ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 22, 2012

Fedha za sensa ni balaa



Zikiwa zimebakia siku tatu kufanyika kwa sensa watu na kamazi inayotarajiwa kufanyika Jumapili ijayo, zogo kubwa juu ya malipo kwa makarani wa kazi hiyo imeibuka na kutishia kugomea kazi hiyo.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kumalizika kwa semina ya mafunzo ya wiki moja, makarani hao walilalamikia kupunjwa kwa posho zao tofauti na makubaliano ya kwenye mkataba, ambao kila mmoja alipaswa kulipwa Sh. 245,000.



Mwenyekiti wa kamati ya semina kituo cha  Banana Miti Mirefu katika Manispaa ya Ilala, Mohamed Mcheni, alisema wameshangazwa kwa kitendo cha kulipwa pesa pungufu  Sh. 40,000 tu ambazo zililipwa Agosti 19 na 20, mwaka huu.

“Kama unavyowaona makarani wapo nje kusubiri majibu ili kujua ni lini watalipwa pesa zilizobaki ambazo ni  Sh.105,000,” alisema Mcheni.

NIPASHE ilishuhudia makarani hao wakiwa nje ya madarasa baada ya kugoma kuingia madarasani kwa ajili ya kuapishwa kwa kudai kuwa walicholipwa ni kinyume kabisa cha makubaliano.

Katika kituo cha Buguruni Manispaa ya Ilala, NIPASHE ilishuhudia baadhi ya makarani wakilalamika kutolipwa kabisa huku wakiwa wamehudhuria siku zote za semina.

Aidha, kwenye kituo cha Shule ya Sekondari Zawadi iliyopo Tabata, hali ilikuwa tete baada ya makarani zaidi ya 1,000 kugomea zoezi la kuapishwa kwa madai ya kutaka kulipwa kwanza posho zao mbele ya mawakili waliokwenda kwa ajili ya zoezi hilo.

Asha Bakari, ambaye ni karani, alisema walilipwa Sh. 140, 000  Jumamosi iliyopita na walitegemea kulipwa posho iliyobaki jana, lakini cha kushangaza waliwaona mawakili wamefika kwa ajili ya kuwaapisha, jambo ambalo walilipinga kwa maelezo kuwa wakishaapishwa hawatalipwa tena posho zao.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi, alisema kuwa malalamiko ya makarani hao katika wilaya hiyo ni ya kweli na kuwaomba radhi makarani hao kwa usumbufu walioupata. Alisema usumbufu huo ulisababishwa na Sikukuu ya Idd ambapo fedha zilichukuliwa nusu na leo watalipwa pesa zao zote zilizobaki.

“Makarani katika Wilaya ya Ilala ni 4,500 kati ya hao 1,500 ni vijana ambao hawana ajira, lakini wamepata nafasi katika kufanikisha zoezi zima la sensa,” alisema Mushi.

Alisema makarani ambao hawajalipwa fedha zao ni suala la kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli, lakini alisema hana taarifa kuhusu makarani ambao hawajalipwa.

Katika Wilaya ya Kinondoni, NIPASHE ilishuhudia makarani wa kituo cha Shule ya Sekondari ya Makumbusho wakigoma kuchukua posho pungufu, hali lilyosababisha mtafaruku, kiasi cha kulazimisha polisi kufika kituoni hapo ili kutuliza vurugu.

Hata hivyo, makarani hao walipuuza kauli ya maafisa wa polisi iliyowataka  kuondoka kituoni hapo na kwenda kuchukua posho zao leo, wakidai kuwa hawataondoka mpaka walipwe.

Mmoja wa makarani hao, Selemani Ally, aliiambia NIPASHE kuwa tangu kuanza kwa semina, hawajawahi kulipwa posho zao hata za siku moja na walipohoji waliambiwa ya kuwa watalipwa posho yao yote ya semina jana, lakini cha kushangaza serikali imeshindwa kutekeleza ahadi yake.

“Tatizo hapa ni malipo ya semina, hawa watu hawajatulipa posho hata ya siku moja, tulipohoji tukaambiwa tutalipwa posho ya siku nne juzi, lakini hawakufanya hivyo. Leo (jana) amekuja mhasibu na tukawa tunaitwa mmoja mmoja ili kwenda kuchukua posho,” alisema Ally.

Ally aliongeza kwamba waliamriwa kuingia kwenye chumba cha mhasibu na kuchukua bahasha iliyofungwa na kuamriwa kusaini na kutoka nje haraka, ambapo baada ya makarani kadhaa kuingia na kutoka ndipo wakagundua kuwa bahasha walizopewa zina Sh.140,000 badala ya Sh. 245,000, ambayo ndiyo posho waliyoahidiwa kulipwa.

“Sasa tumeamua kugoma kuchukua hata kiwango hicho walichoamua kutulipa, kwa kuwa leo ni siku ya mwisho ya semina, sasa tusipolipwa leo tutalipwa lini, na hawataki kutueleza ni lini watatulipa, na kwa maana hiyo hatutakubali kuapishwa,” alisema Ally.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Fortnatus Fueme, alithibitisha kuwepo kwa madai hayo na kuahidi kuwa makarani wote watalipwa leo. Aidha, alithibitisha kuwa makarani hao wanastahili kulipwa Sh. 245,000.

UHABA WA VIFAA

Mkoa wa Ruvuma bado unakabiliwa baadhi ya changamoto zikiwemo za uhaba wa vitabu vya mageresho, madodosho na kutokuwalipa baadhi ya malipo ya makarani na wasimamizi wa sensa

Baadhi ya makarani na wasimamizi wa sensa katika Halmashauri ya Manispaa Songea, walisema kuwa pamoja na kwamba siku zimebaki chache, lakini bado kuna changamoto zinazoonyesha ugumu wa zoezi hilo.

 Walisema kuwa katika manispaa ya Songea kuna uhaba mkubwa wa vitabu, mageresho na madodoso na kwamba hata wakati wa mafunzo bado kulikuwa na uhaba wa vifaa

Walifafanua zaidi kuwa hata malipo kwa makarani na wasimamizi wa sensa walilipwa kwa awamu mbili na kwamba malipo kwa  ajili ya kwenda kutambua maeneo ya kuhesabia mpaka sasa fedha hizo hazijatolewa.

Waliongeza kuwa hata posho ya uandikishaji wa daftari la makazi hawana uhakika italipwa lini.

Mratibu wa sensa wa Mkoa wa Ruvuma,  John  Lyakurwa,  alithibitisha kuwa badhi ya vifaa vilishaletwa na kwamba vingine vinatarajiwa kuletwa kwa ndege ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Alisema vitabu vya maregesho ndiyo tatizo kubwa na kwamba wamelazimika kuazima vitabu hivyo kwa Mratibu wa sensa wa Mkoa wa Iringa ambavyo vinatarajiwa kuletwa wakati wowote kuanzia sasa.

Kuhusu madai ya posho za makarani na wasimamizi, alisema fedha zipo na serikali itawalipa, lakini aliwataka wawe na subira.

Aliongeza kuwa posho ya uwandikishaji wa daftari ya makazi imeandaliwa ya siku tatu ambapo wahusika watalipwa Sh. 50,000 kwa siku.

MWANAFUNZI MBARONI 

Mwanafunzi wa mwaka wa pili Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro, Juma Koosa, anashikiliwa na polisi wilayani Korogwe akituhumiwa kutangaza ujumbe wenye kuwakataza wananchi hususani Waislamu kushiriki katika sensa ya watu na makazi itakayofanyika nchini Jumapili ijayo.

Koosa ambaye pia ni Mratibu wa Elimu Kata ya Vugiri alikamatwa akiwa kwenye Msikiti wa Miembeni katika eneo la Mazinde wakati akizungumza na waumini wa Kiisalmu baada ya sala ya adhuhuri juzi.

Licha ya kuhamasisha waumini kugomea sensa hiyo, pia alikuwa akigawa vitabu 15 vinavyohamasisha Waislamu kutii wito wake huo unaopinga sensa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa alikutwa akiwa na nakala za vitabu 15 zenye kuwakataza kuhesabiwa.

Alisema kuwa kukamatwa kwa mtu huyo kulitokana na jitihada za baadhi ya waumini waliyokuwa wakimpinga maagizo yake ambao walitoa taarifa kwa polisi ambao walifika na kumkamata kisha kumfikisha kituo cha polisi Mombo.

 Massawe alisema wakati wa mahojiano, mtuhumiwa kuwa hakujua madhara ya kitendo alichokuwa akikifanya kama ni kinyume cha kisheria za nchi. Mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamni wakati wowote baada ya taratibu kukamilika.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego, anatarajiwa kuanza ziara ya katika kata 24 zinazounda wilaya hiyo kwa lengo la kukutana na wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji.

Hatua hiyo inatokana na ushirikiano mdogo unaotolewa na viongozi hao katika maandalizi ya sensa.

Katibu Tawala Wilaya ya Tanga, Hilda Makwinya, alisema kuwa ofisi yake imeshapanga ratiba rasmi ya kufanya vikao hivyo ambavyo vitakuwa vya ndani na vya hadhara kuanzia kesho.

DC NYUMBA KWA NYUMBA

Mkuu wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Subira Mgalu, ameanza kupita nyumba hadi nyumba kuhamisha wananchi kujitokeza kuhesabiwa.

NIPASHE limeshuhudia mkuu huyo pia nyakati za asubuhi, mchana na jioni akipita katika masoko na kuhamasisha wafanyabiashara kujitokeza kuhesabiwa.

WAISLAMU WATAKIWA KUSHIRIKI


Serikali mkoani Kagera imewataka viongozi wa madhehebu ya dini kuendelea kuhamasisha waumini wao katika kushiriki sensa.

Mratibu wa sensa Mkoa wa Kagera, Peter Milinga, amesema maandalizi ya sensa mkoani Kagera mpaka sasa yamekamilika kwa asilimia 90 na tayari baadhi ya changanoto zilizokuwepo zimetafutiwa ufumbuzi kwa kiwango kikubwa.

Milinga alizitaja baadhi ya changamoto kuwa ni baadhi ya maeneo kutopelekwa vipeperushi vya kuhamasisha juu ya sensa, malipo kucheleweshwa kwa baadhi ya vituo vya semina na baadhi ya wilaya kutopokea vifaa vya sensa.

Alisema kuwa kufikia leo maandalizi kwa ngazi ya mkoa ni ya kuridhisha, ingawa kuna baadhi ya viongozi wa Kiislamu kuwataka waumini wao kutoshiriki sensa.

Maandalizi ya awali kuhusu sensa katika mkoa wa Simiyu yamendelea huku kukiwepo na changamoto baadhi ya maaeneo kuripotiwa watu wake kutotaka kuhesabiwa.

Taarifa kutoa maeneo ya wilaya za mkoa wa Simiyu zimedai kuwa uhamasishaji na elimu imetolewa katika wilaya zote tano za
mkoa kwa makarani wa sense, pia madiwani wa halmashauri hizo nao walipewa semina.

Sheikh Mkuu wa wilaya ya Maswa, Issah Eliasah, katika mikutano yake na waumini wa Kiislamu aliwahimiza washiriki kimilifu katika sensa na kupuuza kampeni za baadhi ya watu wanaowataka waumini wa Kiisilamu wasishiriki.

Sheik huyo alisema kuwa hakuna mahali popote katika kitabu kitakatifu cha Quran kinakataza waumini wa dini hiyo kuhesabiwa.

RC ATOA ONYO

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, ameapa kuwashughulikia watendaji wote watakaobainikka kushindwa kutimiza wajibu wao katika sensa kwa sababu ya kukosa posho.

Dk. Nchimbi aliyasema hayo wakati wakizungumza na wazee wa mkoani Dodoma kuhusiana na sensa ya watu na makazi.

Akizungumzia kuhusiana na changamoto inayolikabili zoezi hilo,  Dk. Nchimbi alisema watu kutokuwa wepesi kuelewa kazi hiyo.

Alisema pia kulikuwa na changamoto ya fedha kutofika kwa wakati katika Wilaya ya Chemba. Hata hivyo, alisema jana makarani wa wilaya yote walipata posho zao.

Kwa upande wake, Mratibu wa Sensa hiyo, mkoani Dodoma, Iddi Muruke, alisema makarani wa dodoso fupi wapatao 3362 na dodoso refu 2962 walipata mafunzo kuhusiana na zoezi hilo. Alisema asilimia 30 ya eneo la mkoa ndilo limelengwa kupitiwa na dodoso refu.

“Tungependa dodoso refu liwe katika maeneo yote lakini kutokana na kuwa na gharama kubwa tumefanya asilimia 30 itakayowakilisha wananchi wengine,” alisema.

WENYEVITI WATUHUMIWA

Baadhi ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji wilayani chato mkoani Geita wametuhumiwa kutaka kukwamisha zoezi la sensa kutokana na madai ya kutengwa tangu mwanzo wa mchakato hadi hivi sasa.

Mkuu wa Wilaya ya Chato, Rodrick Mpogolo, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na madiwani wa halmashauri hiyo kwa lengo la kuwataka kuongeza nguvu ya kuhamasisha zaidi jamii kuhusiana na sensa.

Mpogolo alisema baadhi ya viongozi wanaotaka kukwamisha zoezi hilo ni wenyeviti wa vitongoji  na vijiji ambao wameshaonyesha wazi nia ya kususia sensa kwa madai ya kuwa wametengwa huku baadhi yao wakiuliza watanufaika na nini kutokana na zoezi hilo.

OFISI YA TAKWIMU YAZUNGUMZA

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema sababu inayopelekea kucheleweshwa kwa posho za makarani walioko kwenye semina ya mafunzo ni mlolongo mrefu wa usafirishaji fedha kutoka Hazina hadi katika akaunti za halmashauri pamoja na tatizo la mtandao.

Ofisa Uhusiano wa NBS, Said Ameir, alisema fedha za kuwalipa makarani wa sensa waliopo katika semina ya mafunzo zinatoka Hazina na kufika katika ofisi za NBS na baadaye kupelekwa katika akaunti za halmashauri, jambo linalosababisha kuchukua muda mrefu kumfikia mlengwa.

Alisema kwa sasa tatizo hilo limekwisha kushughulikiwa na ambao hawajalipwa fedha hizo watapewa hivi karibuni na kuwataka wawe na uvumilivu. “Watu wasilalamike, pesa zao zipo, ni matatizo ya mtandao kwenda polepole pamoja na usafirishaji wa pesa hizo,” alisema Ameir.

Aidha, Ameir aliwaonya watu watakaogoma kuhesabiwa wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria ya Takwimu ya 2002 Sura ya 351 kwa kufungwa kifungo cha miezi sita au kutozwa faini ya Sh. 600,000.

“Mtu akitoa taarifa za uongo, watakaokataa kuhesabiwa, karani wa sensa kutoa siri za kaya, kutotoa ushirikiano, kumzuia karani kufanya kazi ataadhibiwa,” alisema Ameir.

Ameir alisema kutokana na kuwepo kwa tetesi kwa baadhi ya watu kugomea zoezi hilo la kuhesabiwa  na kuleta vurugu siku ya sensa, karani ataongozana na msimamizi wake pamoja na mwenyekiti wa serikali za mitaa ili kuimarisha ulinzi kwa karani wa sensa.

Imeandikwa na Samson Fridolin, Leonce Zimbandu, Gwamaka Alipipi na Aziza Adinani, Dar;  Sonyo Mwenkale, Korogwe; Lulu George, Tanga; Kibuka Prudence, Bukoba; Anceth Nyahore, Simiyu na
Gideon Mwakanosya, Songea.
 
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

my godness CCM mafisadi mmeisha mega fedha za sensa walai 2015 mwisho wenu