ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 23, 2012

Mawaziri walipuana


  Watuhumiana kwa kula rushwa
  Nyaraka za kuumbuana zatolewa
Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu
Mahusiano ya mawaziri yameingia mushkeli na sasa kinachoendelea miongoni mwao ni sawa na kile kinachoelezwa kuwa ni kama ugomvi wa kugombea chakula, mmoja akimwaga ugali mwingine huishia kumwaga mboga ili kila mmoja akose.
Hali hii imedhihirika baina ya mawaziri na manaibu wao katika Wizara za Uchukuzi na ile ya Viwanda na Biashara, ambako sasa kuna mnyukano usiokuwa wa kawaida.
Katika hali ambayo ni nadra kutokea, jana Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu, alifanya mkutano na waandishi wa habari na kumlipua Naibu wake, Dk. Ali Mfutakamba kuwa alihongwa na kampuni ya China Communicaation Construction (CCC), na ndiyo sababu amekuwa akiipigia debe ipewe zabuni ya ujenzi wa gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es salaam.
Vile vile, alisema haoni sababu yoyote ya kujiuzulu kwenye nafasi yake, isipokuwa analazimika kutafakari sana kuhusu shinikizo la kjiuzulu kwani aliomba kazi ya ubunge na si uwaziri.

NAIBU WAZIRI KUHONGWA
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Nundu alisema Naibu wake alisafirishwa nchi mbalimbali na kulipiwa gharama zote na kampuni hiyo lengo likiwa ni kumshawishi wapate zabuni hiyo.

Ujenzi wa gati namba 13 na 14 umezua mjadala mkali bungeni huku Kamati ya Miundombinu ikishinikiza kampuni ya CCC ipewe zabuni ya ujenzi wakati huo huo ikimshutumu Waziri Nundu kuwa anaikataa kampuni ya CCC ili zabuni hiyo ipewe kampuni anayoipigia debe ya China Merchant Limited.
Nundu alisema katika safari hizo naibu wake hakuwahi kumuaga hata safari moja, ingawa alikuwa ofisini kwake wakati wote wa safari hizo.
“Aliporudi nilimuuliza kwanini anakwenda safari bila kunijulisha mimi bosi wake akadanganya kuwa siku hizo aliposafiri mimi sikuwa ofisini, lakini kwa uhakika kabisa siku zote aliposafiri nilikuwa ofisini kwangu,” alisema Nundu.
Alitaja nchi ambazo Naibu huyo alipelekwa na kampuni ya CCC kuwa ni Mauritania na Equatorial Guinea na kwamba aliporudi aliandika taarifa nzuri ya kushinikiza kampuni hiyo ipewe zabuni ya ujenzi wa gati hizo.
“Wale watu wa CCC walikuja kwangu kunishawishi na hizo safari zao eti nikaangalie miradi yao nikakataa maana niliona kuna harufu ya rushwa, sasa walipoona msimamo wangu ni huo wakaenda kwa naibu wangu wakamshawishi na kufanikiwa kumsafirisha na kumlipia gharama zote, nilikuwa nafanya kazi vizuri sana na naibu wangu, lakini aliporudi kwenye hizo safari mambo yakabadilika kabisa, akaanza kunishawishi tuipe zabuni CCC,” alisema.
Nundu alisema msimamo wake ni kutaka zabuni hiyo zishindanishwe kampuni 11 na hatimaye mshindi apatikane ili ajenge gati hizo, lakini wenzake wamemgeuka na kumwoda adui namba moja.
Alisema haiwezekani kampuni ya CCC ambayo ni ya ujenzi ifanye upembuzi yakinifu kwa gharama za serikali ya Tanzania na kampuni hiyo hiyo iitafutie serikali sehemu ya kukopa fedha za kujengea gati hizo.
Alifafanua kuwa kampuni ya CCC ilifanya upembuzi yakinifu na kuandika taarifa kuwa ujenzi wa gati hizo utagharimu dola za Marekani milioni 542 wakati kuna kampuni ambazo zinaweza kufanya kazi hiyo kwa gharama ya dola milioni 300.
Alisema hana kampuni yoyote ya mfukoni kama wanavyomwandama wabunge wa Kamati ya Miundombinu ila anachofanya yeye ni kusimamia haki kuhakikisha kunakuwa na ushidani wa haki kwenye zabuni hiyo.

NIMEVAMIWA NA ‘MAJAMBAZI’
“Kwa hali ilipofikia najiona ni kama vile mtu amekwenda porini peke yake akajikuta kazungukwa na majambazi kisha yakaanza kumshambulia huku akijitetea, lakini majambazi yanazidi kumshambulia tu yakisema ana makosa, kosa langu nini jamani kusema kampuni 11 zishindanishwe ipatikane moja,” alisema.
Aidha, Nundu alisema shutuma kwamba kampuni ya China Merchant ni yake ni uongo na kwamba hajawahi kuingia nayo mkataba wa kibiashara (MoU) kwa ajili ya ujenzi huo kama inavyiodaiwa na wabaya wake hasa kamati ya Bunge.
Kwa mujibu wa maelezo ya kamati ya Bunge ya Miundombinu, Wizara ya Uchukuzi imeingia mkataba na kampuni ya China Merchant kujenga gati hizo kisha kuziendesha yenyewe kwa miaka 45,  jambo ambalo Waziri Nundu alisema halipo.
Alisema kampuni ya CCC tangu mwaka 2008 iliahidi kuwa itatafuta mkopo wa ujenzi wa gati hizo kutoka benki ya EXIM China, lakini hadi leo haijafanya hivyo na hata alipokwenda Makao Makuu ya benki hiyo China aliambiwa kuwa hakuna kitu cha aina hiyo.
Nundu alisema hata maelezo ya kamati ya Bunge kuwa mkopo huo una riba ya asilimia mbili si kweli kwani utafiti alioufanya amegundua kuwa serikali itabeba mzigo mkubwa wa kulipa riba ya asilimia 77 kama mkopo huo ungepatikana.
“Hizi ni pesa za Watanzania siwezi kukaa kimya nikiona zinatafunwa, ndio maana nilisema bungeni kwamba nitaingia chumbani ikibidi hadi chooni, maana yake huko kwenye uozo kote nitaingia kuhakikisha nchi haipati hasara kwa manufaa ya wachache,” alisema kwa msisitizo.
“Kwa nini Kamati ya Miundombinu inasisitiza kuwa mkopo huo wa EXIM China ukipatikana ipewe CCC, yaani gharama ya ujenzi dola milioni 300, sasa wanaweza kutuambia hizo dola milioni 242 zinazobaki zinakwenda kwenye mikono ya nani, kwa nini wanang’ang’ania wa dola milioni 542 wakati kuna kampuni zinaweza kujenga kwa dola milioni 300, ” alisema na kutaka kampuni hiyo ichunguzwe kote duniani.
Alisema alikwenda China hivi karibuni na kuziambia kampuni za huko kuja kufanya upembuzi yakinifu kuhusu ujenzi wa gati hizo kwa gharama zao na kisha ziingie katika ushindani wa zabuni hiyo.
“Nimewaambia wafanye upembuzi kwa gharama zao na ndani ya miezi sita ambaye hajakamilisha upembuzi tunamfuta, nilipokuwa China niliwaita wote nikwaeleza kuwa hayo ndo masharti yetu anayeona anaweza aje asiyeweza asije,” alisema Nundu.
UFISADI TPA
 Nundu pia aligusia ufisadi uliokuwa ufanyike katika Bandari ya Dar es Salaam kuwa ni ujenzi wa sehemu ya kuegesha magari ambao hata Rais Kikwete alishaukataa.

Alisema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari alitaka kumwingiza mkenge kwa kumshawishi mradi wa ujenzi huo utekelezwe ili hali anajua kabisa Rais Kikwete aliukataa.
Alisema mradi huo uliokataliwa na Rais Kikwete ulikuwa ugharimu Sh. bilioni 45 na kwamba ulishakataliwa baada ya kuuona kuwa hauna tija yoyote kwa taifa.
“Huu mradi awali walisema utagharimu bilioni 45, badaye wakageuka wakasema bilioni 65, siku nyingine wakasema utagharimu bilioni 55, hapo ndipo machale yakanicheza nikaona kuna ufisadi hapa, nikashtuka kwamba naingizwa mkenge nikakataa,” alisema
“Baada ya kuukataa mradi huo  Mkurugenzi Mkuu wa TPA akaja ofisini kwangu na maelezo mengi ya kuutetea mradi huo, eti tusipoutekeleza mzabuni atatutoza faini ya bilioni 45, sasa inashangaza mradi haujaanza hiyo faini inatoka wapi jamani kama siyo kuingizana mkenge, mimi nilimweleza kuwa waliomshauri wamempotosha na kama ni bodi nikamwambia aivunje, aliivunja lakini kwa shingo upande,” alisema na kuongeza kuwa tangu akatae mradi huo hana maelewano mazuri na Mkurugenzi wa TPA.
Alisema amekuwa akifanya mikutano mbalimbali na wakurugenzi wa mashirika yaliyo chini yake na wamekuwa wakihudhuria kasoro Mkurugenzi Mkuu wa TPA ambaye mara zote humtuma mwakilishi wake.
Nundu alihitimisha kwa kusema kuwa ataendelea kufanya kazi kwa uzalendo na maadili katika wizara hiyo na kuwaumbua wote wanaojali maslahi yao binafsi badala ya maslahi ya taifa.
Alisema mradi wowote ambao atagundua umepatikana kwa njia za rushwa atausimamisha hata kama umeshaanza na kuwawajibisha maofisa wa wizara watakaobainika kujihusisha na michezo michafu.
MFUTAKAMBA AKANA
NIPASHE ilimtafuta Mfutakamba juu ya tuhuma alizoeleza Waziri Nundu na amekana kuhusika katika mchakato wa tenda ya ujenzi wa bandari.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, Mfutakamba alisema hahusiki katika zabuni kwa kuwa kuna chombo maalum cha kufanya kazi hiyo.

Alisema moja ya kazi zake ni kumshauri waziri wake, lakini siyo kushinikiza kampuni fulani ipewe kazi.
“Nafanya hivyo ili nipate kitu gani kutoka kwenye kampuni husika ninayoipigia debe na unajua ndugu mwandishi masuala ya tenda yana chombo chake maalum ambacho kinafanya kazi hiyo,” alisema.

Aidha, alikanusha madai kwamba aliwahi kuondoka nchini bila kumuaga Waziri wake. “Nimekaa serikali muda mrefu najua utaratibu siwezi kuondoka nchini bila kumuaga waziri wangu pamoja na Waziri Mkuu, sasa nikifanya hivyo halafu nikapata matatizo nitajibu nini?” alihoji.
Alisema yeye na waziri wake wanafanya kazi vizuri na mahusiano yao yapo vizuri.

YA CHAMI YAANIKWA

Wakati Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, akidaiwa kutumia nguvu zake zote kumlinda Mkurugenzi wa Shirika la Viwango (TBS), Charles Ekelege, nyaraka zinazoonyesha Waziri huyo kuwa na taarifa juu ya hali ya TBS zimevuja zikimtaka achukue hatua, lakini hakufanya hivyo.

Kufichuka kwa hali hii kunathibitisha maneno ya Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjimbe (CCM) ambaye Ijumaa iliyopita aliweka wazi bungeni kuwa ingawa hakuna ushahidi wa Waziri Chami kuwa alikuwa ananufaika na fedha za makampuni yaliyokuwa uanagagua magari, amekuwa anatumia nguvu nyingi sana kulinda TBS ili watendaji wake wasiwajibike.

Filikunjombe ambaye pia Ijumaa hiyo alimtaja wazi Waziri wa Fedha, Musatafa Mkulo, bungeni juzi kuwa si kiongozi mwaminifu, na kwamba amekuwa akifanya maamuzi kwa kujinufaisha binafsi, alishangaa nguvu inyotumiwa na Dk. Chami kuilinda TBS wakati uchunguzi uliofanywa na kamati ya wabunge iliyokwenda Hong Kong na Singapore kufanya uchunguzi wa kampuni zinazokagua magari kabla ya kuja nchini iligundua madudu ya kutisha na udanganyifu mkubwa kwani hazina ofisi huko ingawa zimekuwa zikilipwa mabilioni ya fedha kwa kazi hiyo.

Kuibuliwa kwa waraka huu kuwa Waziri Chami amekuwa kizingiti cha kuwajibishwa kwa watendaji wa TBS, kunazidi kumweka katika wakati mgumu katika hasira za wabunge za kuwataka mawaziri wanane wawajibike kwa ama kushindwa kazi au kuwa sehemu ya ubadhirifu uliobanishwa kwenye ripoti tatu za kamati za kudumu za Bunge, Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC). Ripoti hizo ziliridhiwa na Bunge Jumamosi.

Katika waraka huo kwenda Dk. Chami, ulioandikwa Februari 10, mwaka huu, ukimshauri hatua za kuchukua dhidi ya Mkurugenzi wa TBS juu sakata la ukaguzi wa magari nje ya nchi, Dk. Chami anadaiwa ama kuupuuza au kutafuta visingizio vya kutoutekeleza nia ikiwa ni kuilinda TBS kama alivyodai Filikunjombe juzi.

Kutokana na kifua cha Dk. Chami, imebainika kwamba Mkurugenzi wa TBS ambaye anatuhumiwa kuhusika na ubadhirifu huo amekuwa kazini wakati wote wa ukaguzi kinyume cha pendekezo la wabunge.

Katika kikao cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), PAC, POAC na Wizara ya Viwanda na Biashara, ilikubaliwa kwamba Mkurugenzi Mkuu wa TBS asimamishwe kazi ili kupisha uchunguzi huru ambao ungefanywa na CAG.

SIMAMISHA BOSI TBS
Uchunguzi wa NIPASHE umebaini kwamba baada ya kikao hicho, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Lazaro Nyalandu, alimwandikia barua Waziri wake, akimweleza yaliyojiri kwenye kamati za Bunge na kumshauri amsimamishe kazi kwa muda Mkurugenzi wa TBS kama wabunge walivyokuwa wamependekeza; lakini katika hali ya isiyoeleweka jambo hilo halijafanyika hadi sasa.

“Kama ulivyoniagiza leo (Februari 10), nimeshiriki kikao cha pamoja cha kamati tatu za Bunge kilichokaa chini ya uenyekiti wa Mhe. John Cheyo…katika kikao cha briefing na CAG na wabunge, TBS imeshutumiwa kuhusiana na ukaguzi wa magari nje na mchakato wote unaohusiana na suala hilo,” inaeleza sehemu ya barua ya Nyalandu kwenda kwa Waziri Chami.

Katika barua hiyo ambayo NIPASHE inayo nakala yake, inaeleza kwamba Mkurugenzi huyo alilidanganya Bunge kuhusu kampuni zinazofanya ukaguzi wa magari na bidhaa nyingine nje ya nchi na kwamba TBS ilitoa taarifa za uongo juu suala hilo kwani uchunguzi wa kamati ya wabunge iliyokwenda Hong Kong na Singapore iligundua mambo tofauti na yaliyokuwa yameelezwa na Mkurugenzi huyo juu ya ukaguzi wa magari nje ya nchi.

“Wabunge wametoa mapendekezo ya kuiomba Wizara imsimamishe kazi kwa muda mkurugenzi wa TBS ili kupisha uchunguzi wa CAG juu ya tuhuma hizo,” ilifafanua barua ya Nyalandu ambayo pia alitoa nakala kwa katibu mkuu wa wizara hiyo pamoja na naibu wake.

Iliongeza kwamba: “kutokana na unyeti wa TBS na shutuma zilizotolewa, nakushauri uangalie uwezekano wa kumsimamisha kazi kwa muda Mkurugenzi wa TBS ili apishe uchunguzi wa CAG na endapo hatakuwa na tuhuma za kujibu basi arudishwe kazini mara moja.”

Hata hivyo, inaelezwa kwamba CAG amefanya ukaguzi katika shirika hilo, lakini Mkurugenzi huyo hajasimamishwa kazi kama ilivyopendekezwa na wabunge.

Hayo yameibuka wakati ambao wabunge wanawashinikiza mawaziri ambao sekta zao zimebainika kufanya ubadhirifu wa mali za umma wajiuzulu akiwemo Chami ambaye amesema Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Charles Ekelege, asingeweza kusimamishwa kwa sababu ni mteule wa rais bila kufuata taratibu wala kuwa na ushahidi wa tuhuma zinazoelekezwa kwake.

NYALANDU: NIPO MBALI
NIPASHE ilipomtafuta Nyalandu kwa simu jana kuzungumzia shinikizo la wabunge kuhusu sakata la TBS alisema yupo Afrika Kusini kikazi na kwamba asingeweza kusema chochote.

"Siwezi kusema chochote yaani hata sijui nini kinaendelea huko, nipo safarini Afrika Kusini, naomba uniache kwanza pengine nikirudi nitakuwa na cha kusema," alisema.

KAULI YA CHAMI
NIPASHE ilipomtafuta Chami kuhusiana na dokezo hilo, alisema Nyalandu alimwandikia dokezo kuhusiana na suala hilo, lakini alishindwa kuchukua hatua kwa kuwa hakuwa amepata tuhuma thabiti za kumpekekea Rais pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa TBS kwa ajili ya kutekeleza agizo la Bunge.

"Taratibu za kumsimamisha zinafanywa baada ya kushauriana na Rais, kwa hiyo nisingeweza kuchukua hatua kabla sijapata tuhuma zinazomkabili Mkurugenzi," alisema Chami na kuongeza kuwa tayari CAG amekwishafanya ukaguzi wake kuhusu tuhuma hizo.

Mwaka 2010, wabunge wa Kamati ndogo ya Kamati ya Hesabu za Serikali (POAC), wakiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Mbarali (CCM), Estelina Kilasi, ilikwenda Singapore na China kukagua kampuni zinazokagua magari yanayoingizwa nchini, kwa niaba ya Shirika la Viwango TBS.

Baada ya wabunge hao kurejea nchini, walidai kuwa kampuni hizo ni hewa kwani katika nchi walizokwenda hawakukuta ofisi wala wawakilishi wa kampuni hizo.

Kutokana na madai ya wabunge hao, Februari 2012, Ofisi ya CAG,  nayo ilituma wakaguzi kwa ajili ya kukagua ofisi za ukaguzi wa magari nje ya nchi zinazosimamiwa na TBS.

Hatua hiyo ilikuja baada ya kamati za POAC, PAC na Fedha na Uchumi, kudai kuwa Mkurugenzi wa TBS, Charles Ekelege, aliwasilisha taarifa za uongo kwamba Tanzania ina ofisi ya ukaguzi wa magari nje ya nchi wakati siyo kweli.

CAG, Ludovick Utouh, alisema kutokana na tuhuma zenyewe kuhusisha nje ya nchi, ofisi yake inalazimika kutuma wakaguzi ili kufanya uchunguzi na kuhakiki ukweli kuhusu tuhuma hizo.

Januari 27, mwaka huu POAC na PAC zilibaini kuwapo kwa tuhuma hizo zilizoelekezwa kwa mkurugenzi huyo na kumtaka asimamishwe kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yake.
Ukaguzi huo unadaiwa kupoteza fedha za umma dola za Marekani 18,343,540 ambazo ni zaidi ya Sh. bilioni 30.

Imeandikwa na Richard Makore, Restuta James, Dar na Joseph Mwendapole, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE

No comments: