Huduma MOI na Muhimbili tete
Mikoani madaktari kazi nusu nusu
Mikoani madaktari kazi nusu nusu
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Dk. Stephen Ulimboka, akizungumza na NIPASHE jana alisema madaktari hawawezi kupuuza amri ya mahakama, lakini kwa kuwa zuio hilo halijapelekwa rasmi kwao wataendelea na mgomo huo.
“Madaktari vile vile wanazijua sheria walipaswa kutuletea ‘correspondence’, siyo suala hilo wanakwenda kulitoa kwenye vyombo vya habari kabla ya kutuletea, serikali iache kupiga siasa katika suala hili, tunasisitiza mgomo utaendelea kuwepo hadi madai ya msingi yatakapopatiwa ufumbuzi,” alisema Dk. Ulimboka.
Dk. Ulimboka alisema hata hivyo serikali inapaswa kutafuta njia nyingine ya kumaliza mgogoro huo badala ya kukimbilia mahakamani jambo ambalo halitasaidia kufikia mwafaka.
Alipoulizwa kwamba watu wanahoji kuwa anakazania mgomo wakati yeye siyo mtumishi wa serikali, alisema suala hilo halina msingi kwani waliomchagua walilifahamu hilo, lakini kutokana na uwezo alionao walishawishika kumchagua.
TAASISI YA MIFUPA (MOI)
Hata hivyo, wakati MAT wakieleza hayo, katika Taasisi ya Mifupa (MOI), huduma za matibabu kwa wagonjwa zimesitishwa kutokana na madaktari kutokuwepo maeneo yao ya kazi jambo lililosababisha msongamano wa wagonjwa eneo la mapokezi.
NIPASHE ilifika hospitalini hapo na kujionea msongamano wa wagonjwa huku wengine wakichukuliwa na ndugu zao kuwahamishia katika hospitali binafsi na wengine wasiokuwa na uwezo kuwarudisha majumbani.
Baadhi ya wagonjwa walieleza kuwa walifika hospitalini hapo tangu saa 2:00 asubuhi na hadi saa 7:00 mchana walikuwa hawajapatiwa huduma yoyote.
Wagonjwa hao walisema walielezwa na wauguzi wa zamu kuwa madaktari hawajafika kazini na hivyo waendelee kuwasubiri.
Mmoja wa wagonjwa hao, Ramadhani Mussa, ambaye amevunjika mguu, alisema licha ya kuwahi mapema katika hospitali hiyo hajafanikiwa kupata matibabu yoyote.
“Nimefika saa moja asubuhi, lakini mpaka sasa sijapata matibabu yoyote, nimeambiwa na mhudumu wa zamu nirudi nyumbani mpaka nitakaposikia kwenye vyombo vya habari kuwa mgomo umeisha,” alisema Mussa.
Ofisa Habari wa MOI, Jumaa Almasi hakuweza kupatikana kuelezea tatizo hilo ambapo ofisi zake zilikuwa zimefungwa.
HUDUMA MUHIMBILI HAKUNA
Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) madaktari wengi hawakuonekana katika sehemu zao za kazi na hivyo wagonjwa kukosa huduma.
Katika mbao za matangazo hospitalini hapo kulikuwepo na matangazo kutoka uongozi wa juu wa hospitali hiyo ukiwataka madaktari kusitisha mgomo kwa madai ya kuwa amri imetoka katika Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Sehemu ya tangazo hilo lilisomeka: “Hii ni kuwafahamisha madaktari na wafanyakazi wengine wote kwamba Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Kazi imezuia mgomo wa madaktari uliopangwa kufanyika nchi nzima.”
Tangazo hilo lililotiwa saini na Mkurugenzi Mtendaji MHN, Dk. Marina Njelekela, liliendelea kusomeka kwamba: “Mahakama Kuu kitengo cha Kazi imeamuru kusitishwa kwa mgomo huu mara moja kwa kuwa haujafuata utaratibu wa migomo katika maeneo yanayotoa huduma muhimu, kwa mujibu wa kifungu namba 76(1) na (2) Cha sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004.”
MWANANYAMALA, AMANA, TEMEKE
Hali ya huduma katika Hospitali ya Amana imeendelea kusuasua kutokana na baadhi ya madaktari kuendelea na mgomo.
NIPASHE ilizungumza na baadhi ya wagonjwa hospitalini hapo ambao walithibitisha kuwepo kwa mgomo na kwamba madaktari wamekataa kuingia wodini kuwahudumia.
Asha Selemani mkazi wa Kondoa, aliyelazwa wodi namba mbili, alisema alifika hospitalini hapo Ijumaa jioni kisha akafanyiwa vipimo na kupatiwa dawa za malaria, akidai anasumbuliwa na homa ya mapafu, hakuna majibu aliyopewa ya vipimo alivyofanyiwa hadi sasa.
Mgonjwa mwingine Nyasebwa Dominick mkazi wa Gongo la Mboto, aliyelazwa wodi namba tatu, alisema tangu afike hospitalini hapo Ijumaa hakuna vipimo vyovyote alivyofanyiwa licha ya kwamba alipatiwa dawa na mpaka sasa hakuna daktari aliyefika kumhudumia.
Naye Richard William mfungwa wa gereza la Ukonga, alisema jana asubuhi alipita daktari mmoja na hakuna huduma aliyotoa kwa wagonjwa kwa hiyo inaonyesha mgomo bado unaendelea.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE hospitalini hapo ulionyesha kuwa wagonjwa wanaosubiri huduma walionekana kuwa wengi ikilinganishwa na idadi ya madaktari waliokuwa wakitoa huduma.
Hata hivyo juhudi za kumpata Mganga Mkuu wa hospitali hiyo ili kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba kutokana na kuelezwa kuwa kwenye vikao.
Katika hospitali ya Mwananyamala, madaktari wa mafunzo ya vitendo na wa kawaida wamegoma kuendelea kutoa huduma hospitalini hapo.
Katibu wa Hospitali hiyo, Edwin Bisakala, aliiambia NIPASHE jana kwamba takribani robo tatu ya madaktari walioko kwenye mafunzo ya vitendo na baadhi ya madaktari wa kawaida wamegoma huku akidai kuzidiwa na kazi kwa madaktari waliopo.
“Madaktari bingwa wapo, madaktari wa kawaida wachache sana hawapo, madaktari wasaidizi wanaopaswa kuwepo zamu wapo, lakini takribani robo tatu ya madaktari wanaohudhuria mafunzo kwa vitendo ni wachache sana wa kawaida wamegoma,” alisema Bisakala na kuongeza kuwa:
“Mapokezi kwa wagonjwa yanaendelea kama kawaida tangu siku ya kuanza mgomo, mpaka sasa kwenye wodi zote kuna wagonjwa 325 ambao wanaendelea kupatiwa matibabu, lakini kuna overworking (kuzidiwa na kazi) kutokana na mgomo huo.”
Aidha daktari mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alizitaja sababu zinazochangia madaktari kugoma ni pamoja na kuzidiwa na kazi akitoa mfano kuwa kuna idadi ya madaktari wa watoto takribani 124 nchi nzima ambayo ni sawa na wastani wa madakari wanne kila mkoa, lakini siyo katika vituo vyote.
Daktari mwingine ambaye naye hakutaka jina lake litajwe alisema wao hawafurahii migomo wala kuona wagonjwa wanateseka na hivyo aliiomba serikali kuboresha mazingira ya kazi ikiwa ni pamoja na kuongeza vitendea kazi na maslahi ya madaktari.
Hata hivyo, John Mauris, mgonjwa aliyelazwa kwenye wodi namba tano kutokana na majeraha kwenye mwili wake, alidai kwamba madaktari waliendelea kutoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa wodini hapo kwa siku ya jana, lakini kwa upande wake alikuwa bado hajaoshwa jeraha lake tangu Jumamosi siku ambayo mgomo ulitangazwa kuanza.
TEMEKE SHWARI
Hata hivyo, katika hospitali ya Temeke utoaji wa huduma kwa wagonjwa mbalimbali wa nje na wodini ziliendelea kama kawaida toka kwa madaktari wa hospitali hiyo pamoja na wauguzi wao na hivyo kuifanya hospitali hiyo kutoathirika na mgomo wa madaktari unaoendelea katika baadhi ya hospitali.
NIPASHE ilifika katika idara za meno, macho, upasuaji, huduma za X-ray na iliwakuta madaktari wakiendelea kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa kama kawaida.
Eunice Elisante mmoja wa wagonjwa aliyekutwa hospitalini hapo alisema amepata huduma nzuri ya matibabu bila tatizo lolote.
Zainabu Ramadhani ambaye alikuwa amempeleka mgonjwa wake alisema baada ya kuwasili hospitalini hapo alipokewa na wauguzi na madaktari na kupatiwa kitanda kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Amani Malima, alisema wao katika hospitali hiyo wanaendelea kuchapa kazi kama kawaida.
“Kama unaovyoona, tunachapa kazi ya kuwatibu wananchi bila tatizo lolote lile; hali kwetu ni nzuri” alisema.
MBEYA - MADAKTARI 61 WAGOMA
Madaktari 61 katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, Hospitali ya Mkoa na Hospitali ya Wazazi Meta za Jijini Mbeya wameendelea na mgomo wao na kusababisha tatizo la upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa.
Mkurugezi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk. Eliuter Samky alisema madaktari 61 waliopo kwenye mafunzo ya vitendo na wale walioajiriwa na serikali wamegoma.
Alisema kutokana na madaktari hao kugoma, hospitali hiyo imelazimika kuwatumia madaktari bingwa wachache wanaoendelea na kazi katika hospitali tatu za Serikali zilizopo mjini hapa.
Dk. Samky alisema anapotokea mgonjwa aliye katika Hospitali ya Mkoa anayehitaji huduma kutoka kwa daktari bingwa, inabidi daktari aondoke Hospitali ya Rufaa kwenda huko kumuhudumia au mgonjwa huyo asafirishwe kwenda Hospitali ya rufaa kumfuata daktari.
Kuhusu wagonjwa kuondolewa hospitalini hapo, Dk. Samky alisema inabidi ndugu wafanye hivyo ili kuokoa maisha ya jamaa zao kwa vile huduma za hospitali hiyo kwa sasa zimedorora kutokana na mgomo.
“Ni kweli baadhi ya ndugu wanawaondoa wagonjwa hospitalini hapa na kuwapeleka katika hospitali nyingine za watu binafsi, hatua hiyo mimi naona ni sahihi ili kuokoa maisha ya watu, kwa sababu hapa huduma zimedorora kutokana na madaktari wengi kugoma,” alisema Dk. Samky.
MWANZA- NDUGU WAONDOA WAGONJWA WODINI
Huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando Jijini Mwanza imeathirika na baadhi ya wananchi wanawaondoa wagonjwa wao hospitalini hapo huku idadi ya wagonjwa wanaokwenda kupata matibabu ikianza kupungua.
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo walisema kimsingi huduma za matibabu zinasuasua tofauti na huko nyuma kabla ya kuanza kwa mgomo.
Mmoja wa wagonjwa hao Majaliwa Hussein (27) aliyelazwa tangu Juni 21 mwaka huu, alisema baada ya mgomo kuanza daktari amepita mara moja tu katika wodi kuwaangalia wagonjwa.
Mgonjwa mwingine Mulusuli Thobias, alisema alipigwa picha ya X-Ray siku ya Ijumaa wiki iliyopita, lakini hadi jana alikuwa hajapelekewa majibu kujua anaumwa nini.
Emmanuel Malilo ambaye anamuuguza mdogo wake Jack Malilo alisema analazimika kuwasaidia baadhi ya wagonjwa katika wodi hiyo kwa kuwapa huduma za hapa na pale kutokana na madaktari kutoonekana wodini hapo.
Katika hali ya kutaka kuweka mambo sawa, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Baraka Konisaga, alifika hospitalini hapo jana na kutoa rai kwa madaktari waliogoma kurejea kazini ili kuepusha madhara zaidi.
