Ni uzembe wa manesi
Tukio hilo lilitokea saa 11:30, Jumatano ya wiki hii ikimhusu mwanamke huyo, Kuruthum Abdallah (30), mkazi wa Majohe.
Akiongea na NIPASHE Jumapili baada ya tukio hilo, Kuruthum alisema pamoja na dalili za kuzidiwa alizokuwa nazo, alitakiwa na muuguzi wa zamu kusubiri ili atoe maelezo binafsi.
Kuruthum alisema baada ya kufika hospitali hapo akisindikizwa na mumewe Jabir Yahya (38), alipelekwa kwenye wodi namba sita iliyo maalum kwa ajili ya wajawazito.
Alisema muuguzi aliyekuwa zamu, alimuelekeza akabadilishe nguo kisha amfuate ili kutoa maelezo hayo.
“Nilimwambia kwa hali niliyokuwa nayo nisingeweza kwa maana nilikuwa karibu kabisa kujifungua,” alisema.
Kuruthum alidai kuwa muuguzi huyo alionekana mkali na kumtaka afanye kama alivyomueleza, kwani wakati wa `kudeka’ umekwisha na kwamba wakati akiupata ujauzito huo (muunguzi) hakuwepo.
Alidai kuwa alimua kumfuata muuguzi huyo hadi katika meza yake, lakini kipindi hicho uchungu uliongezeka kiasi cha kutoweza kusimama vizuri.
"Nilikwenda hadi katika meza yake na alianza kuniuliza maswali, kwa kweli nilichoweza kujibu ni maswali machache tu kwani uchungu ulizidi, nilijaribu kumwambia tena hakunisikiliza," alisema.
Alisema kutokana na kukabiliwa na maumivu makali ya uchungu, alijaribu kumshika muuguzi huyo ili asikilize anachomueleza, hata hivyo hakumsikiliza.
Alisema wakati anahangaika kujibu maswali, ghafla alishtukia mtoto akitoka na kuangukia sakafuni.
"Nilishtukia mtoto akitoka na kuangukia sakafuni na kisha kuserereka hadi chini ya meza, tukio lilinishtua sana na hata watu waliokaa mlangoni walipiga kelele ya hofu," alisema mama huyo.
Baada ya kuona hivyo muuguzi huyo alifunga haraka mlango, kisha alimuokota mtoto huyo ambaye kipindi hicho alikuwa akilia na kumpeleka kwenye chumba cha wazazi kwa kumsafisha. Hata hivyo mume wake, Yahya alisema tukio hilo alishuhudia kwa macho yake na lilimuogopesha sana kiasi cha kutokuwa na matumaini ya kumpata kichanga akiwa hai.
Akizungumzia tukio hilo, Daktari Kiongozi wa hospitali hiyo, Shauri Mwaluka alisema hawajapata malalamiko yoyote kutoka kwa wazazi wa mtoto huyo.
Aliwataka wazazi hao kwenda ofisini kwake kutoa malalamiko yao rasmi ili yafanyiwe kazi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
1 comment:
jamani huu sio unyama kweli? huyo muuguzi anatakiwa kuchukulia hatua za kisheria hata kama mtoto ni mzima which is tunamuombea kwa mungu ampe afya yake. kitendo cha kutomzikiliza mzazi peke yake ni ukatili wa kutosha. Na sijui kwanini serikali yetu bado inawaachia hawa wauguzi kuwanyanyasa wazazi????????
Post a Comment