ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 24, 2011

Waziri Bernard Membe: Tutasusia chenji ya rada

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
Serikali imewasilisha taarifa bungeni dhidi ya uamuzi wa kampuni ya kutengeneza zana za kivita ya BAE Systems ya nchini Uingereza wa kutaka kutoa jumla ya Paundi milioni 29.5 (Sh. bilioni 75) kwa wananchi wa Tanzania kupitia asasi za kiraia, badala ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku wabunge wa upinzani wakitaka ijadiliwe na Bunge.

 Uamuzi huo umefikiwa na kampuni hiyo, baada ya Mahakama ya Westminster ya Uingereza, kuiamuru kuirejeshea Tanzania fedha hizo zikiwa ni tozo ya fidia ya mauzo ya rada iliyoilangua Serikali ya Tanzania kwa kuiuzia kwa dola za Marekani milioni 40, mwaka 2002, kinyume cha bei yake halisi. 
Kampuni hiyo iliamriwa kufanya hivyo Novemba 23, mwaka jana, baada ya kukiri mahakamani hapo kwamba, ilifanya makosa kwa kutoweka kumbukumbu za fedha na mahesabu katika mchakato wa mauzo ya rada kwa Serikali ya Tanzania. 
Fedha hizo zinajumuisha gharama za kesi hiyo iliyofunguliwa mahakamani hapo na Shirika la Uchunguzi wa Makosa Makubwa (SFO) la Uingereza.
 Kauli ya serikali dhidi ya wanunuzi wa BAE ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, bungeni mjini hapa jana.
 Waziri Membe alisema serikali inashangazwa na uamuzi huo wa BAE Systems kwa vile fedha hizo, si misaada kama kampuni hiyo inavyotaka kuuaminisha ulimwengu.
 “Fedha hizi ni tozo kwa hela zilizokwapuliwa na kampuni ya BAE kutoka Serikali ya Tanzania,” alisema Waziri Membe.
 Alisema serikali pia inashangaa kwa vile uamuzi huo unapishana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Uingereza na una lengo la makusudi la kuonyesha sura ya kutoiamini dhamira ya Serikali ya Tanzania kutumia fedha hizo kwa kusudi lililotolewa. 
“Kwa uamuzi huu, BAE inataka umma wa Uingereza uamini kuwa asasi za kiraia zitatumia fedha hizo kwa umakini zaidi kuliko Serikali ya Tanzania,” alisema Waziri Membe.
 Alisema SFO, Serikali ya Uingereza na Serikali ya Tanzania zilijadiliana na kukubaliana kuwa fedha hizo za wananchi wa Tanzania zirejeshwe kupitia Serikali ya Tanzania na kwamba, serikali hizo mbili (ya Uingereza na Tanzania), zilikubaliana kuwa fedha hizo zitumike kwenye sekta ya elimu.
Alisema katika mpango huo, serikali ilidhamiria kutumia fedha hizo kununua vitabu milioni 4.4 kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi nchini na pia kununua vitabu 192,000 vya kufundishia kwa ajili ya walimu wa shule za msingi.
 Waziri Membe alisema baada ya uamuzi huo wa mahakama kutolewa, BAE Systems haikuchukua hatua yoyote ya kuzirejesha fedha hizo Tanzania.
 Badala yake, alisema Mei 15, mwaka huu, BAE Systems ilieleza nia yake ya kuzirudisha kupitia asasi za kiraia za Uingereza na sio kwa Serikali ya Tanzania kwa kigezo kwamba, sera ya kampuni hiyo zinaruhusu kutoa misaada kwa asasi za kiraia pekee.
 Alisema serikali ilipinga uamuzi huo kwa vile ni wa kuidhalilisha serikali, asasi za kiraia zilizoko nchini na wananchi kwa jumla. 
“Ni uamuzi unaoiondolea heshima nchi yetu. Fedha milioni 29.5 ni za walipakodi wa Tanzania na hazina budi kurejeshwa kwao kupitia serikali yao,” alisema Waziri Membe. 
 “Alisisitiza kuwa katika miaka yote fedha za maendeleo kutoka Serikali ya Uingereza zimekuwa zikitolewa kwa wananchi wa Tanzania kupitia Serikali ya Tanzania na wamekuwa wakiridhika na jinsi zinavyotumika,” alisema Waziri Membe akimnukuu waziri huyo wa Serikali ya Uingereza. 
Waziri Membe alisema serikali, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limetuma timu ya wabunge nchini Uingereza kukutana na kamati husika na kufanya mazungumzo na wabunge wa Bunge la Uingereza.
 “Kampuni ya BAE ina masikio lakini haitaki kusikia kilio cha wengi. Imeonyesha dharau ya wazi wazi dhidi ya serikali yetu na watu wake,” alisema Waziri Membe.
  Waziri Membe alisema serikali imetahadharisha kwamba, haitaruhusu asasi yoyote ya kiraia ya Uingereza itakayonufaika na fedha hizo kuja kuendesha shughuli zake nchini akisema Tanzania ni nchi maskini, lakini haiko tayari kudharauliwa kiasi hicho, kwa serikali yake, taasisi zake na asasi zake kutoaminiwa.
Aliwataka wabunge bila kujali itikadi zao za kisiasa pamoja na wananchi wengine wazalendo kuungana pamoja katika hilo ili kulinda heshima ya nchi.
Baada ya Membe kuwasilisha taarifa hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, alisimama na kutoa hoja akitaka taarifa hiyo ya serikali ijadiliwe na Bunge, hoja ambayo iliungwa mkono na wabunge wa upinzani, ambao walisimama kuashiria kuiunga mkono. 
Kutokana na hilo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliahidi kuwa atatoa muda wa kujadiliwa taarifa hiyo ya serikali.
CHANZO: NIPASHE


No comments: