ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 13, 2011

Watu 3 wafa Dar es Salaam, ofisi za Azam zanusurika

WATU watatu wamepoteza maisha jijini Dar es Salaam akiwemo Mohammed Issa (41), ambaye alikufa kwa kuteketea kwa moto baada ya nyumba aliyokuwa akiishi kuwaka moto wakati akiwa amelala. 

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema, moto huo ulizuka leo maeneo ya Manzese Sisi kwa Sisi katika nyumba yenye vyumba sita inayomilikiwa na Mohamed Hassan (43), mkazi wa Manzese. 

Katika tukio lingine, mtoto Charles Moses (5), amekufa baada ya kuangukiwa na ukuta huko Kimara Matosa wilaya ya Kinondoni. 


Kenyela alisema, tukio hilo lilitokea jana ambapo mtoto huyo alipata majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake na kufa akiwa njiani kupelekwa katika hospitali ya Tumbi Kibaha. 

Katika tukio la tatu, mwanamume asiyefahamika jina lake anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 amekutwa akiwa amekufa katika kituo cha mabasi Ubungo huku akitokwa na damu puani. 

Kamanda Kenyela alisema, sababu za kifo hicho bado hazijafahamika na marehemu alipopekuliwa alikutwa na tiketi za basi la Wifi Nae Video Coach lenye namba T 112 AEK ikiwa imeandikwa jina la Abdallah Hassan ya kutoka Masasi kuja Dar es salaam. 

Amesema tiketi hiyo ilionyesha imetolewa Juni 7 na kisha kupanda gari Juni 9 na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi zaidi. 

Wakati huohuo ofisi za kampuni ya meli ya Azam Marine zilizopo eneo ya Bandarini, wilaya ya Ilala, zimenusurika kuteketea kwa moto, baada ya kutokea hitilafu ya umeme. 

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, moto huo ulizuka jana saa 5.00 usiku katika ofisi hizo eneo la kuoshea vyombo vya chakula. 

Amesema, moto huo uliteketeza vyombo mbalimbali vikiwemo vikombe, mabeseni na plastiki na ndoo za plastiki. 

Shilogile amesema, uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme ambapo taa ililipuka na kudondoka na hatimae kusababisha moto huo.


CHANZO:HABARI LEO

No comments: