ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 25, 2012

‘Sugu’: Fedha za mfuko wa jimbo zitumike kwa wakati


Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi
Godfrey Kahango, Mbeya. 
MBUNGE wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi maarufu kama  “Sugu”, amesikitishwa na kile alichodai kuwa fedha za mfuko wa Mbunge millioni 10 zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Kata ya Itagano iliyopo jijini hapa hazijatumika kwa zaidi ya miezi mitano. 

Mbilinyi aliyasema hayo akiwa  katika ziara ya kukagua shughuli mbalimbali za miradi ya maendeleo zahanati za vijiji na vyumba vya  madarasa na zahanati za vijiji katika kata hiyo. 

Alieleza kushangazwa na kutotumika kwa fedha hizo hadi sasa, hali  inayokatisha tamaa ikizingatia wananchi wa eneo hilo wanalazimika kutembea kwa zaidi ya kilomita 45 kufuata huduma ya matibabu katika  zahanati iliyopo Kawetele Mbeya vijijini. 

“Watu wanaendelea kupata shida ya kutembea mwendo mrefu kufuata matibabu katika zahanati iliyopo zaidi ya  kilomita 45 wakati jengo la zahanati lipo hatua za mwisho, lakini kutokana na uzembe wa viongozi wa kata hiyo ndiyo maana hadi sasa ndiyo maana jengo hilo halijakamilika. ” Alisema. 
Alisema ni ajabu kwa wananchi kuona viongozi hawatoi sababu za kueleweka kuhusu kutotumia fedha hizo kwenye jambo la msingi kama hilo. 

Hata hivyo Mbunge huyo alimtupia lawama diwani wa kata hiyo Abel Ndalama (CCM) kwa kile alichodai kuwa hajaonyesha ushirikiano wowote hata kumpatia sababu za kusuasua kwa matumizi ya fedha hizo huku wananchi wake wakiendelea kuteseka. 

Kwa upande wake diwani Ndalama alikiri kuwepo kwa tatizo hilo ambapo alifafanua kwamba fedha ya mfuko wa jimbo haija anza kutumika kwa kuwa jengo hilo kwa sasa linasimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ( TASAF).  

“Ni kweli pesa ya Mbunge haija anza kutumika kwa kuwa TASAF kwa sasa ndio wanaolisimamia jengo hilo na pesa yao haija malizika, hivyo  hatuwezi kuchanganya na pesa ya mfuko wa jimbo tunasubiri TASAF wamalizie eneo lao ndipo fedha hiyo ianze kutumika.”Alisema. 

Ndalama alisema hatua iliyobaki ni ya umaliziaji, na kwamba hadi kufikia mwisho wa mwezi juni mwaka huu litakuwa tayari na wananchi wataondokana na adha wanayoipata kwa sasa.


Mwananchi

No comments: