ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 25, 2012

Gharama za matibabu MOI juu mara tatu zaidi


Hospitali ya Taifa Muhimbili
Waandishi Wetu 
KATIKA hali inayoashiria mwendelezo wa mfumuko wa bei nchini, Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi), imepandisha gharama za huduma zake kati ya asilimia 80 na 300.Ongezeko hilo la gharama za matibabu limekuja katika kipindi ambacho tayari, kumekuwa na ongezeko kubwa la gharama za maisha katika bidhaa muhimu za chakula yakiwemo mazao ya nafaka.

Kutokana na ongezeko hilo, wapo wagonjwa walioshindwa kupata huduma ya matibabu kwasababu hawakuwa na fedha zinazotosheleza kupata huduma walizokuwa wakizihitaji.

Jana, Ofisa Uhusiano msaidizi wa Moi  Frank Matua alithibitisha kupanda kwa gharama hizo na kwamba jambo hilo ni utekelezaji wa sera za huduma za afya katika hosipitali hiyo. “Kweli gharama zimepanda, lakini, mchanganuo halisi bado haujapangwa,” alisema Matua alipozungumza na gazeti hili ofisini kwake jana.

Matua alisema kwa sasa taarifa bado hazijawa rasmi na unahitajika muda zaidi wa kuandaa takwimu za kuonyesha mchanganuo halisi wa gharama hizo zitakavyotozwa. Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa ongezeko hilo linahusisha huduma zote zinazotolewa na taasisi hiyo.

Miongoni mwa huduma hizo ni kumwona daktari ambazo zimeongezeka kutoka Sh2,000 za awali hadi Sh8,000, huduma ya X - ray kutoka Sh5,000 hadi Sh9,000 wakati gharama za matibabu zimepanda kwa viwango tofauti kwa kuzingatia aina ya ugonjwa.

Kabla ya kupanda kwa gharama hizo za matibabu, uongozi wa Moi ulitoa tangazo ambalo limebandikwa kwenye ukuta ofisini kwa muhasibu likieleza kupanda kwa gharama hizo, lakini bila kuonyesha viwango vya ongezeko hilo. "Kuanzia Mei 21 mwaka huu gharama za matibabu zitapanda," inasomeka sehemu ya tangazao hilo lililopo kwenye ofisi ya mhasibu.

Kauli za wagonjwa
Mmoja wa wagonjwa waliokuwa wakisubiri matibabu ambaye alijitambulisha kwa jina la Abdallah Selemani, alisema ongezeko la gharama za tiba ni kikwazo kwa wagonjwa, kwani  wengi wao hawana uwezo wa kumudu gharama hizo.

“Wapo waliorudi nyumbani kwasababu ya ongezeko hilo ukizingatia kwamba imekua ghafla,”alisema Selemani.

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Debora Ramadhani ambaye pia alikuwa akisubiri matibabu, alisema licha ya ongezeko la gharama za matibabu pia dawa wanazoandikiwa bei zake zimeongezeka na kwamba watu wa kawaida hawawezi kuzimudu.

“Baada ya kuandikiwa dawa na daktari unaambiwa ununue katika maduka yaliyopo katika eneo hilo, lakini wanauza dawa bei kubwa,”alisema Debora.

Mmoja wa wagonjwa  aliyongea na gazeti hili kwa njia ya simu, Yusuph Juma, aliyefika hospitalini hapo kwa ajili ya kutibiwa na kushindwa kupata huduma, alisema  gharama hizo zimebadilika kwa asilimia 300 na kufanya wagonjwa wengi kushindwa kupata matibabu.

Juma alifafanua kuwa awali wagonjwa waliokuwa wakitumia kadi za Bima ya Afya walikuwa wakilipa Sh21,000 kumuona daktari, lakini hivi sasa gharama hizo zimepanda kwa Sh 30,000.

“Na bei hiyo niya majira ya asubuhi, kuanzia mchana malipo ni Sh40,000 hiyo ni bei halali kabisa na stakabadhi zinatolewa kwa wagonjwa waliofanya malipo,”alisema Juma. Aliendelea kusema  kwa watu wanaolipa fedha tasilimu kumuona daktari ni Sh8,000 badala ya Sh 2000 ambayo ilikuwa ikitumika zamani.

Akizungumzia huduma za mazoezi ya viungo alisema kuwa na huko pia gharama zimepanda kutoka Sh10,000 hadi sh 15,000. Alisema kuwa mabadiliko ya gharama hizo za matibabu yalikuwa yakiwagusa sana wagonjwa wanaotibiuwa kwa kutumia fedha tasilimu tofauti na wale wanaotumia kadi za bima.

“Unajua wanaotibiwa kwa kadi wala huwa hawafanyi uchunguzi wa gharama wanazotumia tofauti na mgonjwa anayetoa fedha taslimu,”alisema na kuongeza:

“Wiki moja waliyotumia katika kutoa matangazo ya gharama mpya za matibabu haikuwa inatosha kwani imeleta usumbufu kwa wagonjwa wanaotoka  mikoani ukizingati sasa hivi kuna hali ngumu ya maisha”.

Habari hii imeandaliwa na Mariam Sangoda na Bakari Kiango na Sheilla Sezzy, Mwanza

1 comment:

Anonymous said...

hamtakiwi waislamu mtibiwe pale kwa sababu wengi ni walala hoi ndo maanake itakuwaje waongeze bei kiholela holela wakati wanapata ruzuku kutoka serikalini na kodi za ushuru hawalipi za machine meaning vipaa vyao wanavyotumia kama xray machine,etc
wadanganyika tena wa kiislamu mnazulumiwa lakin mola yupo pamoja na nyiny daima amin