ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 9, 2012

Slaa, Mnyika wadai wanawindwa


  Wawatuhumu Maofisa Usalama
  Mkuchika, Nchimbi:Hatuna taarifa
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeituhumu serikali kupitia Idara ya Usalama wa Taifa na kudai kwamba  imeanzisha mpango maalum wenye lengo la kuwaangamiza viongozi wake wakuu kwa njia ya kuwawekea sumu katika chakula au kuwatumia makundi ya majambazi.

Madai hayo yalitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho yaliyopo Kinondoni.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi rasimi ya Upinzani bungeni na Mbunge wa Hai, alidai kuwa chama chake kumegundua mbinu hizo alizodai kuwa zinafanywa na serikali kupitia Idara ya Usalama wa Taifa baada ya kupewa taarifa na watu wenye mapenzi mema kutoka serikalini.



"Baadhi ya viongozi wa chama hicho, wameanza kufuatiliwa nyendo zao kwa saa 24. Viongozi wanaolengwa katika hatua hii ya awali ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na hii imetokea hasa baada ya kuwa ametoa kauli bungeni kuhusiana na udhaifu wa serikali, viongozi wa serikali yenyewe na Chama Cha Mapinduzi hali inayoonekana kwamba haikuifurahisha serikali na ndiyo ikaja na mkakati huu," alidai Mbowe.

Alidai kuwa mbali na Mnyika, wengine waliolengwa katika mkakakti huo ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Arusha Mjini kupitia Chadema, Godbless Lema.

Aliongeza kudai kwamba mpango huo unaratibiwa na maofisa usalama wawili aliowataja kwa jina moja moja na kueleza kwamba wao kama chama wanajua kila hatua wanayofanya maofisa hao.

Hata hivyo, Mbowe alisema mpango huo hauwatishi na kwamba wataendelea kusonga mbele katika kusimamia maslahi ya Watanzania.

"Kama lengo la serikali ni kukitisha chama chetu kiondoke kwenye msimamo wake, basi imepoteza mwelekeo, kwani sisi hatutishiki na tutaendelea na juhudi zetu za kusimama na kuwaunga mkono wananchi wakiwemo wafanyakazi wa serikali na makundi mengine kama ilivyokuwa kwa madakatari," alisisitiza.

Aliongeza: “Wametutuhumu kuwa tumeshawishi madaktari wagome wakati  si kweli kwa kuwa hakuna kikao chochote tulichokaa na madaktari hao na kuwashawishi wagome. Dk. Ulimboka amepitia kwenye mateso makali akilazimishwa aseme kuwa Chadema wamewashawishi madaktari wagome, kitu ambacho si cha kweli,” alidai Mbowe.

Aliongeza kwamba wao kama chama cha siasa hawatasita hata siku moja kuwaunga mkono wafanyakazi wa kada zote kuanzia madaktari, walimu na wengine wanapojitokeza kudai haki yao kwa kuwa ni wajibu wao.

Kuhusu suala la madaktari, Mbowe aliishauri serikali kuchukua ushauri uliotolewa na viongozi wa dini unaoiasa kukaa meza moja na madaktari hao badala ya kuwafukuza kwa faida ya taifa kutokana na gharama zinazotumika kumfundisha daktari mmoja na umuhimu wa wataalam hao.

Aliishauri serikali ya CCM badala ya kujiingiza kwenye njia za kutafuta kuwatisha kwa kuwadhuru viongozi wa Chadema kupitia Idara ya Usalama wa Taifa, ingewekeza kwenye kuwaletea maendeleo wananchi na si kupambana na chama chao kinachofanya mambo yake kwa uwazi.

“Inawezekana huenda wanafikiri tuna mambo ya siri tunayoyafanya, katu sisi Chadema siku zote hatuna mambo ya siri, hatuna siri na kamwe hatutafanya jambo lolote kwa siri. Siku zote Chadema inafanya mambo yake hadharani ili wananchi wayaone,” alidai.

Hata hivyo, alisema Kamati Kuu ya Chadema inatarajia kukutana leo kuzungumzia suala hilo.

Aidha, alisema licha ya kuwepo vitisho hivyo, hawatatoa taarifa polisi na kwamba hawatafanya hivyo kwa madai kwamba historia inaonyesha kuwa walishatoa taarifa nyingi polisi zinazohusiana na wanachama wao kuuawa, kupigwa na kuhujumiwa lakini hakuna hata taarifa moja iliyofanyiwa kazi na polisi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Slaa, alidai kwamba amekuwa akifuatiliwa na serikali tangu siku nyingi.

“Kama mtakumbuka, nilishawahi kuwekewa vinasa sauti chumbani kwangu hotelini kule Dodoma, polisi walikuja kuvichukua lakini hadi leo hii hakuna lolote nililoelezwa na kuwa nini kilikuwa kinatafutwa kwangu," alidai Dk. Slaa.

Aliongeza: "Familia yangu vile vile ilishafuatiliwa ambapo mke wangu alishawahi kutaka kudhuriwa ili mimi nisiende kwenye shughuli za kichama kwa kuwa ningebaki ninamuuguza mke wangu.”

Alidai kwamba hata kwenye kadhia ya Dk. Harrison Mwakyembe, yeye pia alikuwa ni mmoja wa watu ambao walilengwa kudhuriwa na serikali kama ilivyotokea kwa Dk. Mwakyembe, lakini hakuwahi kuitwa na polisi kwa ajili ya mahojiano yoyote kuhusiana na taarifa hiyo.

Hata hivyo, alidai kuwa ni muhimu idara hiyo ikafahamu kwamba Chadema inajua kinachofanyika na kupangwa ndani ya idara hiyo.

Dk. Slaa alidai kwamba kitendo cha Idara ya Usalama wa Taifa kujiingiza kwenye mkumbo wa kutaka kudhuru wananchi, hakishangazwi kwa kuwa hata ndani ya idara hiyo kuna baadhi ya watu wasio waaminifu ambao kwenye ufisadi wa Epa walituhumiwa.

MNYIKA AFUNGUKA

Kwa upande wake Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alidai kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anayetoa uhai kwa binadamu na ndiye anayeuchukua anapoamua.

“Nimeshauriana na familia yangu kuhusiana na mpango huo wa serikali na wakanihimiza niendelee kupigania ukweli na  uwajibikaji bila ya kurudi nyuma kwa kuwa ninachofanya ni cha wengi na sauti ya wengi ni sauti ya Mwenyezi Mungu, alidai.

Aliiasa idara ya usalama wa taifa kurejea kwenye michango yake aliyoitoa bungeni kuhusiana na idara hiyo kuwa, kuna maofisa waadilifu na wasio waadilifu ndani ya idara hiyo na akaishauri irejee kwenye wajibu wake wa kulinda usalama wa raia na si wa mafisadi.

LEMA NAYE ATETA

Kwa upande wake Lema, alidai kwamba watu wenye mapenzi mema serikalini walimtanabaisha juu ya umuhimu wa kuchukua tahadhari kwa kuwa kuna mpango wa kumdhuru.

“Katika siku mbili zilizopita, nimekuwa nikifuatiliwa na gari moja aina ya Carina kwa saa 24, popote ninapokwenda, wakati mmoja niliamua kuifuata hiyo gari na jamaa aliponiona ninamfuata, alishusha kioo na kuniambia, kwamba wewe ndiye Godbess Lema,Mbunge wa Arusha Mjini…,” alidai Lema mbele ya waandishi wa habari.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, alipoulizwa kuhusiana na madai hayo ya viongozi wa Chadema, alijibu kuwa hana taarifa na kwamba aliingia jana kutoka mjini Dodoma.

"Sina taarifa, wewe ndiyo unaniambia na waandishi walionipigia leo (jana), nimewaambia waniandikie maswali nitawajibu kwa maandishi kwa kuwa madai ya watu kutaka kuuawa ni mazito," alisema Mkuchika kwa njia ya simu jana.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema hajui chochote.

Licha ya mwandishi kumueleza kilichozungumzwa na Chadema, lakini Dk. Nchimbi, alisisitiza kwamba hana taarifa zozote kuhusiana na madai hayo.

Aidha, kuhusu Chadema kukataa kutoa taarifa za kutishiwa maisha kwa viongozi wake kwa Jeshi la Polisi, Dk. Nchimbi alisema: “Kwa sasa siwezi kuwa na ‘comments (maoni)’ yoyote kwa kuwa sijapata taarifa ya nini hasa walichosema Chadema na kwa hiyo sijui lolote kuhusiana na waliyosema.Nitasubiri basi niangalie taarifa ya walichosema kwenye televisheni na baada ya hapo, nitakuwa kwenye nafasi ya kutoa ‘comments’  zangu,” alisema.

Dk. Nchimbi alisema hawezi kutoa maoni yake kabla ya kusikia walichosema Chadema ili kuepuka majibizano yasiyo ya lazima na chama hicho.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema, alipoulizwa kupitia kwenye simu yake ya kiganjani alisikiliza maelezo ya mwandishi hadi mwisho na lilipokuja suala la kutoa maoni yake alisema:

“Unajua mwandishi, unayeongea naye si IGP ila ni simu yake, lakini ameiacha chumba cha mawasiliano na kwa kuwa namba yako tunayo tayari, basi akija atawasiliana na wewe,” alisema mtu huyo aliyedai kutumia simu ya IGP.

Mwandishi aliposisitiza kwamba ni muhimu kujua maoni ya IGP kuhusiana na madai hayo na kwamba habari hii inabidi ichapishwe, alikata simu mara moja.

Hadi tunakwenda mitamboni, IGP hakupiga simu kama alivyoahidi mtu aliyedai kupokea simu yake ya kiganjani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: