MTOTO mwenye umri wa miaka 9 ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu amejeruhiwa vibaya kwa moto na mama yake mzazi baada ya kumtuhumu kula chakula kwa majirani.
Tukio hilo lilitokea hivi karibuni katika Mtaa wa Ihayabuyaga Kata ya Kalangalala Tarafa ya Geita ambapo mtoto aliyejeruhiwa ametambuliwa kwa jina la Amina Said, huku Mama mzazi akitambuliwa kwa jina la Rahabu Alphonce (38).
Mtoto huyo ambaye anaendelea kupata matibabu nyumbani aliokolewa na majirani lakini hata hivyo amejeruhiwa vibaya mikono yote miwili, mgongoni na tumboni.
Akizungumzia tukio hilo katika mahojiano maalumu na gazeti hili, mtoto huyo alisema siku ya tukio alifika nyumbani na mama yake mzazi alianza kumuuliza ni kwa nini anakula kwenye miji ya watu.
Kwa upande wake mama mzazi wa mtoto huyo katika mahojiano alikiri kumuadhibu mtoto huyo kwa kumchapa fimbo, lakini akakanusha kumchoma kwa moto, huku akiwatupia lawama baadhi ya majirani aliodai kuwa hawampendi kutokana na hali yake ya kutokujiweza (umasikini) kwamba ndio waliomfundisha mtoto huyo namna ya kutoa maelezo.
Alisema aliamua kumuadhibu mtoto huyo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa bibi yake kwamba watoto wake wamekuwa na mazoea ya kula kwenye miji ya watu hali inayofanya baadhi ya familia kushindwa kushiba chakula.
Balozi aliyemuokoa mtoto huyo na kumpeleka kwenye Ofisi ya Serikali ya Kijiji, George Makaranga aliyelithibitishia gazeti hili kwamba mtoto huyo aliunguzwa na moto na mama yake mzazi.
Baadhi ya majirani walioshuhudia tukio hilo walisema Mama huyo alimchoma moto mtoto huyo kwa lengo la kumkomesha tabia yake ya kupenda kula kwenye miji ya watu,ambapo alikuwa akidai kuwa watoto wake wamekuwa na tabia ya kula kwenye miji hiyo na kumsababishia lawama kwa majirani.
Tayari mama huyo ametiwa mbaroni na kuhojiwa na Jeshi la Polisi, hata hivyo polisi wamempatia dhamana kutokana na kuwa na mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu, pamoja na wengine ambao hawana mtu wa kuwalea wala kuwapikia chakula.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Geita, Paul Kasabago amethibitisha mama huyo kukamatwa lakini akafafanua kwamba wameamua kumpa dhamana wakati wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo, kutokana na mama huyo kuishi na watoto hao peke yake kwa sababu baba yao anafanya kazi ya kukata mkaa msituni.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment