ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 25, 2012

Usistaduu, ubrazameni na mapenzi ya Kichina -5

WIKI iliyopita nilieleza kuwa wauza magenge na maduka, wanaingilia ndoa za watu. Nafasi hizo wanazipata kwa sababu ya kutokuwepo ubize kwa wanawake hao. Asili yetu tunapenda utani, hivyo wakitaniana mara mbili, mwanamke anahama kihisia. Keshokutwa asubuhi mume akiondoka, huyu anakimbilia gengeni.
Huu ni mfano katikati ya mada yetu. Mtu wa aina hii akiwaona machangudoa barabarani, atawalaani kupita kiasi. Hata hivyo, mtindo wa maisha yake hauna tofauti na changudoa kutokana na ukweli kwamba mtu mwenye staha na heshima, hawezi kujilimbikizia vidumu. Mume usiku, mchana muuza bucha au houseboy, haijakaa vizuri.

Inabidi kutoa mfano wa aina hii kutokana na ukweli kwamba masistaduu wanaweza kukaa vibarazani na kusogoa kuwa mbona wake za watu wanaojionesha ni watu makini, nao wanacheza sana mechi za nje? Wanadanganywa nao wanadanganyika. Maisha yanaendelea, mke wa mtu anaitwa fuska pasipo yeye mwenyewe kujijua.
Dunia ilivyo ni kwamba huwezi kutoka kimapenzi na mtu halafu ikabaki kuwa siri. Iwe isiwe lazima itavuja. Japo maneno yanaweza yasifike kwa mumewe lakini kwa watu baki watamzodoa au kumsogoa kila anapopita. “Yule ni mke wa mtu lakini tabia zake chafu”
Wapo watakaozungumza: “Yule mwanamke hana kinyaa, ana mume lakini utadhani changudoa kwa jinsi anavyoisaliti ndoa yake.” Wewe hutayajua hayo unayosemwa, utajioni upo vizuri ukiamini unayofanya hayaonekani. Kwa kudhani nyendo zako za siri hazijulikani, utawalaani machangudoa wanaojiuza mitaani.
Hapa namaanisha kuwa wakati tunawaweka sawa masistaduu, inapendeza lile kundi la wanawake wanaojiona wapo makini wakawa mfano wa kuigwa. Waache tabia za mafichoni, hadharani kujionesha ni watu wazuri kimaadili, wakati gizani wao ni wachafu kuliko hata hao wanaoonekana.
Japo natoa mifano mbalimbali, jambo muhimu kwako ni kutambua kuwa ninachokielekeza hapa ni somo kwamba kuna jamii fulani inapotosha tafsiri halisi ya mapenzi. Hii inasababisha maumivu makali kwa watu wanaoyaheshimu. Fikiria wewe unapenda, halafu upo kwenye uhusiano ni yule asiyejua maana ya kupendwa.
Wewe unayaheshimu mapenzi na unayazingatia kwelikweli, hivyo unao utambuzi kwamba tafsiri ya kupenda ni kupendwa. Sasa upo kwenye uhusiano na mtu ambaye hajui kurudisha upendo kwa anayempenda. Anachoamini mapenzi ni mtindo huru, kama vile kwenda sokoni na kuchagua sehemu ya kununua bidhaa zako.
Tunaishi kwenye jamii moja, tunaona jinsi masistaduu na mabrazameni walivyochakachua mapenzi. Watoto wadogo siku hizi nao wanayatenda kama game. Tukielewana tunapeana leoleo. Alichoimba Ali Kiba kwenye Single Boy akimshirikisha Lady Jaydee, hakina tofauti na hali halisi iliyopo.
Kwamba hivi sasa hakuna mapenzi zaidi ya kudanganyana. Kwa hiyo, bora ukimpenda mmalizane leoleo. Hoja inayojengwa ndani ya wimbo huo ni kuwa mapenzi yanaumiza kichwa, unaweza kupenda sana matokeo yake ukawa kama mwendawazimu. Wanamaliza kila mmoja akijisifia alivyo singo.
Unaweza kuona wimbo huo kuwa maudhui yake yanalenga kuivuruga jamii kwenye suala zima la mapenzi. Kwa upande mwingine ni vizuri kupata wana fasihi kama Ali Kiba ili waichambue hali halisi kwa mtindo ambao ameuelezea na Jaydee kwenye Single Boy.
Hata hivyo, kama mshauri wa saikolojia ya mapenzi, sikubaliani na hitimisho la Ali Kiba, badala yake nachochea mabadiliko chanya kwa watu ambao wamemfanya mwanamuziki huyo apate sababu ya kuyaponda mapenzi ya sasa, hivyo kutaka kila mtu awe na mtazamo wa kuwa singo.
Suluhu ni nini
Hupaswi kuishi singo, kwani athari zake zipo. Ukisema huyataki kabisa mapenzi, kuna kundi litakalokuvalisha kesi kuwa mambo yako si mazuri. Naijua vizuri jamii yetu, mwanaume anaweza kuambiwa jongoo wake hapandi mtungi, wakati ushahidi hana.
Ukisema uwe unarukiarukia watu hovyo, kama ambavyo wengine wanafanya (kumalizana leoleo tu), huko ni kupotea sana. Maradhi yamezunguka kila upande, hivyo utajikuta unatengeneza mtandao mkubwa wa ngono bila wewe mwenyewe kujijua.

www.globalpublishers.info

No comments: