ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 22, 2012

PINDA KUWAUMBUA MAWAZIRI KESHO


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
-Je, watamkabidhi barua za kujiuzulu?
-Zitto kukabidhi majina 71 kwa Makinda
BAADA ya kuingia vibaya katika mapumziko ya mwisho wa wiki, kesho Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anawaumbua mawaziri wanaoshinikizwa kujiuzulu.
Pinda amesema ataweka mambo hadharani kuhusu hatima ya mawaziri hao, ikiwa ni pamoja na kama watamkabidhi barua za kujiuzulu.

Shinikizo la kuwataka mawaziri hao kujiuzulu, lilikuwa kubwa kuanzia kikao cha Bunge kilichoketi Alhamisi, ambapo wabunge wa CCM na upinzani waliungana kuwataka mawaziri hao kujiuzulu.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, Pinda alisema hadi sasa hajapokea barua ya kujizulu kutoka kwa Waziri yoyote.
Alipobanwa azungumzie habari zilizochapishwa kwenye baadhi ya magazeti kuhusu kujiuzulu kwa mawaziri nane, Pinda alisema hajasoma magazeti hivyo hawezi kuzungumza chochote.
“Sijapata barua yoyote hadi sasa ila kama wapo watakaoleta nitapokea, ila mambo yote yatajulikana Jumatatu, siwezi kuyazungumza kwa sasa,” alisema Pinda.
Juzi usiku, wabunge wa CCM walifanya kikao cha dharura na miongoni mwa mambo yaliyoazimiwa kwa mujibu wa vyanzo vya ndani ya kikao hicho, ni mawaziri nane kutakiwa kujiuzulu wenyewe.
Mawaziri ambao ilisemekana kuwa walishinikizwa na wabunge wajiuzulu kwani wamekuwa mzigo kwa serikali ni pamoja na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Mkuchika.
Wengine ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu, Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe.
Jana kuna habari zilizoenea mjini hapa ambazo hazijathibitishwa kuwa baadhi ya mawaziri wameshaanza kuandika barua za kujiuzulu kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
ZITTO KUKABIDHI SAINI ZA WABUNGE
Habari zaidi zinaeleza kuwa Zitto atawasilisha waraka wenye saini za wabunge kwa ofisi ya Spika Anne Makinda kesho, licha ya Spika huyo kutamka kuwa mchakato huo ni batili.
Kwa mujibu wa mujibu wa Mratibu wa zoezi hilo, Raya Ibrahim Khamis, kuwa hadi kufikia jana jioni wabunge 71 kutoka vyama vyote vyenye wawakilishi bunge isipokuwa mbunge mmoja chama cha UDP, John Cheyo walikuwa wamesaini katika hoja hiyo.
“Sisi tunaendelea na zoezi letu kama kawaida, tutawasilisha Jumatatu hadi kufikia mkutano ujao wa bajeti siku 14 zitakuwa zimeshapita na hivyo kukidhi haja,”alisema Raya ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema).
Hata hivyo, alisema endapo mawaziri wanaotuhumiwa kwa udhaifu katika utendaji wao watakuwa wamewajibika, wataiondoa hoja hiyo.
WALIOSAINI HAWA HAPA
Wabunge waliosaini ni Rashid Ally Abdallah,Salum Ali Mbarouk, Salum Khalfan Barwany, Mkiwa Hamad Kiwanga, Faki Haji Makame, Kombo Hamis Kombo, Magdalena Sakaya na Asa Othman Hamad wote wa CUF.
Prof. Kuliyokela Kahigi, Naomi Kaihula, Sylvester Kasulumbayi, Raya Ibrahim Khamis, Chiku Abwao, Paulinr Gekul, Rebecca Mngodo, Rachel Mashishanga, Mustaph Akoonay, Annamery Stella Mallac, Mhonga Ruhwanya, Sabreena Sungura, Conchesta Rwamlaza, Joseph Selasini, David Silinde, Rose Sukum, Cecilia Paresso na Kabwe Zitto wote wa Chadema.
Orodha hiyo inaonyesha kuwa wengine waliosaidi kuwa ni Deo Fi Maryam Msabaha, Peter Msigwa, Christowaja Mtinda, Philipa Mturano,Christina Mughwai, Joyce Mukya, Israel Natse, Philemon Ndesamburo, Vicent Nyerere, Jeremia Opulukwa na Lucy Owenya wote wa Chadema.
Deo Filikunjombe na Aphaxar Lugola wote wa CCM. Wengine ni Susan Kiwanga, Joshua Nassari, Tundu Lissu,Grace Kiwelu, Susan Lyimo, Esther Matiko, Joseph Mbilinyi, Freeman Mbowe, Kuruthum Mchuchuli, Halima Mdee, John Mnyika, Shibuda Magalle wote wa Chadema,
Wengine ni Moses Machali (NCCR-Mageuzi), Augustino Mrema (TLP),
Wengine ni Ahmed Juma Ngwali, Rashid Ali Omar, Moza Abedi Said na Hamad Rashid Mohammed wote wa CUF.
Wengine ni Abdallah Haji Ali, Khatib Said Ali, Hamad Ali Hamad, Riziki Omar Juma, Haji Khatib Kai, Hamad Rashid Mohamed, Rajab Mbarouk Mohamed, Thuwayba Idrisa Muhamed, Masoud Abdallah Salum, Muhamad Ibrahim Sanya, Ali Khamis Seif, Haroub Muhammed Shamis na Amina Amour Nassoro ambao wote wanatoka chama cha CUF.
Hoja hiyo iliwasilishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto, ambapo alisema wanafanya hivyo kwa kuwa Bunge linammudu kumwajibisha Waziri Mkuu pekee kwasababu alithibitishwa na wao.
Ingawa wabunge wengi wa CCM hawakujitokeza kusaini katika hoja hiyo imefahamika wabunge karibu wote wanaunga mkono uamuzi huo baada ya kuchoshwa na kutowajibika kwa mawaziri.
BANDARI YA DAR YAIBUA MAPYA
Wakati huo huo, ujenzi wa gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam jana ulizua tafrani bungeni kutokana na mabishano makali baina ya Kamati ya Miundombinu inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba, Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu na baadhi ya wabunge.
Mabishano hayo yalitokea kuhusu upembuzi yakinifu unaodaiwa kufanywa na kampuni ya kigeni China Communication Construon Company (CCC), kuhusu ujenzi wa gati hizo na kuweka ghalama ya dola za Marekani milioni 325.
Wabunge wengi walihoji iweje serikali itegemee upembuzi yakinifu uliofanywa na kampuni ya kigeni ambayo wakati huo huo ndiyo inatarajiwa kupewa zabuni ya kujenga gati hizo.
Mbunge wa Ubungo, Chadema John Mnyika, alitaka serikali iteue kampuni inayojitegemea kwa ajili yaa kufanya upya upembuzi yakinifu ili kujua gharama halisi zitakazotumika kujenga gati hizo.
Alisema kutegemea upembuzi yakinifu uliofanywa na kampuni ya kigeni kunaweza kulitia hasara kubwa taifa hivyo alitahadharisha serikali ijiridhishe kwanza kabla ya kutoa zabuni ya ujenzi.
Awali, katika ripoti ya Kamati ya Miundombinu, iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake, Peter Serukamba, ilisema Mamlaka ya Bandari TPA ikishirikiana na kampuni hiyo ya China, ilishafanya upembuzi yakinifu hivyo hakuna haja ya kurudia upya.
Serukamba alisema kuanza upya kufanya upembuzi yakinifu ni kupoteza muda wa ujenzi wa gati hizo ambazo zilianza kuzungumzwa tangu mwaka 2008.

No comments: