KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod
Slaa amemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa maelezo juu ya fedha na
mali zilizochangwa na Watanzania wakati wa maafa mbalimbali yaliyotokea
hivi karibuni nchini, yakiwamo ya Kilosa, Gongo la Mboto, Dar es Salaam,
vinginevyo ajiuzulu.
Aidha, amemtaka Waziri Mkuu kumwagiza
Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovic Utouh kukagua
hesabu hizo na kutoa taarifa hadharani na endapo atashindwa kuchukua
hatua hizo ndani ya siku 30 Chadema kitachukua hatua nyingine.
Kauli
hiyo ya Dk Slaa ilitolewa wakati wa tathmini ya chama hicho katika
operesheni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) iliyofanyika katika
majimbo saba ya Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana wakati wa kutoa tathmini hiyo, Dk Slaa alisema endapo Waziri
Mkuu atashindwa kuwajibu au akitoa maelezo yasiyoridhisha, ajiuzulu
vinginevyo watamshtaki kwa umma wa Watanzania.
Alisema hali
waliyonayo waathirika wa mafuriko ya Kilosa yaliyotokea miaka mitatu
iliyopita ya kulala sakafuni na familia kuchangia chumba kimoja ni ya
kusikitisha.
Alisema waathirika hao wamekuwa wakiendelea kuishi
katika kambi hizo kwa shida huku utu wao ukidhalilishwa kutokana na
kuishi baba, mama na watoto katika chumba kimoja na kutumia vyoo
visivyokuwa na staha.
Alisema Watanzania wengi walijitokeza kutoa
misaada mingi kwa watu walioathiriwa na maafa ya Gongo la Mboto,
Mbagala na wale waliokumbwa na mafuriko na kuhamishiwa eneo la
Mabwepande, Dar es Salaam.
Alisema katika majanga hayo, Ofisi ya Waziri Mkuu haikutoa hesabu za fedha zilizochangwa wala namna zilivyotumika.
Alisema
haiingii akilini Serikali kuwapatia waathirika wa Kilosa kila mmoja
mabati sita, mfuko mmoja wa saruji, misumari kilo moja na ubao mmoja kwa
ajili ya kujengea nyumba huku wakiwa hawajakabidhiwa viwanja vya
kujengea.
“Kutokana na hali hiyo, Chadema tunamtaka Waziri Mkuu
kueleza fedha, mali na vitu vilivyochangwa na Watanzania vimekwenda wapi
na kwa nini watu hawa wanapata shida huku Waziri Mkuu na viongozi
wengine wakiangalia,” alisema Dk Slaa.
Katibu mkuu huyo
alisisitiza kuwa Chadema kitawaagiza wabunge wake kupeleka hoja bungeni
ya kuitaka Serikali kutoa taarifa za fedha na mali zilizochangwa ili
kuwasaidia waathirika.
Mbio za Mwenge
Kuhusu Mbio za
Mwenge ambazo zimekuwa zikiendeshwa kila mwaka nchini, Dk Slaa alisema
malengo yake yamepoteza misingi halisi iliyowekwa na hayati Mwalimu
Julius Nyerere.
Alisema anachoona ni kwamba hivi sasa zinaeneza
Virusi Vya Ukimwi (VVU) pamoja na kuwanyanyasa wananchi kwa kuwabebesha
mizigo ya michango, badala ya malengo yaliyokusudiwa.
Alisema
katika kipindi cha Mwalimu, mwenge ulikimbizwa nchini ukiwa na maana ya
kueneza upendo pasipokuwa na upendo, amani pasipokuwa na amani, kueneza
mwanga palipo na giza tofauti na ilivyo sasa.
“Hakuna sheria
inayolazimisha mtu kutoa mchango wa mwenge. Mchango wa mwenge ni sawa na
mchango wa harusi au send-off kwa hivyo Serikali iache kuwanyanyasa
wananchi kwa michango hiyo isiyo ya kisheria,” alisema.
Alisema
ikiwa chama chake kitafanikiwa kushika dola mara baada ya Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2015, mwenge huo utapelekwa makumbusho ili watu waweze kufika
na kupewa historia yake.
Tathmini ya operesheni
Akizungumzia
tathmini ya siku 12 ya operesheni hiyo mkoani Morogoro, Mkuu wa M4C,
Benson Kigaila alisema Chadema kimepata mafanikio makubwa ikiwa ni
pamoja na kuingiza wanachama zaidi ya 31,537 kutoka katika vijiji 471
vya majimbo hayo saba.
Kigaila alisema tangu kuanza kwa
operesheni hiyo mkoani Morogoro Agosti 8, mwaka huu chama hicho
kimefungua zaidi ya matawi 100 akisema hiyo itasaidia kuwa takwimu
sahihi za wapiga kura wake.
Alisema katika operesheni ya M4C,
jumla ya kadi 7,605 za vyama vingine zimekabidhiwa kwa Chadema huku
chama hicho kikifanikiwa kuuza kadi zake na kupata kiasi cha Sh15.8
milioni na wananchi wakikichangia kiasi cha Sh17.9 milioni.
Sensa ya Watu na Makazi
Kwa
upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Zanzibar, Said Issa Mohamed
alisema Chadema kinaunga mkono Sensa ya Watu na Makazi na kuwataka
wanachama wake kujitokeza kuhesabiwa.
Mohamed amewataka
wanaChadema na wananchi kwa ujumla kuondoa itikadi zao za kidini,
kisiasa na ukabila katika suala hilo akisema ni muhimu kwa ajili ya
Serikali kuandaa mipango yake ya maendeleo.
Wakati huo huo: Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anatarajia kwenda Marekani wiki hii kwa ziara ya kukiimarisha.
Mbowe
alisema mjini hapa juzi kuwa lengo la ziara hiyo ni kwenda kuhamasisha
na kufungua matawi ya chama hicho kwa kushirikiana na Watanzania
wanaoishi huko.
No comments:
Post a Comment