Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema hoja ya kufuta posho za vikao kwa wabunge na watumishi wengine wa serikali ni hoja ya chama hicho na kwamba kwa kufanya hivyo fedha za walipakodi zaidi ya Sh. bilioni 900 zitaokolewa kwa mwaka.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha kambi ya upinzani.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, alisema mapendekezo hayo yatatolewa kama sehemu ya bajeti yao watakayoiwasilisha bungeni Jumatano ijayo.
“Hoja hii ichukuliwe kama hoja sensitive (muhimu), na isichukuliwe kama hoja ya kuleta migogoro miongoni mwa Zitto (Kabwe) na wabunge ama wabunge wa Chadema na wabunge wengine,” alisema Mbowe. Alisema wabunge na watumishi wengine wa serikali wamekuwa wakipata posho wakati wa vikao licha ya kwamba wamekuwa wakipata mshahara kila mwezi. Alitoa mfano wa mbunge ambapo amekuwa akipata posho ya kujikimu na vile vile akihudhuria bungeni anapewa posho wakati hiyo ni kazi ya mbunge.
“Mbunge analipwa per diem (posho ya kujikimu) akija bungeni analipwa posho ya kikao hata kama amekaa bila kuongea…huu ni ugonjwa ambao umesambaa nchi nzima,” alisema Mbowe.
Alisema kuwepo kwa posho za vikao kumewafanya watumishi wengi wa umma kukosekana ofisini na hivyo kushindwa kuwahudumia wananchi kwa wakati.
Kuhusu uamuzi wa Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, kuandika barua kwa Katibu wa Bunge kuomba posho yake ya vikao ipelekwe katika mfuko wa Maendeleo wa Jimbo, Mbowe alisema Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini, alifanya hivyo kutokana na tafsiri potofu juu ya jambo hilo.
“Kupokea kwangu posho ama Zitto bado hakuzuii mimi kutolizungumzia tatizo hilo,” alisema.
Akizungumzia kuhusiana na suala hilo, Naibu Spika, Job Ndugai, alisema kuwa hawawezi kulizungumzia jambo hilo hadi hapo kambi hiyo itakapowasilisha bungeni.
MKULO ATANGAZA NYONGEZA YA MISHAHARA
Wakati huo huo, serikali imesema bajeti ya mwaka 2011/2012, imetenga fedha kwa ajili ya nyongeza ya mishahara ya watumishi wa umma kwa kuzingatia majadiliano kati yake na vyama vya wafanyakazi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, alisema kuwa kiasi kilichoongezwa kitatajwa na Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa umma bungeni wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake. “Sina dhamana ya kutangaza kiasi kilichongezwa, atatangaza bungeni waziri anayehusika(Waziri wa Nchini, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, atakapowasilisha bajeti yake,” alisema Mkulo.
AMJIBU ZITTO KABWE
Aidha, Mkulo alisema kuwa kauli ioliyotolewa na Zitto Kabwe, kuwa bajeti iliyowasilishwa ni bajeti ya kulipa madeni haina ukweli.
Alisema kuwa bajeti ya mwaka 2010/2011 ilitenga Sh. trilioni 1.8 kwa ajili ya kulipa madeni na bajeti ya mwaka huu ilitenga trilioni 1.9 kwa ajili ya kulipa madeni. Alisema kuwa mwaka 2010/2011 ilitenga Sh. trilioni 11.6 na mwaka huu trilioni 13.525 na kwamba anashangazwa na kambi ya upinzani kusema kuwa bajeti hiyo ni hewa na kwamba hakuna kilichoongezeka.
Kuhusu faini za magari, alisema kuwa awali walipanga ongezeko la faini kwa watenda makosa ya barabarani iliyoandikwa katika kitabu chake ni Sh. 300,000, lakini walipata maoni kutoka kwa wadau kuwa ingechochea kwa kiasi kikubwa suala la rushwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment