkubwa sana kutokana na matatizo haya ya Nishati ya umeme".
Akizungumzia suala la kuwa kikwazo kwa Tanesco pale walipokutana na kamati ya bunge ya Nishati na Madini, Ngeleja alisema kwa mujibu wa Kanuni za bunge toleo la mwaka 2007 kila waziri wa kisekta ni mjumbe katika kamati husika.
"Mimi sikuvamia kamati kama inavyodaiwa, wala sikwenda wa lengo lolote baya bali mimi ni mjumbe wa kamati ile kama kanuni zetu za bunge zinavyosomeka, tena bora umeniuliza hili maana wapo watu wanaweza kudhani mimi ni mvamizi wa vikao vya kamati,"alifafanua.
Waziri huyo akizungumzia suala la IPTL alisema yeye hawezi kufahamu sababu za kampuni hiyo kutozalisha umeme kwa kiwango cha juu cha uwezo wake, lakini akabainisha kuwa inawezekana ni kutokana na mahitaji waliyopewa na Tanesco.
"Mimi niko ofisini ndugu yangu, mambo mengine siwezi kuyaelewa maana inawezekana mahitaji ya Tanesco kutoka IPTL ni kiasi hicho kinachozalishwa ama pengine kuna hitilafu kwenye mitambo huwezi jua,"alisema Ngeleja huku akilishauri gazeti hili kuwasiliana na mfilisi wa IPTL aliyemtaja kwa jina moja la Rugonzibwa ili kupata ufafanuzi wa kina.
CTI nao waitaka Dowans
Naye Mwandishi Leon Bahati, anaripoti kuwa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) limetoa msimamo wake likisema kwamba suluhisho la haraka la kuokoa uchumi wa nchi usiendelee kuteketea ni kuruhusu mitambo ya kampuni ya Dowans iwashwe na kupunguza tatizo la uhaba wa umeme unaolikumba Taifa kwa sasa.
CTI imeitaka serikali pia kufanya mazungumzo na kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ili izalishe umeme kwa kiwango cha juu kama moja ya njia ya kusaidia pia kutatua tatizo lililopo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa CTI, Felix Mosha katika taarifa yake iliyotoa msimamo wa shirikisho hilo baada ya kutafakari kwa kina tatizo la umeme nchini.
“Tumetafakari kwa kina na kutambua kuwa pamoja na suala la Dowans kuingiliana na misimamo ya kisiasa, njia pekee na ya busara inayofaa kwa sasa kutatua tatizo hili la umeme ni kuruhusiwa kwa mitambo ya Dowans kufanya kazi,” alisema Mosha kupitia taarifa hiyo aliyoitoa jana.
Alisema watumiaji wakubwa wa umeme kupitia CTI wapo tayari kufanya mazungumzo na Tanesco ili kuangalia namna watakavyoshirikiana kukabiliana na gharama za wazalishaji wa nishati hiyo muhimu kwa uchumi.
Mosha alielezea kilio cha wenye viwanda nchini ambacho kiliwasilishwa kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwamba tatizo la umeme nchini limewasababishia hasara kubwa ambayo inatishia kusimamisha uzalishaji.
“Viongozi pamoja na baadhi ya wanachama wa CTI Februari 21, mwaka huu walikutana na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na kuwaelezea kwa kina jinsi wanavyopata hasara na kutishia kuviua,” alisema Mosha.
Kwa sababu hiyo akasema ni jambo la busara kutumia mitambo ya Dowans na IPTL kwa kuwa tayari ipo nchini na ndio suluhisho la haraka linaloweza kuchukuliwa kwa sasasa.
Mgawo wa Umeme kuendelea
Wakati hayo yakijiri, imebainishwa kuwa mgao wa umeme utaendelea kuwa tishio huku ikielezwa kuwa mitambo ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) haina mafuta ya kutosha kuzalisha kiwango cha umeme kinachotakiwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Makamba iliwaambia waandishi wa habari jana kuwa IPTL inashindwa kuzalisha umeme kwa kiwango kikubwa kinachotakiwa kutokana na kukosa mafuta ya kutosha.
Kutokana na hali hiyo, Makamba aliitaka Wizara ya Fedha (Hazina) kutoa fedha za kutosha kwa Kampuni hiyo ili iweze kununua mafuta ya kutosha kwa ajili ya kuendeshea mitambo hiyo ambayo ina uwezo wa kuzalisha megawati 100.
“Kwa sasa IPTL inazalisha megawati 10 mpaka 50 tu, jambo ambalo halitoshelezi kulingana na uwezo wa kuzalisha umeme katika mitambo hiyo,” alisema Makamba.
Alisema kutokana na hali hiyo Hazina inatakiwa kutoa fedha ya kutosha ili uzalishaji huo ufikie angalau megawati 80 na kwamba kama Hazina hawatafanya hivyo machungu ya mgawo wa umeme yataendelea.
Makamba alifafanua hayo muda mfupi baada ya kutoka kuzungumza na wadau mbalimbali wa umeme katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi ndogo za bunge.
Makamba pia aliiagiza Shirika la Petroli nchini (TPDC) liipatie Kamati yake bei halisi ya gesi ilivyo nchini kutokana na bei ya nishati hiyo kupanda mara kwa mara.
“Bei ya gesi imekuwa ikipanda mara kwa mara, hivyo nimeiagiza TPDC kutupa maelezo kwa maandishi yanayoeleweka kuhusu bei halisi ya gesi,” alisema Makamba.
Alisema kuwa mitambo ya kusafirishia gesi iliyopo nchini imezidiwa uwezo kutokana na kuongezeka kwa viwanda na mashirika mbalimbali ambayo inatumia nishati hiyo, hivyo aliishauri serikali waongeze uwezo wa mitambo hiyo.
“Kwa sasa gesi inayotakiwa nchini ni mita za ujazo 15,000 ambazo ni sawa na megawati 10 kwa mwezi jambo ambalo hatuwezi kulimudu, serikali itoe fedha kwa ajili ya kubadilisha mitambo hii,” alisema Makamba.
Kamati hiyo ambayo pia ilipatiwa mikataba ya gesi inatarajiwa kukutana tena Jumatatu ijayo kwa ajili ya kufanya majumuisho.
Kutokana na hali hiyo, Makamba aliitaka Wizara ya Fedha (Hazina) kutoa fedha za kutosha kwa Kampuni hiyo ili iweze kununua mafuta ya kutosha kwa ajili ya kuendeshea mitambo hiyo ambayo ina uwezo wa kuzalisha megawati 100.
“Kwa sasa IPTL inazalisha megawati 10 mpaka 50 tu, jambo ambalo halitoshelezi kulingana na uwezo wa kuzalisha umeme katika mitambo hiyo,” alisema Makamba.
Alisema kutokana na hali hiyo Hazina inatakiwa kutoa fedha ya kutosha ili uzalishaji huo ufikie angalau megawati 80 na kwamba kama Hazina hawatafanya hivyo machungu ya mgawo wa umeme yataendelea.
Makamba alifafanua hayo muda mfupi baada ya kutoka kuzungumza na wadau mbalimbali wa umeme katika kikao kilichofanyika kwenye ofisi ndogo za bunge.
Makamba pia aliiagiza Shirika la Petroli nchini (TPDC) liipatie Kamati yake bei halisi ya gesi ilivyo nchini kutokana na bei ya nishati hiyo kupanda mara kwa mara.
“Bei ya gesi imekuwa ikipanda mara kwa mara, hivyo nimeiagiza TPDC kutupa maelezo kwa maandishi yanayoeleweka kuhusu bei halisi ya gesi,” alisema Makamba.
Alisema kuwa mitambo ya kusafirishia gesi iliyopo nchini imezidiwa uwezo kutokana na kuongezeka kwa viwanda na mashirika mbalimbali ambayo inatumia nishati hiyo, hivyo aliishauri serikali waongeze uwezo wa mitambo hiyo.
“Kwa sasa gesi inayotakiwa nchini ni mita za ujazo 15,000 ambazo ni sawa na megawati 10 kwa mwezi jambo ambalo hatuwezi kulimudu, serikali itoe fedha kwa ajili ya kubadilisha mitambo hii,” alisema Makamba.
Kamati hiyo ambayo pia ilipatiwa mikataba ya gesi inatarajiwa kukutana tena Jumatatu ijayo kwa ajili ya kufanya majumuisho.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment