ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 13, 2012

JE, NI KWELI WANAWAKE HAWAJITAMBUI KWENYE MAPENZI? TUJADILI - 2

 
TUKIANZIA kutoka pale tulipomalizia wiki iliyopita ni hivi; hata jamii ya wasamaria, alipatikana mmoja aliye mwema ndiyo maana akaitwa msamaria mwema. Hivyo basi, wasisemwe vibaya wanawake wote kwa ajili ya makosa ya wachache.
Hata hivyo, hao wachache wanapaswa kubadilika ili wawape heshima wenzao. Tamaa haifai kwa namna yoyote. Binafsi nawaheshimu wanawake kwa maana ndiyo waliotufanya tustarehe kwenye matumbo yao kwa miezi tisa, wanawezesha tuitwe akina baba na kadhalika. 

Mambo hayo makuu, hayapingiki ndani ya kila mwanaume isipokuwa Adam.
Pamoja na hivyo, zipo dhana nyingine nyingi ambazo zinafanya wanawake wasemwe vibaya. Twende kwa mifano.
Hivi karibuni, niliitwa nimshauri kijana mmoja ambaye kwa hakika alikuwa amechanganyikiwa kabisa. Alichanganywa na mapenzi. Mwanamke ambaye aliamini ndiye wa maisha yake, alimuacha katika mazingira ambayo hakuyategemea. Alikuwa anamhudumia kwa kila kitu lakini akapigwa kibuti kwa SMS.
 Kijana huyo anaitwa Mully, akiwa kazini kwake, akaona SMS iliyotoka kwa mtu ‘aliyemsevu’ kwa jina la My Dream. Kama ujuavyo tena mapenzi, kijana akafungua haraka, akitegemea atapata maneno matamu kutoka kwa mwenzi wake lakini alichokutana nacho ni hiki: “Kuanzia leo, mimi na wewe basi. Nimepata mchumba nataka kuolewa.”
Mully aliposoma maneno hayo akapagawa, akaamua kupiga simu ya mpenzi wake lakini hakupokea. Akaamua kumuuliza kwa SMS: “Baby upo serious au unatania?” Haikupita hata dakika moja, majibu yakarudi: “Nipo serious kabisa, tena kuanzia leo usiniite baby na usinijue kwa lolote.”
Meseji hiyo ikamchanganya akili kijana, akaondoka kazini kwake bila hata kuwaaga wenzake. Yule mpenzi wake anaitwa Janette, ni mtumishi wa ndani kwenye nyumba ya ofisa wa benki Masaki, Dar. Kijana akaondoka kazini kwake Mwenge hadi kazini kwa mkewe. Akili siyo zake.
Alipofika, akagonga geti halikufunguliwa, kwa hiyo akapanga matofali getini akakaa. Baadaye Janette akatoka, alikuwa anakwenda dukani, akakutana uso kwa uso na Mully. Yakaanza maneno, baby nimekukosea nini? … sikutaki… baby niambie kosa langu… nimesema sikutaki...
Mtoto wa kike akaona ubishi unampotezea muda, akaingia ndani, akatoka nje na beseni la maji machafu, akamwagia Mully. Kijana wa watu akaloa chapachapa. Janette akarudi ndani, akapiga simu kwa bosi wake, punde polisi wakafika na kumzoa, eti ni mwizi.
Kaka yake Mully akaenda kumuwekea dhamana Oysterbay Polisi. Kuanzia hapo kijana akawa amepigwa chini, akawa anazungumza hovyo, kazi akawa hafanyi. Kijana akasema: “Mbona mimi ningemuoa tu, sina shida.” Kijana akawa hali, haogi, kazi hafanyi. Akili zikamruka.
Nilijitahidi kumpa ushauri unaofaa kwa vipindi vitatu ndani ya siku tatu mfululizo, baada ya kuona anapata nafuu, nilishauri apelekwe eneo ambalo atabadili mazingira. Alipelekwa nyumbani kwao Singida. Wiki iliyopita, alirudi Dar akiwa mpya kabisa. Anatazama mbele na hamfikirii tena yule mwanamke.
 Hata kazi anaendelea vizuri. Machungu ya kuachwa na Janette yamebaki historia. Vema amekaa sawa lakini kitu ambacho kipo wazi ni kuwa Mully alimpenda 
sana mpenzi wake na aliamini ndiye mwanamke wa maisha yake. Hali hiyo ndiyo ilimfanya ashindwe kupokea matokeo ya kuachwa.
Alishawekeza mambo mengi kwa Janette hususan rasilimali. Mully aliniambia kuwa kwa siku alikuwa anampa Janette kuanzia shilingi 15,000 mpaka 20,000. Alikuwa anamnunulia mavazi ya kisasa, kiasi kwamba ukimuona, usingeweza kudhani ni mfanyakazi wa ndani.
Baadaye ikaja kubainika kuwa kumbe Janette alipata kiburi cha kuachana na Mully kwa sababu ya bosi wake. Kwamba yule ofisa wa benki baada ya kumuona mfanyakazi wake anameremeta, akaamua kujiweka, binti naye badala ya kufikiria kuwa ni mume wa mtu akakubali.
Wameendelea kuwa na uhusiano lakini za mwizi ni 40, mke akashtukia kuwa anaibiwa mumewe ndani ya nyumba yake. Akamtimua kazi Janette na kipigo juu. Yule jamaa wala hakumtetea ndiyo kwanza akashiriki kusaidia kumtimua. Binti aende wapi? Kazini ameshaharibu, kwa Mully nako alishalikoroga.
Tuachane na mateso ya Janette baada ya kutoswa na Mully aliporudi mara ya pili. Jambo la kuzingatia ni jinsi alivyomtenda boyfriend wake aliyekuwa anamhudumia na kwenda kuangukia kwa mwanaume ambaye ni mume wa mtu. Hakutafakari mwenye faida kwake ni nani, leo anahangaika.
Aina ya wanawake kama Janette ndiyo wanaosababisha wanaume watambe mitaani wakitoa maneno ya kebehi kwamba wanawake wote mwalimu wao ni kipofu. Hakutambua jema wala hakujua kwenye maisha haya anahitaji nini. Mtu anayejihusisha kimapenzi na mume au mke wa mtu, maana yake hajui kesho yake ni nini.    Itaendelea wiki ijayo.


www.globalpublishers.info

No comments: