ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 23, 2012

Makinda aikataa taarifa ya Serikali

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda leo ameikataa taarifa ya Serikali kuhusu utekelezaji wa maagizo ya Bunge kuhusu tuhuma zinazomkabili aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo. 

Taarifa hiyo ambayo ilikuwa iwasilishwe leo bungeni na Serikali haikuwasilishwa. 

Makinda ameliambia Bunge kuwa amelazimika kuikataa kwa vile majibu ya Serikali hayakumridhisha. 


Kabla ya tamko hilo, Mbunge wa Karatu, Israel Natse (Chadema) alihoji sababu ya kuondolewa ratiba ya Serikali kuwasilisha majibu kuhusu azimio la Bunge kuhusu Jairo. 

Mbunge huyo aliomba mwongozo iweje suala hilo liondolewe wakati tayari ratiba iliyotolewa tangu awali ilionesha kuwa suala hilo lingepelekwa jana bungeni na Serikali. 

Akijibu mwongozo huyo, Spika alisema “Mbunge umenitangulia, lakini nilikuwa nitoe taarifa bungeni hapa kuwa majibu ya Serikali yameletwa kwangu na nimeyakataa. “Nimewarudishia wakayaandae upya kwani hayako katika kiwango ambacho Bunge tulitarajia.” 

Sakata la Jairo liliibuka wakati wizara yake ilipokuwa inawasilisha bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/12 na ikadaiwa kuwa kiongozi huyo alichangisha kiasi cha Sh bilioni moja kutoka kwenye taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara yake kwa ajili ya kusaidia kupitishwa kwa bajeti hiyo. 

Baada ya wabunge kutoa madai hayo, Serikali ilichunguza suala hilo kupitia Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utoah aliyebaini fedha zilizokusanywa hazikuwa kiasi hicho. 

Uamuzi huo wa CAG ulitangazwa na aliyekuwa Katibu Kiongozi Philemon Luhanjo kuwa Jairo hakuwa na makosa na akamwamuru arejee kazini kwa vile hakuna sehemu ambayo alivunja taratibu za kikazi. 

Hali hiyo iliwaudhi wabunge waliolazimika kuunda Kamati Teule ya Bunge ambayo katika uchunguzi wake ilimtia hatiani Jairo na hivyo wakataka Serikali ichukue hatua za kinidhamu juu ya mtumishi huyo wa umma. 

Bunge katika kujadili taarifa hiyo ya kamati teule lilitoa maazimio ambayo yanatakiwa kutekelezwa na Serikali juu ya Jairo. 

Hatua hizo za utekelezaji ndizo zilikuwa ziwasilishwe jana bungeni, lakini Makinda aliwaambia Wabunge kuwa majibu ya Serikali hayakumridhisha. 

Jairo amepewa likizo hadi sasa na nafasi yake ilishajazwa na Eliakim Maswi, ambaye awali aliteuliwa kukaimu nafasi hiyo wakati Jairo akichunguzwa na Bunge.

Habari Leo

No comments: