Advertisements

Wednesday, March 16, 2011

Mume na mkewe wauawa kinyama

  Walivamia usiku wamelala

Vikongwe wawili ambao walikuwa wanaishi kama mke na mume, wakazi wa Kijiji cha Tanangozi, Wilaya ya Iringa Vijijini, wameuawa kinyama kwa kukatwakatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za miili yao.
Vikongwe hao, Abdallah Ngíngo, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka zaidi ya 90 na mkewe, Maria Semagoyo, anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 85, waliuawa usiku wa kuamkia juzi wakiwa ndani ya nyumba yao.
Habari zilizopatikana kutoka kwa mmoja wa majirani na vikongwe hao, Issa Nyalusi, zilisema kuwa marehemu Ng'ingo, alikuwa amepoteza uwezo wake wa kuona na inasadikiwa kuwa mauaji hayo yanahusishwa na imani za kishirikina.

Nyalusi, aliiambia NIPASHE kwa njia ya simu jana kutoka eneo la tukio kuwa kabla ya mauaji hayo, vikongwe hao walikuwa wakiishi na mjukuu wao wa kike anayesoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Tanangozi ambaye yeye hamfahamu kwa jina.
Alisema inadaiwa kuwa kabla ya mauaji hayo ya kutisha kutokea, mjukuu huyo aliwaandalia babu na bibi yake chakula cha mchana na walipokula yeye (mjukuu) jioni hakuhisi njaa na hivyo alikwenda kulala majira ya saa 1:00 jioni.
Nyalusi aliongeza kuwa akiwa mjukuu huyo amelala katika chumba chake kwenye nyumba hiyo yenye vyumba takriban sita, watu wasiojulikana, walimvamia bibi yake aliyekuwa ameketi sebuleni akijipumzisha na kumshambulia hadi kumuua.
Alisema baada ya wauaji hao kumuua ajuza huyo, walikwenda moja kwa moja katika chumba alichokuwa amelala mzee Ng'ingo, na kumuua pia kwa kutumia vitu vyenye ncha kali.
Nyalusi alifafanua kwamba mjukuu wao ndiye aliyekuwa wa kwanza kugundua mauaji hayo baada ya kuamka asubuhi na kukuta mlango wa sebuleni ukiwa wazi.
Alisema baada ya mjukuu huyo kuona mlango wa sebuleni uko wazi, alidhani kuwa bibi yake alikuwa ameamka na yuko na nyumba yao lakini alifika sebuleni aliukuta mwili wa bibi yake ukiwa umelala chini ya dimbwi la damu.
Nyalusi aliongeza kuwa mjukuu huyo alianza kupiga yowe lililowakusanya majirani ambao baada ya kufika pale sebuleni na kuingia chumbani, ndipo walipobaini kuwa hata mzee Ng'ingo, alikuwa ameuawa pia.
“Hakika ni mauaji ya kutisha ambayo hayaelezeki na nadra kutokea hapa kwetu kijijini,” alisema Nyalusi na kuongeza kuwa polisi walifika mapema na kuibeba miili ya vikongwe hao na kuipeleka katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa kwa hifadhi.
Alipoulizwa na NIPASHE kama wazee hao walikuwa na tabia za kishirikina, Nyalusi alijibu kuwa pengine hiyo inatokana na dhana potofu kwamba wazee ni wachawi.
“Ni dhana potofu tu kwamba kila wanayemuona amezeeka huhusishwa na ushirikina,” alisema.
Alisema vikongwe hao walizikwa jana jirani na makazi yao na kwamba mazishi yao yalihudhuriwa na umati mkubwa wa watu kutoka eneo hilo na vijiji vya jirani kutokana na kwamba mzee Ng'ingo alikuwa ni maarufu eneo hilo na ni mmoja wa wazee wa zamani walioheshimika mno kijijini Tanangozi.
Mmoja wa wajukuu wa marehemu hao, Bahati Msuya, pia alithibitisha tukio hilo la kinyama na kuliomba Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kuwakamata watu wote waliohusika.
“Jamani, siamini kama watu wanaweza kuwa na unyama wa kiasi hiki, bibi na babu yangu wameuawa kinyama sana ndugu yangu, maiti hazitamaniki,” alisema Msuya kwa simanzi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Claus Mwasyeba, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kueleza kuwa uchunguzi ulikuwa unaendelea kuwapata waliofanya kitendo hicho.
Alisema taarifa za awali ambazo polisi wamezisikia zilidai kuwa mauaji hayo yanahusishwa na imani za kishirikina.
Mkoa wa Iringa ni moja kati ya mikoa kadhaa nchini ambayo mauaji ya vikongwe kutokana na imani za kishirikina hutokea.
Mikoa mingine ambayo imekuwa na matukio makubwa ya mauaji ya vikongwe kutokana na imani za kishirikina ni Shinyanga hususan Wilaya ya Bariadi na Mwanza hasa katika wilaya za Misungwi na Magu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: