Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu |
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu, amesema hayumo katika makundi ya vigogo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotajwa kupenda kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Amewataja vigogo wanaotajwa kuwania kiti hicho katika uchaguzi huo, ambao anahusishwa kuwamo katika makundi yao kuwa ni pamoja na Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Nyalandu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
Aliitisha mkutano huo kwa lengo la kueleza msimamo wake kuhusu madai ambayo yamekuwa yakitolewa dhidi yake kupitia vyombo vya habari (hakuvitaja) kwamba, ama ana mpango wa kugombea urais au yumo chini ya moja makundi ya wanaotajwa kuwa na nia ya kugombea kiti hicho.
Pia kueleza msimamo wake kuhusu vijembe ambavyo alidai amekuwa akirushiwa kwamba, si raia wa Tanzania.
“Naomba niseme wazi kwamba kwa namna yoyote na jinsi yoyote ile, mimi sio mgombea wa urais wa Tanzania. Mimi siko chini ya kundi lolote lile la yeyote anayesema ama anayependa kugombea urais wa Tanzania,” alisema Nyalandu ambaye mbali na nafasi ya kisiasa ya ubunge na unaibu waziri nyingine aliyonayo ni ujumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Singida.
Alisema kimsingi, yeye amejikita na ataendelea kumtumikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wadhifa anaomteua.
Hivyo, akasema kamwe katika kutekeleza wajibu wake wa kikatiba ndani ya Bunge, jimboni na kokote nchini, asitokee mtu kudhani kuwa anafanya hivyo kwa nia ya kugombea urais ama kusaidia kundi lolote dhidi ya kundi lingine.
Alisema baadhi ya viongozi kujikita katika kutafuta urais wa 2015 na wafuasi wao kuendelea mapambano ya wazi dhidi ya wale wasiokubali kuwa ndani ya kundi husika inasikitisha na ina lengo la kukatisha tamaa viongozi wote wenye lengo la kufanya kazi walizopewa kwa bidii na moyo wao wote.
Alisema Rais Kikwete ana miaka minne ya kuwa madarakani hivyo hakuna sababu wala tija kwa mtu ama kundi lolote kufikiria urais wa 2015, bali jambo la busara kwa viongozi wote ni kufanya kazi kwa moyo na kwa uadilifu.
Alisema amekuwa akihusishwa na makundi mengi ya wanaotajwa kuwania urais katika uchaguzi, hasa la Lowassa, Membe na Sitta.
Hata hivyo, alisema anahusishwa na vigogo hao kutokana na uhusiano wa karibu alionao na kwamba kila mmoja ni rafiki yake kwa namna tofauti, na kumtaja Membe na Sitta kuwa ni marafiki zake wa kawaida.
ANAVYOHUSISHWA NA LOWASSA
Akielezea namna anavyohusishwa na kundi la Lowassa, Nyalandu alisema: “Kuna kipindi nilitembelea Monduli. Na Mheshimiwa Edward Lowassa akiwa Waziri Mkuu, kama kuna kazi, ambazo nimefanya mimi na yeye, ilikuwa kujenga mashule Singida. Na tulijenga shule kwa muda mfupi zikawa nyingi. Tulifanya kazi ngumu.”
“Kwa hiyo, ninamheshimu, ninamheshimu sana (Lowassa) na ni mara nyingi niseme tukiwa Dodoma nakunywa naye chai. Mi naendaga nyumbani kwake. Na kuna kipindi nimeshawahi kuambiwa na baadhi ya watu tulionekana Monduli, kwa hiyo, moja kwa moja uko kwenye hilo kundi la mzee wa Monduli. Nilicheka sana.”
WAZIRI MEMBE JE?
Kuhusu Waziri Membe, alisema: “Sasa turudi kwa marafiki zangu wanaojulikana wa kawaida, Bernard Membe. Ni rafiki yangu mzuri sana. Tumeanza naye Bunge mwaka 2000. Unajua siamini kwamba mwaka 2000 ni karibu miaka 12 iliyopita. Maana yake ni kama jana tu. Tukiwa 'ma-back bencher', Kamati ya Mambo ya Nje wote. Sisi ni marafiki, yaani ni marafiki. Kwanza nyumbani tunakaa jirani.”
“Jioni lazima tuzungumze. Kwa simu lazima tuongee. Nikitaka 'kubipu' ugali nyumbani kwake sipigi hodi. Ni marafiki wa kiasi hicho. Kwa hiyo, mtu anayejisikia kunihusisha na lile kundi kama lipo, of course wamesema sana.”
KUHUSU WAZIRI SITTA
“Haya! Lingine ni kundi la mzee Sitta. Huyu ni mentor (mwalimu). Ni mtu, ambaye kwanza ananishauri vitu vingi. Ni rafiki yangu hata kama akinisikia. Sidhani kama kuna siku itapita sijaenda kumuona mzee Sitta. Kama hatujaonana kesho yake tutaonana, tutazungumza, tunaenda kwenye maeneo mengi pamoja, jambo lipo tunashauriana,” alisema Nyalandu.
Aliongeza: “Sasa nasema dhana ya kuhusishana na kundi ndiyo inayomaliza nchi kwa sababu watu wanasema wewe okay tumegundua Nyalandu wewe siyo wa kundi letu. Hao hao wanaanza kukubonda.”
VIJEMBE KUWA SI RAIA
Kuhusu vijembe, ambavyo amekuwa akirushiwa kwamba, yeye si raia wa Tanzania, Nyalandu alisema madai hayo ni ya uongo.
“Uongo ni dhambi mbele za Mungu. Wahenga walisema, akutukanaye hakuchagulii tusi. Naomba turejeshe upendo, mshikamano na utaifa. Tufanye kazi kwa pamoja kuikomboa nchi yetu dhidi ya changamoto tulizonazo.”
Alisema yeye ni mzaliwa wa mkoa wa Singida anayetokana na kabila la Wanyaturu na kwamba wazazi wake wote wako hai na anayetaka kupata ukweli kuhusu uraia wake anaweza kuwatafuta na kuwauliza.
Pia alisema anaamini serikali ina vyombo vya uhakika vinavyoweza kuthibitisha kama yeye ni raia wa Tanzania au la.
Hata hivyo, Nyalandu alisema kamwe hawezi kwenda mahakamani kuvishtaki vyombo vya habari vilivyotangaza habari hizo kwa vile siku zote amekuwa akiamini katika uhuru wa vyombo vya habari.
“Mimi ni mtu ninayeamini katika uhuru wa vyombo vya habari, hiyo ni imani yangu. Na gazeti linapoandika habari, nyinyi kama gazeti au wahariri mnakuwa na vyanzo mbalimbali sana vya kupata habari na isiwe moja kwa moja kwamba nikasema kwa sababu uliandika Nyalandu siyo raia au kitu gani nikimbilie mahakamani, wala sitaenda,” alisema Nyalandu.
Aliwashauri wanahabari kuzingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari kwa kuandika habari sahihi, ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi kwa pande zote zinazohusika na jambo linalohusu tuhuma.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment