Rais Jakaya Kikwete, aliondoka nchini
jana kwenda Maputo, Msumbiji kuhudhuria Mkutano wa Mwaka wa Wakuu wa
Nchi Wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) unaoanza
leo.
Kwenye mkutano huo wa siku mbili, Rais Kikwete anatarajiwa kuchaguliwa
rasmi kuwa Mwenyekiti wa Chombo Maalum cha Sadc cha Kusimamia Masuala ya
Siasa, Ulinzi na Usalama (Troika).
Kwa sasa Troika inaundwa na Tanzania, Afrika Kusini na Zambia.
Miongoni mwa mambo ambayo wakuu hao wa nchi wanachama wa Sadc watajadili
ni pamoja na hali ya siasa na usalama katika eneo la Sadc na hasa
katika nchi za Madagascar na Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC) ambazo zote mbili ni wanachama wa Sadc.
Sadc ina nchi wanachama 15 ambazo ni Tanzania, Angola, Botswana, DRC,
Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Mozambique,Namibia, Shelisheli,
Afrika Kusini, Swaziland, Zambia na Zimbabwe.
Wakati huo huo, Rais Kikwete ametuma salamu za rambirambi kuomboleza
kifo cha ghafla cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, Athuman Ramadhan Chamuya, kilichotokea
usiku wa kuamkia jana.
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, ametuma salamu hizo kwa
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Tanga, Mussa Shekimweri, akimweleza kuwa
amepokea taarifa za kifo kwa huzuni na mshtuko.
“Chamuya ametutoka katika kipindi wakati uongozi wake katika Wilaya ya
Handeni ulikuwa bado unahitajika sana. Nakutumia wewe Mwenyekiti wa Mkoa
salamu zangu za rambirambi. Kupitia kwako natoa mkono wa pole na
rambirambi kwa familia ya ndugu Chamuya. Aidha, nawapa pole wana-Handeni
wote na wana-CCM wa wilaya hiyo,” alisema.
Na katika hatua nyingine, Rais Kikwete, jana alipokea hati za
utambulisho za mabalozi wa India na Hispania ambao wataziwakilishi nchi
zao hapa nchini.
Akizungumza na Balozi wa India, Debnath Shaw, baada ya kupokea hati
yake ya utambulisho katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu, jijini Dar es
Salaam, Rais Kikwete, amemhakikishia balozi huyo kuwa ni dhamira ya
Serikali yake kukuza zaidi uhusiano kati ya Tanzania na India.
“Tanzania na India zimekuwa na uhusiano mzuri sana na muda mrefu sana.
Tumekuwa na uhusiano kati yetu na pia tumeshirikiana kwenye taasisi
mbalimbali za kimataifa ikiwamo ya Kundi la Nchi 77 na kwenye Umoja wa
nchi zisizofungana na upande wowote,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza: "Siyo tu kwamba uhusiano kati yetu umekuwa mzuri sana, lakini
pia Tanzania imenufaika mno kutokana na uhusiano huo. India imekuwa
chimbuko kubwa ya uwekezaji katika Tanzania. India pia imekuwa ni soko
kubwa la bidhaa za Tanzania. Tungependa kuona uhusiano huu unakua
zaidi.”
No comments:
Post a Comment