ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 14, 2011

Soma alama, ni aibu, mateso kulazimisha penzi lililokufa-GPL

Makala haya lengo lake kubwa ni kukutaka ujifikirie na kujitambua wewe ni nani. Baada ya hapo ni vyema kutambua kwamba, mwenzi wa maisha yako ana nafasi kubwa ya kuijenga au kuibomoa sifa yako.

Mathalan, kila siku wewe na mwenzako mnatibuana mpaka majirani na marafiki wanabaini tofauti zenu. Hapo usitegemee kuwa utasemwa kwa mazuri. Badala yake tegemea kuchekwa na kusemwa kwa lugha za kejeli na vijembe.


Huishi kwa ajili ya watu. Hilo linafahamika lakini tambua kuwa dunia si ya wewe na mwenzi wako peke yenu. Unapaswa kushirikiana na wengine katika kusukuma mbele gurudumu la maisha yako. Je, utashirikiana na watu wanaokuona hamnazo? La hasha!

Bila shaka unahitaji kusemwa vizuri. Hilo litawezekana kama mwandani wako ni mtu anayejiheshimu, anayekuheshimu na anayejipenda. Hayo yawepo, ila kubwa zaidi ni upendo wake kwako. Je unasomeka? Kama jibu ni ndiyo basi mshike, usimwachie.

Hata hivyo, upendo wake hauwezi kuwa na maana ikiwa wewe mwenyewe humwoneshi kwa vitendo jinsi gani moyo wako ulivyomwangukia. Bustani ukiipenda itakupa mazao mazuri, ukiichukia itakauka na hutaambulia kitu chochote.

Tatizo kubwa ambalo linawagharimu wengi ni kuwa, mapenzi yanabebwa kama aina ya mchezo wa kuigiza. Watu wanaingia kwenye uhusiano kwa kujaribu. Kuna waliofunga ndoa si kwa kuchaguana, isipokuwa walidanganyana kwa hisia za “mapozeo” mwisho wakazoeana, ikawa ngumu kuachana.

Wapo wanaoingia kwenye ndoa si kwa kuvutwa na nyoyo zao, ila wanakabiliwa na fikra za “waoaji wenyewe hawapo, acha nimkubali huyu huyu!”

Mapenzi ni nguzo maalum katika maisha ya binadamu, kwa hiyo ni vyema yabebe heshima inayostahili.

Ogopa sana mtu anayekuwa na wewe kwa sababu haoni chaguo lake. Adhabu yako ni kubwa mbele ya safari ingawa unaweza kujiona upo kwenye bwawa la asali mwanzoni. Kiama chako ni pale atakapomwona anayedhani ndiye sahihi kwake. Utasalitiwa upende usipende!

Dhana ya mapenzi duniani kote inaelekeza kuwa, asili yake ni moyoni. Hii ina mantiki kuwa, ndani ya kila mtu kuna vitu ambavyo anahitaji mwenzi wake awe navyo. Sura, umbo na tabia.

Hata hivyo, kuna nakshi nyingi ambazo si za lazima lakini huwavutia watu na kufunika hata yale ya msingi.
USHAURI: Zingatia sifa muhimu na kuachana na vionjo vya ziada (accessories).

Tambua kwamba nakshi za ziada haziwezi kumfanya mwenzi wako awe mzuri kiasi cha kukupa heshima ya kweli. Sifa muhimu ndizo ambazo unapaswa kufa nazo kwa lengo la kujiwekea mazingira ya kuheshimiwa na jamii yako kila siku.

Wiki iliyopita nilikupa mfano wa penzi la Ester na Sam. Kama ulisoma vizuri makala hayo, utakuwa na jibu lililonyooka kuwa baadaye Sam alijuta ni kwa nini alijitumbukiza kwenye penzi na Ester ingawa mwanzo alimpenda kwa dhati.

Kutokana na mfano wa jinsi Ester alivyoenda kufanya fujo kwa baba yake Sam, ni wazi utaona kuwa ni rahisi mtu kudharauliwa ikiwa utakuwa na mtu ambaye ni ‘waluwalu’ au asiye na mapenzi ya dhati kwako.

Atakusaliti, watu watazungumza pembeni. Atakusema vibaya, ukipita mitaani utaonekana kituko. Mpenzi mwenye uelewa na anayekupenda kwa dhati, atakulinda mahali popote.

Hatakusaliti, ataishi ndani yako. Linalokuuma, litamtesa. Wasiokupenda atawachukia. Marafiki zako atawageuza ndugu. Kinyume chake ni kwamba mwenzi asiyekupenda kwa dhati si ajabu akashiriki kukumaliza.

Pigania kuhifadhi moyo wako. Uweke katika himaya salama. Usijidanganye kwa penzi lisilo na uelekeo, lenye sura ya upande mmoja. Unampenda lakini yeye anakuchora, presha inapanda na kushuka mwenzako hana habari hata kidogo, tena ikiwezekana atakucheka kama katuni.

Usikubali hilo likutokee. Huna upungufu ambao huyo anayekudharau anadhani unao. Ikiwa anakuona wa nini, wengine wanaumiza kichwa watakupata lini. Kumkataa mwenzi mbaya ni mwanzo mzuri wa safari ya kumpata mtu sahihi kwako.

Tukutane wiki ijayo ili tuelekezane vizuri.

No comments: