ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 25, 2012

Mbulgaria adaiwa kuiba Standard Chartered-Habari Leo

RAIA wa Bulgaria Petaz Petov Ninkov (32) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kuiibia Benki ya Standard Chartered Sh milioni 35 kupitia mashine za ATM. 

Ninkov alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa shitaka la hilo mbele ya Hakimu Mkazi Tarsila Kisoka. 

Wakili wa Serikali Aidah Kisumo alidai kuwa kati ya Februari 6 na Aprili 4 mwaka huu katika benki hiyo tawi la Ilala, Ninkov aliiba dola za Marekani 23,000 kutoka katika mashine ya kutolea fedha (ATM) mali ya benki hiyo. 

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa Mei 17 mwaka huu katika benki hiyo, Ninkov alikuwa na nia ya kuiba fedha hizo kwa kupitia mashine ya ATM. 

Mshitakiwa alikana kutenda kosa na kurudishwa rumande hadi Juni 6 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena. 

Katika hatua nyingine, Frank Kivenule (28) amefikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na shitaka la kuiba pikipiki yenye thamani ya Sh milioni 1.8. 

Mwendesha Mashitaka Credo Rugaju alidai mbele ya Hakimu Pamela Kalala kuwa, Aprili 11 mwaka huu saa 6:00 mchana katika ofisi za Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Kivenule aliiba pikipiki yenye namba za usajili T 131 BMN mali ya Godfrey Sewa. 

Mshitakiwa alikana shitaka na kurudishwa rumande hadi Juni 7 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

1 comment:

Anonymous said...

aisee hii kali lakin ndo hivyo tena wadanganyika kila siku wadanganye na serikali yao na pia na watu wa njee halafu hata hatuabiwi amejaribu kuibiya vipi katika hii ATM,Kwamfana kama alikuwa fundi wa ATM, AU Katumia kaji kiujanja ujanja etc duu kila kitu siri siri wadanganyika poleni kwa kudanganywa kila leo kidumu chama cha mapinduzi, zidumu sera za baba wataifa ha ha ha