ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 9, 2012

Dk. Ulimboka aendelea vizuri


Hali ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, aliyelazwa nchini Afrika Kusini, imeendelea kuimarika, ingawa bado yuko chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Katibu wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Edwin Chitage, alisema pamoja na kwamba bado Dk. Ulimboka yuko ICU, lakini hali yake inaendelea kuimarika.



"Tunasubiri ripoti kutoka kwa daktari anayemtibu Dk. Ulimboka ili tufahamu ni kitu gani kinachomsumbua... ingawa daktari wake amesema hajapata ridhaa kutoka kwa mgonjwa wake ya kutoa ripoti hiyo kwa jumuiya yetu," alisema Dk. Chitage.

Mapema wiki iliyopita, baadhi ya vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii, viliripoti kuwa hali yake ni mbaya na kwamba amelazwa ICU.

Kutokana na taarifa hizo kutofautiana, NIPASHE lilikwenda nyumba kwa wazazi wa Dk. Ulimboka eneo la Ubungo Kibangu, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata taarifa za hali yake.

Hata hivyo, mama mzazi wa Dk. Ulimboka, alipoulizwa kuhusu hali ya mwanaye aliyepelekwa Afrika Kusini, hakuwa tayari kusema chochote kwa kudai kuwa tukio lililompata mwanaye hawezi kulizungumzia.

Mama huyo ambaye alikataa kutaja jina lake, alikuwa na hali ya wasiwasi hasa anapokwenda mtu yeyote ambaye familia haimfahamu.

Usiku wa kuamkia Juni 25, mwaka huu, Dk. Ulimboka alitekwa na watu wasiojulikana wakiwa na silaha za moto, ambao walimjeruhi vibaya ikiwemo kumng’oa meno na kucha.

Kufuatia tukio hilo, madaktari wenzake walichangishana fedha, ambapo Jumamosi ya wiki iliyopita, waliamua kumpeleka nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

CHANZO: NIPASHE


No comments: