ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 20, 2011

Ndoa inamfuata anayefaa, inamkwepa asiyefaa, jiangalie – 3-GPL

Sipingani na ukweli kwamba ndoa hupangwa na Mungu lakini bado kuna mantiki kuwa nidhamu na jitihada binafsi zina nafasi kubwa katika kufanikisha suala zima.

Barabarani unaitwa paka mapepe. Hujawahi kuwa na utulivu wa angalau dakika 30 na watu wakaaamini. Palipo na ngoma ndipo unapoweka kambi. Una hulka ya ugomvi. Unadhani nani anataka matatizo kwenye ndoa?


Daima watakuona kama mtu wa maonesho na mifano. Wakitaka kuzungumzia mtu ambaye ni ngumu kuolewa watakutaja wewe. Na kama ni mwanamume, ndivyo hivyo utakavyoelezewa.

Kuna watu wameweza kufunga ndoa kwa urahisi lakini baada ya muda mfupi wakazivunja kwa sababu ya hulka zao. Hata hivyo, asilimia kubwa ambao ndiyo kundi ninalolilenga ni lile ambalo wanatibua katika mitindo yao ya maisha.

Nimegusia hapo juu. Tayari nimeshachambua makundi matatu ambayo sitayarejea kutokana na nafasi. Unaweza kutazama matoleo yaliyopita kama unaweza kuyapata.

Kuna kundi la watu wanaoamini fedha zao kuliko chochote. Kwamba mambo yakiwa sawa mfukoni hata masuala ya uhusiano hayatakuwa na migogoro. Wanakosea sana kama siyo kupoteza muda wao.

Kwa mwanamke ambaye atakuwa anaamini katika fedha zake ndiyo mtihani mkubwa. Anaweza kujenga kiburi kwa hisia kuwa anaweza kumnunua mwanamume yeyote. Watu wa aina hiyo wamefeli.

Tupo kwenye jamii moja, tunawaona wanawake wengi ambao wamekosa mapenzi ya dhati, kutokana na fedha zao, wanakuwa watu wa kubeba vijana wadogo. Wanakosa heshima, wanaanza kuitwa mashugamami.

Heshima ipi kwako watu kukwita shugamami? Kwamba vijana wadogo wanakutumia kwa sababu ya fedha zako, baadaye wanakuacha. Wanaambiana, eti wewe ni ATM kwa ajili ya matumizi madogo madogo.

Je, hiyo ni sawa? Vijana ambao hawana mapenzi ya dhati wakutumie wewe mama ambaye umri wako umekwenda. Fedha zako zinakutesa. Hupati penzi la kweli, isipokuwa unatazamwa kama mti wa kuchumia fedha.

Kijana anachukua fedha kwako anakwenda kumhonga mwanamke mwingine anayempenda. Usiku unalala na mawazo, eti kijana unamhudumia mwenyewe lakini anakusaliti. Unaingiwa na mawazo mabaya.

Pengine kuna mwanamume wa umri wako anakupenda kwa dhati na anatamani kuwa na wewe katika maisha ya ndoa lakini anaghairi baada ya kuona uhusiano wako na vijana wadogo. Awe na wewe, atatokaje na skendo zote hizo.

Ndoa humfuata anayefaa kwa maana endapo ungekuwa unajiheshimu, umetulia. Fedha zako hazikutawali. Una heshima kamili, ungempata mwanamume wa kweli katika moyo wako na kuepukana na aibu ya kuitwa shugamami.

KUNDI LA NNE
Ni tabaka la watu wachafu. Mwanamume akiwa mchafu ni ndoto kumpata mwanamke sahihi. Mapenzi yana maana pana, yanabeba maana ya maonesho, kwamba mtu ajisikie kuonekana na mwenzi wake.

Wewe ni mchafu, kwa hiyo mwanamke anaona hufai hata kutambulishwa kwa marafiki zake achilia mbali kwa wazazi wake. Muonekano wako haukubaliki, mavazi yako yanabadilika rangi kwa uchafu.

Atajishauri kuwa na wewe lakini jibu la mwisho kwake itakuwa kwamba endapo atakukubali, basi na heshima yake itashuka. Kwa maana, anaona marafiki zake wanavyojiachia na wapenzi wao wasafi na wanaotazamika.

Kwa mwanamke mchafu ndiyo msiba kabisa. Wanaume watamuona na kujisikia kinyaa. Itakuwa vipi kutoka nao ‘out’? Jibu hapo ni kuwa haiwezekani. Wanaume wanahitaji wanawake bora na siyo bora wanawake.

Ukijiweka katika hali ya usafi, utapendwa. Wakati mwingine hata aina ya utembeaji ni jambo ambalo linaweza kuwafanya wanaume kukutafsiri kwa thamani. Ukitembea kama bata, hata kama ni msafi watakuona wa bei nafuu. Tembea vizuri ili upewe sifa.

KUNDI LA TANO
Linagusa watu wenye skendo za mapenzi. Sifa kuwa leo upo na huyu kesho unatoka na yule ni mbaya na imewagharimu wengi.
Hata kama unateleza, hebu fanya kwa siri. Siyo kila unayempata unamuonesha waziwazi, baadaye mnaachana, mwisho inaonekana umeshatembea na kundi kundi kubwa.

HITIMISHO
Kwa kumaliza ni kwamba tabia njema ni pointi ya msingi katika kuisogeza ndoa karibu. Jiangalie, naamini utapata majibu na kuchukua hatua inayofaa.

No comments: