ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 12, 2011

JK AWAACHIA HURU POLISI WALIOMUUA JENERALI KOMBE

WALIHUKUMIWA KUNYONGWA NA MAHAKAMA KUU, RUFAA
ASKARI Polisi wawili waliokuwa wamehukumiwa adhabu ya kifo mwaka 1998 baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa makusudi Mkurugenzi wa zamani wa Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe wameachiwa huru.Koplo Juma Mswa na Konstebo Mataba Matiku, ambao wamekuwa gerezani takriban kwa miaka 16, wamechiwa huru kwa huruma ya Rais Jakaya Kikwete ambaye alipunguza adhabu hiyo ya kifo, kuwa kifungo cha miaka miwili jela.


Kombe aliuawa kwa kupigwa risasi nne kifuani Juni 30, 1996 baada ya polisi waliokuwa wakisaka gari aina ya Nissan Patrol mali ya W. Ladwa, kumfananisha na mtuhumiwa sugu wa wizi wa magari.

Akizungumza na Mwananchi jana, Matiku alisema walitoka gerezani Mei mwaka huu walikokuwa wakisubiri kutekelezwa kwa adhabu yao ya kunyongwa, kabla ya Rais Kikwete kuwaonea huruma na kuwapunguzia adhabu.

“Unajua baada ya jaji kutuhukumu kunyongwa tulikata rufaa, Mahakama ya Rufani ambayo iliona ile hukumu ilikuwa ni sahihi ikasema tuendelee nayo hadi tulipoomba huruma ya Mheshimiwa Rais,” alisema Matiku na kuongeza:

“Jopo lililomshauri Rais lilipendekeza tupunguziwe adhabu kutoka kunyongwa hadi kifungo cha miaka miwili na kwa kuwa tulikuwa mahabusu tangu 1998, kifungo hicho kilitosha.”

Alipoulizwa wanachofanya sasa yeye na mwenzake Mswa, Matiku alisema anajishughulisha na shughuli za kilimo wakati mwenzake anajishughulisha na biashara.

Maisha gerezani
Konstebo Matiku aliliambia alisema katika miaka yote 16 aliyokuwa gerezani (1996 – 2011), aliishi katika magereza matatu tofauti, Karanga, Kilimanjaro; Maweni, Tanga na Ukonga, Dar es Salaam.

“Kwanza tulikaa Karanga kwa miaka miwili hadi tulipohukumiwa na Mahakama Kuu mwaka 1998, tukahamishiwa Gereza la Maweni kwenda kusubiri kunyongwa, lakini mwaka 1999 mimi nilianza kuumwa hivyo nikahamishiwa Ukonga ili niweze kupata matibabu,” alisema Matiku.Alisema kuanzia wakati huo alitengana na mwenzake, Mswa hadi walipoachiwa kwa huruma ya Rais Mei mwaka huu.

Alisema katika kesi hiyo walikuwa washtakiwa sita wakiwamo askari polisi watano na raia mmoja. Alidai kwamba raia huyo aliyekuwa akiitwa Ismail Katembo alifariki dunia akiwa gerezani mwaka 1997, huku askari wengine wakiachiwa huru na Mahakama Kuu baada ya kutopatikana na hatia.

Matiku alisema katika kesi hiyo walikuwa wakitetewa na mawakili watatu tofauti na kwamba wakili wake anamkumbuka kwa jina moja tu la Sande... “Alikuwa akiitwa Sande, lakini kwa bahati mbaya mimi sina mawasiliano naye hadi sasa, wale wengine walioachiwa walikuwa wakitetewa na Profesa Msenga na huyu Mswa alikuwa akitetewa na wakili mmoja hivi ni profesa naye lakini jina lake limenitoka.”

Matakwa ya Katiba
Madaraka ya Rais ya kumsamehe mtu yeyote aliyepatikana na hatia, yamo katika Ibara ya 15 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2005.

Ibara hiyo inatamka “Bila kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Ibara hii, Rais anaweza kutenda lolote ikiwamo kuibadilisha adhabu yeyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote ili iwe adhabu tahafifu.”

Kisheria, huruma hiyo ya Rais inatambulika kama 'Presidential Amnesty' wakati madaraka hayo ya Rais yakifahamika kama 'Prerogative Mercy' na hata Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliwahi kuitumia wakati wa utawala wake.

Madai ya familia
Baada ya polisi hao kupatikana na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa kile Jaji Buxton Chipeta alichosema: “Uzembe wa hali ya juu”, mjane wa Kombe, Roselyne Kombe alifungua kesi ya madai dhidi ya Serikali.

Mjane huyo na watoto wa marehemu, walifungua kesi Mahakama Kuu wakiidai Serikali fidia ya Sh690 milioni kwa msingi kuwa kifo cha Kombe kiliifanya miradi iliyoanzishwa na marehemu kupoteza mwelekeo na kufa.

Oktoba 4, 2001, Jaji Lawrence Mchome ambaye sasa amestaafu, aliiona Serikali kuwa inawajibika kuilipa familia hiyo fidia kutokana na vitendo vya watumishi wake hao wawili lakini ikaiamuru ilipe fidia ya Sh300 milioni.

Hata hivyo, Serikali haikuridhika na hukumu hiyo na ilikata rufaa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ambayo kimsingi nayo iliafiki Serikali kulipa fidia isipokuwa ilipunguza kiwango cha fidia hadi kufikia Sh200 milioni.

Adhabu ya kifo
Hatua ya Rais kuwapunguzia adhabu polisi hao imekuja katika kipindi ambacho wanaharakati wa haki za binadamu wakipaza sauti kutaka adhabu ya kifo ifutwe na badala yake iwe kifungo cha maisha.
 
Tangu Rais Kikwete aingie madarakani 2005, hajawahi kusaini hukumu yoyote ya kifo kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, Benjamin Mkapa na hadi sasa zaidi ya watu 500 wanasubiri kunyongwa.

Kwa mujibu wa hotuba ya aliyekuwa msemaji wa kambi ya upinzani bungeni, Fatma Maghimbi (CUF), mwaka 2008, Mkapa alibadilisha hukumu za watu 100 waliohukumiwa kunyongwa na kupewa adhabu mbadala.

Maghimbi ambaye sasa ni mwanachama wa CCM, alisema Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ndiye pekee aliyesaini utekelezwaji wa hukumu ya kifo kwa watu 21 ambao walinyongwa mwaka 1994.

Adhabu ya kifo ni kati ya zile sheria 40 ambazo Tume ya Marekebisho ya Sheria chini ya, hayati Jaji Francis Nyalali ilipendekeza zifutwe, kwa kuwa haimsaidii aliyeua, aliyeuliwa wala Serikali kuzuia kosa kama hilo kutokea.

Mwananchi

No comments: