Thursday, February 23, 2012

Slaa aibuka mahakamani, aongezewa mashitaka

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa (kulia) na mchumba wake, Josephine Mushumbuzi

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mkewe, Josephine, jana walijisalimisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, kutii amri ya Hakimu Mkazi, Charles Magesa, ya kujisalimisha katika kipindi cha saa 24, vinginevyo wangekamatwa kwa nguvu.

Dk. Slaa na mwenzi wake walipewa amri hiyo juzi baada ya kushindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi inayowakabili pamoja na viongozi na wanachama wengine wa Chadema wanaoshtakiwa kwa kuandamana Januari 5, mwaka jana na kukataa kutii amri ya polisi mjini Arusha.
Juzi Hakimu Magesa alionya kuwa kama Dk. Slaa na Josephine wasingefika mahakamani hapo jana, angetoa hati ya kuwakamata.
Mshtakiwa mwingine ambaye alionywa na Hakimu Magesa kwa kutofika mahakamani hapo juzi ni mfuasi wa Chadema, Aquline Chuwa.
Wakili Albert Msando, akiwatetea Dk. Slaa na wenzake kwa kutofika mahakamani, alidai kuwa walichanganya tarehe ya usikilizwaji wa kesi hiyo.
Wakili wa Serikali, Edwin Kakolaki, juzi aliiomba mahakama hiyo kutoa hati ya kuwakamata washtakiwa hao na kuwafikisha mahakamani kwa nguvu kwa kosa la kuidharau.
“Hawa washtakiwa si kweli kama anavyodai wakili wao (Msando) kuwa wamechanganya tarehe ya kesi kutokana na wingi wa kesi walizonazo na kwa kuwa wana wadhamini wao, wangepaswa kufanya nao mawasiliano pamoja na wakili wao, hivyo naiomba mahakama itoe hati ya kuwakamata na kuwaleta hapa kwa nguvu ili wasipate mkanganyiko wa kuchangaya tarehe,” alidai.
Baada ya maombi ya ya Wakili Kakolaki, Hakimu Magesa alitoa amri ya kuwataka Dk. Slaa na wenzake kuhakikisha wanakuwepo mahakamani jana, vinginevyo angelazimika kutoa hati ya kuwakamata.
Jana baada ya kufika mahakamani, Dk. Slaa, Josephine na Chuwa walisomewa mashitaka kama waliyosomewa wenzao 16 juzi, lakini waliyakana.
Dk. Slaa, Josephine na Chuwa pamoja na washtakiwa wengine, awali walikuwa wakikabiliwa na mashtaka manane, lakini juzi waliongezewa mashtaka hadi kufikia 13, wakidaiwa pamoja na mambo mengine kufanya kusanyiko bila kibali, kukataa amri halali ya polisi na hivyo kusababisha vurugu Januari 5, mwaka jana.
Katika hatua nyingine, mahakama hiyo jana iliiahirisha kesi hiyo ambayo pia inamkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe hadi kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, itakapomalizika katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Hakimu Magesa, alisema amechukua uamuzi huo kufuatia ombi lililotolewa na wakili wa utetezi, Method Kimomogoro, aliyetaka iahirishwe ili kutoa nafasi kwa Lema kusikiliza kesi yake ya uchaguzi iliyopo Mahakama Kuu.
Kimomogoro pia alidai kuwa, kifungu namba 196 hadi 197 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), vinatoa haki ya mshtakiwa kuwepo mahakamani wakati kesi yake inaposikilizwa.
“Lema ana haki na wajibu kuwepo mahakamani hapa kusikiliza shauri lake, sasa kwa kuwa kuna kesi nyingine Mahakama Kuu, naiomba mahakama yako iahirishe shauri hili ili kutoa nafasi kwa mteja wangu kusikiliza shauri lake muhimu Mahakama Kuu,” alidai.
Akitoa sababu nyingine ya kutaka kuahirishwa kwa kesi hiyo, Kimomogoro alidai kuwa pamoja na kusimamia kesi hiyo, pia ni wakili wa Lema katika kesi yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi.
Alidai kuwa Mahakama Kuu ilipoahirisha kesi ya Lema wiki iliyopita, Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Gabriel Rwakibarila, alimuagiza kufanya maandalizi ya kutoa ushahdi wao mara baada ya walalamikaji kumaliza kutoa ushahidi wao, hivyo aliomba muda wa kufanya kazi hiyo.
Pamoja na ombi hilo, Kimomogoro pia aliiomba mahakama iwaamuru upande wa Serikali uwapatie majina ya mashahidi 75 pamoja na maelezo yao ambayo yamekusanywa kwa lengo la kuyatumia kwenye ushahidi wa kesi hiyo.
Kimomogoro alidai upande wa mashtaka tayari umewapatia maelezo kama yalivyoandikwa na mpelelezi wao kuhusu mtu aliyewapa taarifa za matukio ya Januari 5, mwaka jana, na sio maelezo ya mashahidi kama walivyohojiwa na upande wa upelelezi.
Wakili wa Serikali, Edwin Kakolaki, akijibu hoja hizo, alidai kuwa hawawezi kutoa majina ya mashahidi wao, na pia hawawezi kuwapa hati ya maelezo ya mashahidi wao kwa kuwa sheria haiwataki kufanya hivyo.
Alidai kuwa hawawezi kuwapa maelezo hayo kwa sababu sheria inawapa uhuru wa ama kuwapa au kutowapa.
Kuhusu ombi la kuahirisha kesi, Wakili Kakolaki alipinga ombi hilo na kuiomba mahakama kuendelea na kesi kwa hatua ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka.
Alidai kwa kuwa washtakiwa wana mawakili wawili, basi inatosha kuwakilishwa na wakili mmoja, Albert Msando, wakati Kimomogoro atakapokuwa kwenye kesi ya Lema.
Hata hivyo, mabishano hayo yaliendelea na Hakimu Magesa akaahirisha kesi hiyo kwa muda wa robo saa na baada ya muda huo, alisema: “Ombi la kupewa maelezo ni kwamba wanachopewa ni yale maelezo ya awali, lakini maelezo ya ushahidi uamuzi upo upande wa mashtaka kama wanataka kuwapa au wasiwape.”
Akitoa uamuzi wa kuahirisha kesi, Magesa, alisema ameuchukua baada ya kuona kwamba kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi inayomkabili Lema inasikilizwa na mahakama kubwa kuliko hiyo, na kutokana na sababu hiyo usikilizaji wa kesi hiyo utategemea kumalizika kwa kesi iliyopo Mahakama Kuu.
“Mahakama inayosikiliza kesi ya uchaguzi ni kubwa kuliko hii, basi mahakama hii inaahirisha kesi hii hadi kesi ya uchaguzi itakapomalizika …tujipe mwezi mmoja kuona kama kesi hiyo itakuwa imemalizika au la, kama itakuwa imemalizika, basi tutaendelea na kesi yetu kwa hatua ya usikilizaji na kama itakuwa bado basi tutaiahirisha,” alisema hakimu Magesa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake