SIKU chache baada ya Padri wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Lugoba Jimbo la Morogoro, Philipo Mkude kuzuiwa na waumini kuongoza misa baada ya kudaiwa kuwakashifu waumini
kutoka kabila la Wakwere, mmoja wa wazee wa kabila hilo ameibuka na kumtetea padri huyo.
Mwananchi huyo Clarence Mahunda, aliyejitambulisha kuwa mfanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika Kituo cha Hale mkoani Tanga ambaye kwa sasa anasomea Shahada ya Uhandisi katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), amesema maneno ya Padri Mkude ni changamoto kwa Wakwere.
Mahunda alisema kauli ya Padri Mkude ni sahihi na kwamba ametumia mbinu ambayo inawaumiza Wakwere na kuwafanya waamke na kujua walipo na kuchukua hatua.
“Mbinu hii hutumiwa hata na wazazi wanapokuwa na mtoto ambaye ni mvivu wa kula humwambia kuwa wewe hata fulani anakushinda, ili apate uchungu na asikubali kushindwa,
kisha amalize chakula,” alisema Mahunda ambaye amejitambulisha pia kuwa ni Mkwere.
“Padri Mkude anadaiwa kuwaita Wakwere ni wachafu, masikini, hawasomi na wanaendekeza
kucheza ngoma.
Amenukuliwa na majibu yake lakini mimi siyahitaji kwa kuwa ninaangalia kauli anazotuhumiwa na kutoa maoni yangu, kwani nayaelewa kiasi mazingira ya Ukwere. Mimi ni Mkwere na mama yangu ni Mluguru, kabila atokalo Padri Mkude.
“Padri Mkude ni jasiri na anafaa kuwa kiongozi. Ni viongozi wachache sana wa kijamii, kiroho
na hata kisiasa wenye uwezo wa kuwaambia watu udhaifu wao.
Ndiyo maana tunaendelea kutafunwa na uzinzi, maradhi, ufisadi na mengineyo.
“Maneno aliyoyasema kasisi huyu juu ya Wakwere ni kweli na wala hana sababu ya kuwadhalilisha; ili apate nini?
Angalia leo hii Wakwere wauzavyo maeneo ya barabarani kwa bei ya kutupa, sasa huu si umasikini? “Tembelea vijiji vingi Tanzania hii, wenyeji wanavyochangamkia nyumba za matofali ya kuchoma; Ukwere wao kimya. Sasa mtu wa namna hii atajenga choo bora?
Kuhusu shule nalo kweli mnahitaji mjadala?
“Ni nani asiyejua kuwa kuna baadhi ya mikoa ukitangaza nafasi ya kazi utapata zaidi ya asilimia 90 ya wenye sifa ni wenyeji asilia, kwa Ukwere nadhani hata utangaze kijijini waweza pata si zaidi ya asilimia 25, sasa hili nalo uongo ni upi?
Tembelea mashule, vyuo utapata ukweli, sasa tunabisha nini?” alisema Mahunda.
Alisema anahisi Padri Mkude hakueleweka na jamii husika au kuna kundi la wachache ambao si
wenyeji asilia au wanatumia udhaifu wa wenyeji kumfanya kasisi huyo aonekane mbaya.
“Kwa kuwa wanajua wenyeji wakiamka hawatapata mashamba na viwanja kwa bei ya chee, pia
wenyeji wakisoma watampa nani soda na maji akimbizane nazo katika mabasi? Kwa kweli inasikitisha sana.
“Kuhusu ngoma, Mluguru na Mkwere hawana tofauti hata huko kwao Tangeni wanacheza,
isipokuwa lazima tuwe na vipau mbele. Nina imani alimaanisha hivi na si vinginevyo.”
“Naamini wanaomtuhumu Padri Mkude hawana nia njema na Wakwere. Nahisi si wenyeji asilia”. Mahunda alisema anamfahamu Padri Mkude tangu mwishoni mwa miaka ya 1980 wakati akiwa Mkuu wa Shule wa Kigurunyembe Sekondari.
“Alitoa mchango mkubwa sana katika taaluma, nidhamu na michezo. Itakumbukwa kuwa yeye
ndiye alijenga uzio ili kudhibiti utoro ambao ulikuwa umekithiri.
Kitaaluma sitaongea kwani hatuwezi kumaliza, isipokuwa katika michezo amefunda nguli wengi katika uchezaji mpaka uongozi wa kitaifa.”
Habari Leo
No comments:
Post a Comment