ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 16, 2012

11 wafa ajali ya gari


  Wamo baba, wanawe watatu
Watu 11 wamekufa papo hapo wakiwemo wanne wa familia moja na wengine wanane kujeruhiwa vibaya kwenye ajali mbaya iliyotokea jana katikati ya kijiji cha Chibingio na Nyemigota, wilayani Geita mkoani Geita.
Ajali hiyo ilihusisha magari mawili ya abira aina ya Toyota Corolla maarufu kama michomoko, yaliyokuwa yakitokea Geita kwenda Katoro.
Mashuhuda wa ajali hiyo walisema kwamba ilisababishwa na madereva wa magari hayo yaliyokuwa yakifukuzana na kwamba gari la nyuma lilikuwa likitaka kulipita gari la mbele.
Walisema wakati dereva huyo akitaka kufanya hivyo, gari lililokuwa mbele kuongeza mwendo na hivyo madereva wote walishindwa kuzimudu gari hizo hivyo kuserereka na kisha kupinduka baada ya kuacha njia.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Paulo Kasabago, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kwamba watu 11 walifariki dunia eneo la tukio akiwemo dereva wa gari mojawapo.

Alifafanua kuwa kati ya marehemu hao, wanne ni familia moja ya baba na wanawe wanne ambao alikuwa akiwapeleka kuwanunulia bidhaa mbalimbali (shopping).
Alisema wengine wanane walijeruhiwa vibaya wanne kati yao hali zao ni mbaya na walipelekwa Hospitali ya Rufaa Bugando na hali zao zinaelezwa kuwa mbaya.
Alisema maiti za watu wanane zimetambuliwa na tatu bado hazijafahamika na kwamba Jeshi la Polisi mkoani humu linaendelea na uchunguzi wa ajili hiyo.
Magari yaliyohusika kwenye ajali hiyo ni yenye namba T344 BKE iliyokuwa mbele na yenye namba T 813 AZE, ambayo ilikuwa nyuma na zote zilikuwa zikitoka Geita kwenda Katoro.
Ajali hiyo ililazimu viongozi wote wa mkoa wa Geita kufika eneo la tukio akiwemo Mkuu wa Mkoa, Said Magalula, ambaye alipiga marufuku michomoko na Noah kufanya biashara ya usafiri.
Kamanda Kasabago alisema Jeshi la Polisi litafanyia kazi agizo la Mkuu wa Mkoa na kwamba halitaruhusu magari hayo kutoa huduma ya usafiri.
Marehemu wametambuliwa kuwa ni Maria Elisante (18), mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Muganza iliyoko katika wilaya ya Chato, Sarah Eliud (4), Amin Eliud (10,) mwanafunzi Shule ya Msingi Kalangalala, Emilson Eliud (7) na baba yao Eliud Ngovongo mfanyakazi wa mgodi wa Geita.
Wengine ni James Ntungilege (38), dereva wa gari T 344 GPE, Emasafra Benjamin (17), Edward Dotto Juma (25) na watatu wakiwemo wanawake wawili ambao bado hawajatambuliwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: