Kwa niaba ya Tanzania kama nchi (ardhi na taifa) na siyo Tanzania kama watu(watanzania na viongozi), mimi binafsi nasikitika kuwa nchi yetu imebaki njia ya panda. Tanzania(nchi/ardhi) ambayo inawapa(watanzania wanaoishi hapa ndani) na imewapa(wanaoishi huku nje) siyo tu uraia bali makazi na utambulisho wa utaifa bado hawajapata moyo wa kufa na kupona kuiendeleza.
Tanzania inatafuta suluhisho kutoka kwa watu waliozaliwa umo, haijali kuwa bado unaishi hapa ama kwa sasa unaishi huku nje.
Maoni na mawazo mengi yaliyotolewa na watanzania wa nje na ndani katika "Mjadala Mchachu" uliopita "TANZANIA INAHITAJI WATU WAKE KURUDI NYUMBANI KUIJENGA NCHI" yameonesha kila mmoja wetu anataka kushiriki kukamilifu kuijenga nchi yetu lakini pia ni kweli inaonekana kila mmoja anajiuliza tutaanzaje na tutaanzia wapi? Swali ambalo linawafanya watanzania wengi kuonekana kukata tamaa. Kwa maneno mengine nguvu ya pamoja kuchukua hatua madhubuti kuanza kazi ngumu sana inayotukabili ya siyo tu ujenzi mpya wa taifa letu, bali kuliendeleza itatoka wapi?
Watanzania tuwe na moyo wa, hata kama tutaanzia kuishi katika huduma hadimu na hafifu za afya, mabarabara machache na chakavu, mavumbi, mbu, ajira adimu, rushwa/ufisadi, bado tukumbuke nani atufanyie kazi ya kuliendeleza taifa letu? Tanzania (nchi yetu) ni kama mtoto wako wa kumzaa, inabidi upange mikakati ya kumlea vyema kusudi afanikiwe katika maisha ya baadaye. Bila mzazi kumpa mtoto lishe bora, malazi bora, mavazi na kumpa elimu nzuri mzazi atakuwa amemkosea haki yake, na ndivyo watanzania tunachoelekea kukifanya kwa nchi yetu. Mawazo ya baadhi ya watoa hoja kusema wanapenda kuishi nje kwa kuwa huduma ni bure, mafao kibao nk. unaleta wasiwasi kuwa watanzania hatuko tayari kukabiliana na matatizo tulionayo kusudi tuvipe vizazi vijavyo uraisi kidogo kuanza maisha yao kama wenzetu wa ulaya, marekani nk.
Watanzania kumbukeni hakuna kitu kizuri kinachokuja kwa urahisi, na kama kipo mara nyingi kina matatizo makubwa. Kwa upande wangu siyo tu naepuka kupata kitu kirahisi rahisi bali naviogopa pia. Kazi kwetu watanzania, Tutaikana nchi yetu, nchi yetu itatukane sisi ama tuko tayari kupigana na matatizo tuliyonayo kusudi Tanzania na watu wake tuitwe Taifa?
MASWALI YA KUCHANGIA
1. Tanzania itaendelezwaje na itaendelezwa na nani ikiwa kila mmoja anasema maisha ni kivyako?
2. Kweli unaipenda Tanzania kwa moyo na nguvu zako zote?
3. Nini kifanyike kwa vitendo na siyo maneno kupata mwelekeo tofauti na sasa?
4. Wewe binafsi ungekuwa kwenye mamlaka ya uongozi wa nchi yetu ungefanya nini totauti kuwaamasisha watanzania
washiriki kikamilifu kupambana na matatizo tulionao kwa moyo na bila woga.
Tafadhali elekeza majibu yako sehemu ya maoni. Tuanzie hapo kupata ufumbuziwa kurekebisha mwelekeo wetu.
Katika Tanzania ya sasa blogs zinaweza kufahamisha, kuelimisha na kukosoa jamii zaidi kuliko radio na tvs.
2 comments:
Mdau inaonekana una uchungu wa kweli na Tanzania au una kanjaa kanachokusumbua. Nachukulia una uchungu wa kweli. Mdau inaonekana umeshaishi majuu sana kisha umejifunza kuwa pamoja na vitu vizuri vya nje lakini Tanzania pekee ndiyo inakupa utambulisho wako kimataifa, kuiendeleza hatukwepi. Hongera mdau tutafahamu umuhimu wa uzalendo.
Jibu la swali la kwanza; Tanzania itaendelezwa kwa teknologia yetu wenyewe. Tuanze kuvumbua vi-motor na vimashine vidogo vidogo vitakavyotimika katika ukulima wa kisasa (large scale, viwanda vidogo na vikubwa na hii itaanzisha ajira kwa watanzania wengi. Tanzania itaendelezwa na watanzania wenyewe na siyo vinginevyo. Reginald Mengi(IPP) ni mfano wa kuigwa. Naamini anaweza kutugawia siri ya mafanikio yake.
Jibu la swali la pili; Ndiyo (Off Course)naipenda Tanzania kwa moyo na nguvu zote.
Jibu la swali la tatu; Viundwe vikundi vya kujitolea visivyo vya kisiasa viwaelimishe wananchi hasa wa vijijini na miji midogo jinsi ya kuchagua wabunge na viongozi wenye sifa ya kushika nyazifa hizo. Pili kuwakumbusha viongozi wetu kuwa wao wamepewa dhamana ya uongozi kwa wakati huo maalum na wasidhani kuwa wao ni smart kuliko sisi wengine bali wanatuwakilisha kwa kuwa hatuwezi wote kuwa viongozi.
Jibu la swali la nne; Viongozi wa serikali wawe chachu wawe na muda wa kukutana na wataalamu wetu, kama vile ma-engineer, madaktari, maprofesa machuoni, mafundi gereji uswahilini kusudi kutafuta skills na talents ambazo hazitumiki. Kiundwe kitengo cha uvumbuzi na uendelezaji wa teknologia yetu, itengewe bajeti na serikali au bunge, pesa zake zichungwe na wahusika wafanye kazi. Ukiwa kiongozi alafu huna muda wa kukutana na wataalamu basi kuna tatizo.
Post a Comment