Madaktari waliogoma wamesema mgomo wa sasa utakuwa na madhara makubwa kwa sababu serikali imeonyesha dharau kushughulikia madai yao.
Mmoja wa madaktari hao Dk. George Adriano ambaye licha ya kuwepo hospitalini hapo lakini hakuwa kazini, alisema hatua ya serikali kutaka kutumia nguvu au propaganda kushughulikia mgomo huo haiwezi kuzaa matunda.
Alidai tofauti na baadhi ya wananchi na viongozi wanavyofikiri, madaktari wengi wa Tanzania ni wazalendo ndiyo maana hawajakwenda kufanya kazi nje ya nchi ambako kuna maslahi makubwa, lakini serikali imeshindwa kulitambua hilo.
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Bugando Dk. Japhet Gilyoma, alikataa kuzungumza na waandishi wa habari kwa madai kuwa amekwishatoa taarifa kwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
IRINGA NI MGOMO WA SIRI
Madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa wamekuwa na mgomo baridi ambapo wapo waliofika kazini na wengine hawajafika na huduma ni za kusuasua.
Mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo ambaye alizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotoja jina lake, alisema siku chache zijazo hospitali zote za rufaa katika mikoa zitaathiriwa na mgomo huo kutokana na kwamba matabibu wanaofanya kazi katika ngazi hiyo wameamu kutotoa huduma kikamilifu hadi hapo serikali itakapotimiza madai yao ya msingi.
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika wodi za hospitali hiyo walisema huduma zimeanza kuzorota jambo ambalo linawafanya wahisi kama madaktari hao nao wameanza mgomo baridi wa kutotoa huduma.
Zainab Mbijo ambaye ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini mjini Iringa alisema amekaa kwa zaidi ya saa tano katika hospitali hiyo bila kupatiwa matibabu.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa Dk. Robert Mahimbo, alipotafutwa na NIPASHE kuzungumzia hali ya hospitali hiyo kwa sasa endapo madaktari wameungana na wenzao katika kudai madai yao, simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
TANGA, K’NJARO, DODOMA HAKUNA MGOMO
Katika Hospitali za mkoa wa Tanga hali ni shwari kutokana na watendaji hao kuendelea kazi kama kawaida.
Katibu wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tanga Bombo, Adam Lyatuu, alisema madaktari katika hospitali hiyo wanaendelea na kazi kama kawaida na wala hakuna dalili yoyote ya mgomo.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe) mkoa wa Tanga, Jacob Barnabas, alisema mpaka sasa hajapokea taarifa zozote za kuwepo kwa mgomo wa madaktari katika hospitali za Serikali zilizopo mkoani humo.
Katika hospitali ya Rufaa ya KCMC, madaktari walionekana kuendelea na kazi kwa kuwahudumia wagonjwa na hata wagonjwa waliozungumza na NIPASHE walithibitisha kupewa huduma.
Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Kituo cha Afya cha Makole zilikuwa zikiendelea kama kawaida. Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Ezeckiel Mpuya, alisema wao wameendelea na huduma za matibabu kama kawaida katika hospitali yao.
“Sisi tuko shwari madaktari na watumishi wengine wako kazini kama kawaida na hudma zimeendelea kutolewa bila kutetereka,”alisema.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, alipoulizwa kuhusiana na hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali kumaliza mgomo huo, alikataa kuzungumza kwa madai kuwa hakuwa na taarifa rasmi za hali ya hospitali hivyo asingeweza kuzungumza.
Badala yake alisema atatoa tamko leo baada ya kupata taarifa za kina na athari za mgomo kutoka kwenye hospitali ambazo madaktari wake wanashiriki mgomo.
Imeandikwa na Thobais Mwanakatwe, Raphael Kibiriti, Gwamaka Alipipi, Ninaeli Masaki, Nebart Msokwa, Isaya Kisimbilu, Francisco Haule na Mrobezi Yoramu, Dar; Emmanuel Lengwa, Mbeya; George Ramadhan, Mwanza; Godfrey Mushi, Iringa; Lulu George, Tanga na Sharon Sauwa, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment