MUUNGANO kati ya Tanganyika na Zanzibar unatimiza miaka 48 tangu ulipoanzishwa April 1964 baada ya Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume walipokubaliana kuziunganisha nchi zao.
Katika hati za muungano kulikuwa na mambo 11 ambayo viongozi hao walikubaliana kushirikiana ambayo ni Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, mambo ya nchi za nje, ulinzi na usalama, Polisi, mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hatari, uraia, uhamiaji, mikopo na biashara za nje na utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Mengine ni kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika,ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini unaosimamiwa na na idara ya forodha na la mwisho ni ushirikiano wa bandari, usafiri wa anga na posta na simu.
Hata hivyo baadaye mambo hayo yaliongezeka hadi kufikia 22. Yaliyoongezeka ni pamoja na mambo yanayohusika na sarafu na fedha kwa ajili ya malipo yote halali, mabenki na shughuli zote za mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni.
Mengine ni leseni ya viwanda na takwimu, elimu ya juu, maliasili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokari, mafuta aina ya petrol na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa na gesi asilia.
Mambo mengine ni kuhusu Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania na mambo yote yanayohusika na kazi za baraza hilo, usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, utafiti wa hali ya hewa, takwimu, Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano na uandikishwaji wa vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana navyo.
Pamoja na mambo yote hayo, suala la elimu hasa elimu ya juu limekuwa likigonga vichwa vya watu wengi, huku baadhi ya Wazanzibari wakihoji sababu ya jambo hilo kuendelea kuwa suala la muungano.
Kwa mfano, Kikundi cha Wazanzibari kinachodai kutambuliwa kwa Jamhuri ya Zanzibar (Zanzibari Right for Freedom Autonomy- Zarfa) kimekuwa katika mkakati wa kupigania Zanzibar ijitegemee katika mambo yake, likiwamo suala la elimu.
Kiongozi wa kikundi hicho, Rashid Salum Adiy anasema kuwa haoni sababu ya suala la elimu kwa ujumla kuwa la muungano, ikiwa tayari Zanzibar ina wizara yake ya elimu.
“Suala la elimu katika muungano lina utata mwingi, pamoja na ukweli kwamba tuko kwenye muungano, sioni sababu ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kusimamia utungaji na usahihishaji wa mitihani visiwani” anasema Adiy na kuongeza:
“Sikatai, tunweza kushirikiana kwenye vyuo vikuu, lakini huku chini kuanzia kwenye elimu ya msingi hadi sekondari, hakuna sababu. Isitoshe, silabasi za Zanzibar na Bara zinatofautiana, lakini unapofikia wakati wa mitihani, Necta wanaleta mtihani mmoja”.
Anaendelea kufafanua kwamba kwa muda mrefu suala hilo limekuwa likifanywa kisiasa zaidi, ili kuendelea kuikandamiza Zanzibar kielimu.
“Masuala mengine yamefanywa kuwa ya kisiasa tu. Ni kweli kwamba elimu ya sekondari inayotolewa Bara na Zanzibar ni ile ile tena inatolewa kwa lugha ya Kiingereza, lakini misingi ya utoaji wa elimu hiyo ni tofauti. Imefika wakati sasa Wazanzibari tuwe na mfumo wetu wa elimu unaozingatia misingi yetu,” anasema Adiy na kuongeza:
“Hata nchi nyingine kama vile Kenya inatoa elimu ya sekondari kama Tanzania, sema tu elimu ya Kenya inatolewa kwa Kiingereza tangu shule za msingi, lakini elimu ni ile ile tu. Mbona hatukuungana nao tuwe na mtihani mmoja? Zanzibar nayo ni nchi tunapaswa kuwa na mfumo wetu.”
Adiy anasema hata kwa siku zijazo, suala la elimu ya juu nalo halitokuwa na haja ya kuwa sehemu ya muungano, kwani Zanzibar imeshapiga hatua katika daraja hilo la elimu.
“Kwa sasa Zanzibar tuna vyuo vikuu tofauti na zamani ambapo tulitegemea tu vyuo vikuu vya bara. Siku za mbele tutajitegemea hata katika elimu ya juu. Hakuna sababu ya kuifanya elimu kuwa kwenye mambo ya muungano, hizo ni siasa tu,” anasema.
Naye kiongozi wa Umoja wa Vijana wa Kitaifa Zanzibar Khalid Said Suleiman, anasema wakati umefika kwa Wazanzibari kujitegemea kielimu kuanzia elimu ya chini hadi ile ya juu.
Suleiman ambaye kitaaluma ni mwanasheria na wakili wa kujitegemea, elimu aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema mfumo uliopo wa Baraza la Mitihani la Taifa siyo shirikishi.
“Wakati umefika sasa Wazanzibari tujitegemee kielimu tangu sekondari hadi chuo kikuu. Siyo kwamba tujitoe kabisa, lakini tuweke mfumo ambao utakuwa sawa na wenzetu wa bara,” anasema na kuongeza:
“Baraza la Mitihani la Taifa limekuwa likiegemea upande mmoja tu, halina hata ofisi Zanzibar wakati ni chombo cha muungano. Ingekuwa bora sasa kwa Baraza hilo kuhamia kwa muda Zanzibar na kusahihishia mitihani huku likishirikisha walimu wetu.”
Suleiman ana matumaini kwamba siku za usoni Zanzibar itajitegemea kielimu hasa kwenye elimu ya juu anayosema imepiga hatua visiwani humo.
Upande wa pili wa shilingi
Mhadhiri wa lugha wa Chuo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Martha Qorro haoni sababu ya Zanzibar kuwa na mfumo tofauti wa elimu na ule wa muungano.
“Kama sisi ni Taifa moja lililo katika muungano si vibaya tukawa na mfumo mmoja wa elimu, labda kama tunataka kutengana. Lakini kama ni umoja kwa nini kila nchi iwe na mfumo wake wa elimu?” anahoji .
Kuhusu suala la Baraza la Mitihani la Taifa kutokuwa na ofisi za Zanzibar, Dk Qorro anasema hilo ni suala la kiutawala, lakini cha kuzingatia ni sera ya elimu,
“Hilo ni suala la kiutawala, kama wanataka kuwe na tawi wanaweza kupanga, lakini kama sera yetu ya elimu kitaifa ni moja, basi hata mfumo wetu utakuwa mmoja. Ni vizuri tuwe na chombo kimoja kinachosimamia elimu kitaifa ili tuwe na mwelekeo mmoja,” anasema.
Naye mdau wa elimu, Japhet Makongo anamuunga mkono Dk Qorro akisema kwa kuwa Taifa ni moja, ni heri kukawa na mfumo mmoja wa elimu wa kitaifa.
“Kama mifumo yetu ya elimu iko tofauti na tunalenga kuwa tofauti, basi tunaweza kutofautisha hata vyombo vya kusimamia, lakini kama sisi ni Taifa moja na mfumo wetu wa elimu ni mmoja, sioni sababu za kila upande wa muungano kuwa na mfumo wake wa elimu,” anasema Makongo.
No comments:
Post a Comment